RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amemtumia
salamu za pongezi mshambuliaji wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa TP
Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Samatta kwa
kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.
Magufuli alituma salam hizo jana kupitia Wizara ya Habari, Michezo,
Utamaduni na Sanaa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari, Dk
Magufuli alimtumia salamu za pongezi Waziri wa Wizara hiyo, Nape Nnauye
afikishe salamu zake za pongezi kwa Samatta.
“Rais Magufuli amemtaka Waziri Nnauye amfikishie salamu zake za
pongezi kwa mchezaji huyo, ambaye pia anaichezea TP Mazembe,” imesema
taarifa hiyo ikiongeza kuwa tuzo hiyo imejenga heshima kwa Samatta na
Tanzania.
Katika taarifa hiyo, Magufuli amewasihi wachezaji wa soka wote na
wadau wa mchezo huo kuongeza juhudi kuuendeleza mchezo ili upige hatua
zaidi kimaendeleo. Samatta alitwaa tuzo ya mchezaji bora juzi usiku
iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) katika sherehe
zilizofanyika Abuja, Nigeria.
Mchezaji huyo alikuwa akipambana na wachezaji wengine wawili ambao ni
Robert Kidiaba Muteba (wa TP Mazembe na Congo) na Baghdad Bounedjah
(Algeria & Etoile du Sahel).
Samatta alipata pointi 127, mbele ya mchezaji mwenzake wa TP Mazembe,
kipa Kidiaba wa DRC aliyepata pointi 88, wakati mshambuliaji wa Etoile
du Sahel ya Tunisia na timu ya taifa ya Algeria, Bounedjah alipata
pointi 63.
Mchezaji huyo wa Tanzania ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza
wa Afrika Mashariki kushinda tuzo kubwa ya Afrika. Mafanikio hayo
yamekuja baada ya kuiwezesha Mazembe kutwaa taji la tano la Ligi ya
Mabingwa Afrika, huku akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake manane.
Mshambuliaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang ameshinda tuzo ya
Mwanasoka Bora wa Afrika kwa mara ya kwanza na kumshinda Yaya Toure wa
Man City na Ivory Coast aliyekuwa akisaka tuzo hiyo kwa mara ya tano.
Aubameyang wa Borussia Dortmund ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 26,
amewaangusha Toure aliyekuwa anashikilia tuzo hiyo na Andre Ayew wa
Ghana. Amekusanya pointi 143, saba zaidi ya Toure wakati Ayew ameshika
nafasi ya tatu kwa kupata pointi 112.
Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi ametoa pia pongezi zake kwa mchezaji huyo. Naye, Kocha wa Yanga,
Hans Pluijm amempongeza Samatta kwa tuzo hiyo akisema kuwa, itawatia
moyo wachezaji wengine wa ndani wa Tanzania kubadilika katika mtizamo wa
kucheza soka la kulipwa.
“Tuzo hiyo itawafanya wachezaji wengine wa Tanzania kucheza katika
kiwango cha juu sio tu katika kujipandisha wao wenyewe, bali kuisaidia
timu ya taifa hasa katika mashindano ya kimataifa,” alisema.
SERIKALI imesema ubomoaji na uondoaji wananchi waishio katika Bonde
la Mto Msimbazi utaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na
usumbufu kwa wananchi. Watakaohusika na uhamishwaji huo, sasa ni wale tu
ambao makazi yao yapo ndani ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia
bondeni na kwenye kingo za mto.
Imesisitizwa, awamu hii ya ubomoaji, itajikita katika Bonde la Mto
Msimbazi tu na watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za
umma, zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo,
hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga.
Maamuzi hayo yamefikiwa juzi baada ya mawaziri watatu wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI);
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii.
Mawaziri hao walifanya mkutano wa kutathmini uhamishaji wa wakazi wa
mabondeni katika jiji la Dar es Salaam. Waliamua kuwa watumishi wa umma
waliowamilikisha wakazi maeneo hayo, watachukuliwa hatua za kinidhamu na
kisheria.
