Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amefanya uteuzi wa wakuu wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara, ambapo kati yao
13 ni wapya, 7 wamebakizwa katika vituo vyao vya kazi, 5 wamehamishwa
vituo vya kazi na 1 amepangiwa Mkoa Mpya wa Songwe.
Uteuzi huo umetangazwa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Mussa
Ibrahim Iyombe leo tarehe 13 Machi, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam.
Wakuu wa Mikoa walioteuliwa ni kama ifuatavyo;
Mh. Paul Makonda - Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.
Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Elias Kyunga - Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu - Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga - Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Brigedia Jeneral Mstaafu Emmanuel Maganga - Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Mh. Godfrey Zambi - Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Dkt. Steven Kebwe - Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Kamishna Mstaafu wa Polisi Zerote Steven - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Mh. Anna Malecela Kilango - Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Mhandisi Methew Mtigumwe - Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Mh. Antony Mataka - Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
Mh. Aggrey Mwanri - Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Mh. Martine Shigela - Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Mh. Jordan Mungire Rugimbana - Mkuu wa Mkoa Dodoma.
Mh. Said Meck Sadick - Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.
Mh. Magesa Mulongo - Mkuu wa Mkoa Mara.
Mh. Amos Gabriel Makalla - Mkuu wa Mkoa Mbeya.
Mh. John Vianey Mongella - Mkuu wa Mkoa Mwanza.
Mh. Daudi Felix Ntibenda - Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Mh. Amina Juma Masenza - Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Mh. Joel Nkaya Bendera - Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Mh. Halima Omary Dendegu - Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Dkt. Rehema Nchimbi - Mkuu wa Mkoa wa Njombe.
Mhandisi Evarist Ndikilo - Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Mh. Said Thabit Mwambungu - Mkuu wa Mkoa Ruvuma.
Luteni Mstaafu Chiku Galawa - Mkuu wa Mkoa wa Songwe (Mkoa mpya).
Wakuu wote wa Mikoa walioteuliwa, wataapishwa Jumanne tarehe 15 Machi, 2016 saa 3:30 Asubuhi Ikulu, Jijini Dar es salaam.
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe, yupo katika wakati mgumu kutokana na wajumbe wa Baraza Kuu na
wabunge wenye ushawishi kumtaka amteue Waziri Mkuu wa zamani, Frederick
Sumaye, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Hii inakuwa mara ya kwanza kutokea katika historia ya kuasisiwa kwa
chama hicho kikuu cha upinzani kwa wajumbe wa Baraza Kuu kumshawishi
Mwenyekiti kumteua mtu anayefaa kushika wadhifa huo.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu, linalotarajiwa kuketi leo wanaotajwa
kujipanga kumshawishi Mwenyekiti kumteua Sumaye kuwa Katibu Mkuu ni
Profesa Mwesiga Baregu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na
Mbunge wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa.
Wengine ni pamoja na Makamu Mwenyekiti Bara, Profesa Abdallah Safari,
Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa, Anthony Komu na Benson Kigaila
na Katibu Mkuu Baraza la Wanawake (Bawacha), Grace Tendega.
Katika orodha hiyo pia wamo wabunge wenye ushawishi mkubwa ambao ni
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Mbunge wa
Ukonga, Mwita Waitara.
Katika orodha hiyo yumo Mbunge wa zamani wa Ilemela, Ezekia Wenje na
baadhi ya waliokuwa wagombea ubunge wenye ushawishi mkubwa ndani ya
chama.
Hadi jana Profesa Safari hakuwa amehudhuria vikao vya Mwanza kutokana na kile kilichoelezwa kukabiliwa na matatizo mbalimbali.
Juzi Lissu aliweka wazi sifa za kiongozi aliyekuwa akimtaka, jambo
ambalo lilitafsiriwa na wachambuzi wa mambo kwamba alikuwa akimuelezea
Sumaye.
Naye mmoja wa wajumbe ambaye hakupenda jina lake litajwe anayemuunga
mkono Sumaye ashike nafasi ya Katibu Mkuu, alisema ukiondoa sifa
alizotaja Lissu za kumtaka Katibu Mkuu anayeweza kuzungumza na
Watanzania, vyama vya Ukawa, ndani na nje ya nchi wakamsikiliza,
nyingine ni mtu aliyeingia Chadema kwa kutofuata cheo.
“Hakuna mwingine zaidi ya Sumaye, ambaye alijiunga na chama hiki
wakati ambao nafasi nyingi zilikuwa zimeshanyakuliwa na wanachama
wengine,” alisema mjumbe huyo.
Sababu kubwa ya wajumbe kumtaka Sumaye inaelezwa kutokana na kubaini
kuwepo kwa mpango wa Mwenyekiti, Mbowe kumtaka Salum Mwalimu, anayekaimu
nafasi hiyo.
WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge amewasimamisha kazi
kupisha uchunguzi vigogo tisa wa Kampuni ya Maji Safi na Taka (Dawasco)
na kutaka aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Jackson Midala
kusakwa na kuchunguzwa na ikibainika alihusika kwenye ubadhirifu wa
maji, afikishwe mahakamani.
Kadhalika,Waziri Lwenge ameitaka Bodi ya Dawasco, kuchunguza tuhuma
za wizi wa maji zinazofanywa na baadhi ya watendaji wa kampuni hiyo kwa
kuwaunganishia maji bure kampuni na viwanda kadhaa jijini Dar es Salaam
na kulipwa ujira kila mwisho wa mwezi na viwanda hivyo.
Waziri Lwenge alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati
alipotembelea Dawasco kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe, kuona
utendaji wao na kuzungumza na watumishi hao.