Taarifa ya maamuzi hayo ilitolewa jana na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Pia, taarifa hiyo ilisema mawaziri hao wameamua katika siku tatu zijazo,
serikali itaanza kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji
umefanyika.
Mawaziri hao walibainisha kuwa serikali itaheshimu amri za mahakama
kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi wa mabondeni, lakini
pia itafuatilia kesi hizo ziishe haraka ili taratibu zinazofuata
zifanyike.
“Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake
wanaoendesha zoezi hili kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa, na
kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwemo wanaoweka alama za X zaidi
ya mita zilizowekwa kisheria,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali imeanzisha dawati la malalamiko
katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupokea malalamiko
au maswali kuhusu zoezi hilo.
Walisema nyumba na majengo yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa
kwa sheria zinazotekelezwa katika ubomoaji huo hayatabomolewa,
isipokuwa tu pale maisha ya wakazi yapo hatarini.
Vile vile ilisema wanaoishi katika makazi hayo, watapewa miongozo ya
hatua za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa, kwani serikali haina
dhamira ya kubomoa hoteli kubwa za siku nyingi zilizo karibu na fukwe
katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa hoteli hizo, watapewa masharti na
miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria.
Pia, serikali inaweka utaratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi
zake ili hatua za utekelezaji wa sheria za nchi, zisiwe chanzo cha
taharuki katika jamii. “Serikali haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake
kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi.
Lakini, pia haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika maeneo
ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yapo hatarini,” ilisisitiza
taarifa hiyo. Itakumbukwa kwamba katika mafuriko ya mwaka 2011, wananchi
49 waishio mabondeni walipoteza maisha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya Hewa, mwaka huu
zinatarajiwa kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea miaka ya hivi
karibuni. Tathmini ya ubomoaji huo iliyotolewa ripoti kwa mawaziri hao,
ilieleza kuwa hadi sasa wananchi katika nyumba 774 wamehama na nyumba
hizo kubomolewa.
Taarifa hiyo ilieleza pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa kuhama,
uhakiki kuhusu uhalali wa makazi anayoishi hufanywa. Kutokana na uhakiki
huo, jumla ya wakazi 20 walikuwa na hati halali za makazi na wakazi 119
walikuwa na leseni za makazi za muda mfupi, hivyo hawakuhamishwa.
Nchi ina kingo za mito na mabonde na maeneo mengi hatarishi, ambamo
watu wanaishi kinyume cha sheria, huku wakiharibu mazingira na
kuhatarisha maisha yao, lakini kutokana na uhaba wa makazi, hali ni
mbaya zaidi katika mabonde ya jiji la Dar es Salaam, hasa bonde la Mto
Msimbazi.
Taarifa hiyo ilisema sababu za kufanya usafishaji wa mabonde na mito
katika jiji la Dar es Salaam na mazingira yanayozunguka, unalenga
kunusuru maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Eneo la Bonde la Mto Msimbazi, lilitangazwa ni eneo hatarishi kuishi
binadamu tangu mwaka 1949 na baadaye 1979, hivyo usafishaji huo utapanua
uwezo wa mito ya Dar es Salaam kupitisha maji ya mvua kwa kasi kubwa na
kupunguza uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa wakati wa mvua nyingi.
Taarifa hiyo ilisema kabla ya nyumba kubomolewa, taasisi
zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba anayokaa mkazi ina nyaraka za
umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo nyaraka hizo zina uhalali wowote.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo nyumba ambazo zimethibitika kuwepo katika
maeneo yasiyostahili, ndizo zinawekwa alama X kuashiria kwamba wakazi
wanapaswa kuhama au kubomolewa, baada ya hapo mkazi hupewa muda wa
kubomoa na kuhama mwenyewe.
“Kutokana na utaratibu huu, sehemu kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni
zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa wenyewe, baada ya hapo alama
huwekwa kuonesha mpaka wa bonde,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Pia, taarifa hiyo ilieleza kwamba imebainika sehemu kubwa ya wakazi
wa mabondeni ni wapangaji huku wamiliki wanakaa sehemu nyingine salama.
Suala la Mchungaji Rwakatare Taarifa ya mawaziri hao pia ilieleza kuhusu
suala la Mchungaji Getrude Rwakatare.
Ilisema mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) amefukuzwa kazi Januari 6 mwaka huu na taarifa zake
zimekwishafikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
kutokana na tuhuma za kufanya udanganyifu kwa niaba ya Baraza, kwa lengo
la kumlinda Mchungaji huyo wa kiroho.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais imeshafungua upya kesi mahakamani
kuanzia Desemba 29 mwaka jana, kuomba “makubaliano” kati ya mwanasheria
huyo wa NEMC na Mchungaji Rwakatare, yawekwe pembeni kwa sababu
yalipatikana kwa njia ya udanganyifu.
Taarifa hiyo ilisema Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake mahali
ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi
katika eneo la miti ya mikoko, kinyume na sheria tatu muhimu.
Ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza, jitihada za
kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za serikali za mitaa, lakini
ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali. NEMC ilipoingilia kati na
kutaka kubomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani na wakati
kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye
mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, Mei 11 mwaka jana
aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya
Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali kwa niaba ya Baraza,
kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
Ilielezwa kuwa makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu
Mei 13 mwaka jana, kisha Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa
miezi mitano hadi Oktoba mwaka jana, yalipogundulika na mtumishi
mwingine wa Baraza.
Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (DART) Taarifa hiyo
ilisema mkutano wa mawaziri hao, ulielezwa kwamba Sheria ya Mazingira
Kifungu 57 (2) inatoa nafasi ya kutolewa ruhusa kwa miradi au shughuli
zenye maslahi ya taifa kufanyika katika maeneo ya mabondeni.
Hivyo, waziri mwenye dhamana ya mazingira anaruhusiwa kutoa miongozo
ya namna ya shughuli hizo, zinavyoweza kufanyika bila kuathiri
mazingira. “Mradi wa DART ulipata kibali hicho na una mkataba na Baraza
la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya
mazingira, zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo,” ilisema sehemu ya
taarifa hiyo.
Mawaziri walitaka kufahamu hayo kutokana na hoja inayozungumzwa
kwamba wananchi wanaondolewa katika maeneo ya kuishi mabondeni, lakini
mradi wa DART umeachwa.
SERIKALI imesema haitosita kuwafungulia mashtaka na kuwapeleka
mahakamani ifikapo Machi 30, mwaka huu, wazazi ama walezi wote
watakaoshindwa kupeleka watoto wao shuleni ili kupata elimu ya msingi na
sekondari.
Aidha, imepiga marufuku kwa jamii kutumia jina la ‘watoto wa
majumbani’, badala yake waitwe wasaidizi hao ‘wasichana wa kazi’ au
‘vijana wa kazi’. Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Dar es Salaam jana.
Alisema hayo ili kuhamasisha wazazi na walezi juu ya watoto kujiunga
na shule za msingi na sekondari kwa mwaka huu 2016. Kuhusu kuwafungulia
wazazi mashtaka, alisema serikali inaamini kuwa ikiwa inataka kujenga
taifa lililoelimika ni lazima kuwekeza kwenye elimu, hivyo ni wajibu wa
kila anayehusika kuhakikisha anatimiza wajibu wake.
“Elimu ndio njia bora ya kuwajengea watoto wetu msingi imara wa
maisha yao…serikali haitosita kuchukua hatua za kisheria kwa wazazi au
walezi ambao watazembea, kumficha, kumtorosha au kuzuia mtoto kuanza
masomo ya shule za msingi na sekondari,” alisema Ummy.
Alisema serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
itawafungulia mashtaka na kuwapeleka mahakamani wazazi na walezi wote
watakaoshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwapeleka watoto shule, kwani
hata Sheria ya Mtoto Namba 2 ya mwaka 2009 Kifungu cha 8, inaelekeza
kuwa ni wajibu wa mzazi kuhakikisha mtoto anapata elimu.
Waziri Ummy alisema Kifungu cha 14 kinatamka kuwa ni kosa la jinai,
kushindwa kutimiza wajibu huo na adhabu yake ni faini isiyozidi Sh
milioni 5 na kifungo kisichozidi miezi 6; au vyote kwa pamoja.
Alisema pia wazazi na walezi, wahakikishe kuwa watoto wanaoendelea na
masomo ya shule ya msingi na sekondari, wanahudhuria masomo yao kwa
ufanisi, kwa kuwa serikali haitarajii kuendelea kuona utoro wa watoto
shuleni kutokana na sababu zinazoweza kuepukika.
Kuhusu kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa watoto wanaoanza masomo,
alisisitiza kuwa wazazi, walezi na jamii kuhakikisha kila mtoto mwenye
umri wa kuanza elimu ya msingi yaani darasa la kwanza na elimu ya awali,
kujiunga na shule kwa muda uliopangwa na kuhudhuria masomo ipasavyo.
Kuhusu kuwepo kwa michango mbalimbali katika baadhi ya shule wakati
huu wa maandalizi ya shule, alisema serikali imeshatoa mwongozo stahiki.
Waziri huyo alisisitiza kwamba sio ada peke yake iliyofutwa, bali hata
michango yote na tayari serikali imekwishatoa fedha za kugharimia elimu
bure na zimekwishapelekwa katika shule zote nchini.
Kwa ujumla, walimu wakuu hawatakiwi kutoza mchango wa aina yoyote,
kama vile ya ulinzi, maji, umeme, uzio, fagio, jembe, ndoo na mingineyo,
kwani fedha za kugharimia elimu ya bure zitatumika pia kwenye masuala
hayo yote
Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa Makatibu wakuu na Manaibu Katibu wakuu wa wizara mbalimbali.
Aidha,
Dkt Magufuli pia amemteua Eliakimu Maswi kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na kutengua uteuzi wa Naibu Kamishina
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Lusekelo Mwaseba.
Miongoni mwa Makatibu walioteuliwa ni pamoja na nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, ambaye amebaki Balozi Ombeni Sefue.
Baadhi
ya Makatibu waku hao waliochaguliwa ni pamoja na Mhandisi Mussa
Iyombewa ameteuliwa katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Ofisi ya Makamu wa Rais anakuwa Mbaraka A. Wakili.
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano waliochaguliwa ni Mhandisi Joseph.
Nyamuhanga (Katibu Mkuu – Ujenzi), Dokta Leonard Chamuliho (Katibu Mkuu -
Uchukuzi) na Profesa Faustine R. Kamuzora (Katibu Mkuu - Mawasiliano).
Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni Dokta Yamungu Kayandabira,
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ni Maimuna Tarishi.
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanakuwa ni Dokta
Mpoki Ulisubisya atakayesimamia Afya na Sihaba Nkinga - Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Wizara ya Nishati na Madini ni Profesa Justus W. Ntalikwa, Wizara ya Mambo ya Ndani ni Jaji Meja Jenerali Projest A. Rwegasira.
Wizara
ya Fedha na Mipango anabaki kuwa Dokta Silvacius Likwelile , Wizara ya
Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa ni Dkt Aziz Mlima.
Huku Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akiteuliwa Job D.
Masima.
BAADA ya Mtibwa Sugar kupata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Azam, Kocha
Mecky Maxime amemlaumu mwamuzi wa mchezo huo akidai aliwabeba wapinzani
wao.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi juzi, bao pekee la Azam lilifungwa na John Bocco.
Akizungumza baada ya mchezo huo Maxime alisema mwamuzi Ngole Mwangole
ambaye alikuwa akichezesha mchezo huo alikuwa akitafuta namna ya kuipa
ushindi Azam.
“Ukiangalia kwa mfano faulo iliyotolewa kwa Azam na Mwangole haikuwa
ya haki, wanadai Bocco alitendewa madhambi na Salim Mbonde katika eneo
la hatari, lakini ukiangalia halikuwa kosa,” alisema.
Alisema kikosi chake kilicheza vizuri mechi hiyo isipokuwa mchezo
uliharibiwa na mwamuzi huyo na kuvuruga baada ya kupata kipigo hicho.
Maxime alisema mara nyingi waamuzi wamekuwa wakiharibu mpira hata kama
timu imeanza vizuri.
“Timu zote zilicheza vizuri inavyotakiwa lakini refa tu aliharibu
mpira, alikuwa anatafuta kitu na ndio alichokifanya kwa sababu mchezaji
wangu ndio alianza kushikwa,” alisema.
Alieleza kuwa waamuzi imekuwa tatizo la muda mrefu na wanachangia
kuua soka nchini kutokana na kufanya makosa yanayojirudia bila
kuchukuliwa hatua yoyote.
Alisema halalamiki kwa kuwa amefungwa kwani ni sehemu ya mchezo isipokuwa afungwe kihalali.
YANGA na Azam FC zinatarajia kuondoka leo kwenda Zanzibar kwa ajili
ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza
keshokutwa mpaka Januari 13 kwenye uwanja wa Amani mjini Zanzibar.
Akizungumza na gazeti hili jana Meneja wa Yanga, Hafidh Salehe
alisema timu yao inaondoka na wachezaji wote isipokuwa Nadir Haroub
ambaye ni majeruhi. “Mchezaji ambaye hataungana na sisi ni Haroub peke
yake ambaye ni majeruhi,” alisema.
Katika michuano hiyo, Yanga imepangwa Kundi B pamoja na Azam FC,
Mtibwa Sugar na Mafunzo, wakati Kundi A lina timu za Simba, ambao ni
mabingwa watetezi, URA ya Uganda, JKU na Jamhuri ya Pemba.
Yanga watafungua dimba kwa kucheza na Mafunzo keshokutwa, mchezo
ambao utafuatiwa na mechi kati ya Mtibwa Sugar na Azam FC usiku.
Mabingwa watetezi, Simba SC watateremka uwanjani kwa mara ya kwanza
Januari 4, kumenyana na Jamhuri usiku, mchezo ambao utatanguliwa na
mechi kati ya URA na JKU.
Nusu fainali zitachezwa Januari 10, wakati fainali itachezwa Januari
13 sambamba na kilele cha sherehe za Kombe la Mapinduzi 2016.
WAKATI makatibu wakuu wateule na manaibu wao wanaapishwa leo Ikulu
jijini Dar es Salaam, baadhi ya wasomi wamesema uteuzi wao ambao
ameufanya Rais John Magufuli unalenga kuisaidia nchi iweze kuingia
kwenye uchumi wa Viwanda.
Profesa Emrod Elisante wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) alisema
kwamba uteuzi huo ni mzuri kwani umezingatia utaalamu zaidi. Alisema
lazima wizara ziwe na wasimamizi madhubuti ambao wataisaidia nchi kuwa
yenye viwanda.
“Nikiwaangalia watu kama Dk Chamriho (Leonard, Katibu mkuu Uchukuzi)
Profesa Mkenda (Adolf, Katibu mkuu katibu Mkuu Biashara na Uwekezaji)
hawa ni watu makini na ni watendaji wazuri naamini wataisaidia nchi,”
alisema.
Alisema iwapo watapewa malengo na rais, wana uwezo wa kuyatekeleza
hasa kuifanya Tanzania iwe sekta ya viwanda kama alivyoahidi Rais
Magufuli wakati wa kampeni.
Profesa Elisante alisema licha ya nchi kuwa na changamoto mbalimbali
kama za kifedha na rasilimaliwatu, lakini alisema uteuzi huo umejaa
wataalamu ambao wengi wamepelekwa kwenye fani zao.
“Unajua hata waliopita ni wazuri, ila tatizo waliingia kwenye siasa,
Rais Magufuli akiweza kuwadhibiti hawa wasiingie kwenye siasa na
wakafanya kazi yao kwa weledi na kujua malengo ya wizara na nchi naamini
tutachomoka,” alisema.
Naye Mwanaharakati za haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa alisifu
uteuzi wa makatibu wakuu hao kwa maelezo kuwa umewapeleka watu katika
fani walizosomea.
“Mfano Profesa Mchome (Sifuni ambaye ni Katibu mkuu wizara ya katiba
na sheria) yule ni mwanasheria aliyebobea naamini ataisaidia nchi kwa
kutumia taaluma yake,” alisema Olengurumwa.
Alisema kitendo cha Rais Magufuli kujaza wataalamu kama maprofesa na
madaktari katika Serikali yake kunaonesha kuwa anathamini wataalam hao
na angependa kuona wanatumia taaluma yao kuisaidia nchi.
“Utakuta katika wizara kwa mfano ya Madini, kuanzia Waziri hadi
makatibu wakuu ni profesa na daktari, wakikaa pamoja wanaweza kufanya
vizuri lakini pia wanaweza kufanya vibaya,” alisema Olengurumwa.
Alisema dhamira ya rais ni nzuri, hata hivyo alikosoa wingi wa
makatibu wakuu hao hasa uteuzi wa manaibu makatibu wakuu kuwa haukuwa na
maana kwani kila kitengo na idara kina mkurugenzi ambaye kama katibu
mkuu hayupo anaweza kufanya kazi zake.
“Alipunguza baraza la mawaziri tukafurahi, lakini amerudi nyuma kwa
kuleta makatibu wakuu wengi tofauti na alivyotangaza kuwa makatibu wakuu
pia wangepungua, kwa hiyo tuko kule kule,” alisema Olengurumwa.
Naye Katibu Mkuu mteule wa Afya katika wizara ya Afya,Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya amesema ameupokea
uteuzi wake kwa mshituko mkubwa kwa kuwa ni jambo ambalo hakuwahi
kulifikilia.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake ya Ukurugenzi wa
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dk Ulisubisya alisema uteuzi wake
umekuja kwa ghafla huku akiwa na mipango aliyokuwa amejiwekea ya
kuendeleza hospitali hiyo.
Alisema mawazo yake yote ilikuwa ni kujipanga kuhakikisha anatekeleza
majukumu aliyokuwa ameachiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii majuma mawili yaliyopita, Dk Donan Mbando aliyefanya
ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo.
Dk Ulisubisya alisema agizo lingine lilikuwa kuhakikisha hospitali
hiyo inaanzisha Chuo Kikuu kwa ajili ya kuongezea taaluma kwa madaktari
na kuboresha huduma za dharura na kupunguza foleni kwa wagonjwa, mambo
ambayo tayari alianza kuyafanyia kazi na kuyawekea mikakati.
Wakati huo huo, leo Rais Magufuli anawaapisha makatibu wakuu na
manaibu katibu wakuu wa wizara mbalimbali aliowateua juzi. Kazi ya
kuwaapisha inafanywa leo Ikulu na kwa hatua hiyo, Rais atakuwa
amekamilisha kazi ya kupata watendaji wa ngazi za juu katika wizara
mbalimbali, ambazo ni moja ya vyombo vinavyotegemewa kuleta maendeleo ya
watanzania ikiwa kila mmoja kwa nafasi yake, atatimiza wajibu wake.
Imeandikwa na Shadrack Sagati, Dar na Joachim Nyambo, Mbeya.