Pia ameitaka bodi hiyo kuchunguza Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na
kampuni nyingine pamoja na viwanda jijini Dar es Salaam kama wana
akaunti za maji ya Dawasco na kwamba madai ya kuwa wao wana visima vyao
vya maji, lazima ukweli upatikane.
Alisema kama kampuni inasema ina visima vyake binafsi vya maji, ni
lazima wawe na kibali walichopata kutoka Wizara ya Maji, kinachowaruhusu
wao kuchimba na kinaonesha kiwango cha maji, na kwamba kuna madai mengi
ya kampuni na viwanda kuwa na visima vyao, ila wizara haifahamu.
“Kama unadai una kisima cha maji cha kwako kibali kinatolewa na
wizara yangu, sasa yapo madai mengi viwanda vinasema vinatumia maji yao,
ila zipo taarifa kwamba wanajificha kwenye hilo na ukweli ni kwamba
wanaiba maji ya Dawasco, sasa lazima mchunguze hayo,” alisema Lwenge.
Waliosimamishwa kazi ni Meneja Rasilimali Watu, Mvano Mandawa, Meneja
Ufuatiliaji na Tathmini, Reinary Kapera, Teresia Mlengu, Emmanuel
Guluba, Peter Chacha, Fred Mapunda, Reginald Kessy, Jumanne Ngelela na
Bernard Nkenda.
“Sehemu kubwa ya upotevu wa maji ni wizi unaofanywa na wezi ambao ni
baadhi ya viwanda na kampuni kubwa kwa kushirikiana na watendaji wa
Dawasco, tuna taarifa na kila mwisho wa mwezi wako kwenye ‘payroll’
wanaenda kuchukua malipo, hawa ni majipu lazima yatumbuliwe,” alisema
Waziri Lwenge.
Mara baada ya kusomewa taarifa fupi ya utendaji kazi wa Kampuni hiyo
kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja, Waziri
Lwenge alitoa maagizo hayo na kusema pamoja na Kampuni kuwa na malengo
mazuri, lakini ni lazima ifanyiwe mabadiliko ili kupata watendaji
waadilifu.
Alisema upotevu wa maji hivi sasa ni asilimia 47 na kwamba maji hayo
yanapotea katika mazingira tatanishi na kuikosesha kampuni hiyo mapato.
Strabag Alitoa mfano mzuri wa Kampuni ya Ujenzi wa Barabara ya Strabag,
ambayo ilipewa zabuni ya kujenga barabara za mradi wa Mabasi Yaendayo
Haraka (Dart), kwamba tangu kampuni hiyo ianze kufanya kazi hadi sasa,
haijalipa Dawasco bili ya maji iliyotumia.
“Strabag walifanya wizi wa maji, wamejenga barabara lakini hakuna
malipo yoyote waliyofanyika Dawasco, wanadaiwa zaidi ya Sh bilioni 2.9
pamoja na faini na natoa siku 14, wawe wamelipa vinginevyo wakamatwe
wafikishwe mahakamani.
Waziri Lwenge alisema Serikali haiwezi kufanya kazi na wabadhirifu
ambao wako ndani ya taasisi, kampuni au mashirika yake na kusisitiza
kuwa ni lazima watendaji wasio waaminifu waondolewe ili kuleta ufanisi
nchini.
“Tunafanya mageuzi ili tufanye kazi kwa ufanisi na lazima tuwe na
watendaji waadilifu na wenye maadili, si wanaoangalia maslahi binafsi,”
alisema Lwenge. Waziri Lwenge alitoa wiki mbili kwa bodi hiyo kufanya
uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo na zile za wateja wakubwa wa Dawasco
kutokuwa na akaunti za maji, ili kuthibitisha ukweli wa madai hayo.
Maagizo mengine ni kuitaka Dawasco ifikapo Juni, mwaka huu
kuhakikisha wamefanikiwa kupunguza upotevu wa maji kwa asilimia 30 na
ifikapo 2020 upotevu huo uwe chini ya asilimia 20.
Awali Ofisa Mtendaji wa Dawasco, Luhemeja alisema changamoto kubwa ya
Dawasco ni upotevu wa maji na kubainisha katika maeneo 10 wanayohudumia
maji Dar es Salaam na Pwani, Magomeni ni eneo korofi kwa wizi wa maji.
Alisema eneo hilo hivi sasa limebainishwa na wameweka mtandao ambao
kuanzia mwisho wa mwezi huu, utabaini wezi wote lakini pia hatua
nyingine walizochukua ni kuweka vituo vya kuuza maji kwenye eneo korofi,
vinavyosimamiwa na jamii ya eneo husika.
Alisema kwa miezi kadhaa sasa, tangu kuanza kwa huduma hiyo wameweka
vituo 47 vya kuuza ambavyo vimefungiwa mita na wauzaji hutakiwa kulipa
Dawasco bili ya maji baada ya kuwauzia wateja wadogo wadogo.
Ofisa Mtendaji huyo mpya wa Dawasco, alisema kwa kipindi cha muda
mfupi tangu aingie kwenye kampuni hiyo, wamefanikiwa kuongeza mapato ya
maji kutoka Sh bilioni 2.9 mwaka jana hadi kufika Sh bilioni 7.1 Januari
mwaka huu.
Aliongeza kwamba lengo lao ifikapo Juni mwaka huu, ni kukusanya Sh
bilioni 12 kwa mwezi na hiyo ni kutokana na kuweka mifumo imara na
dhabiti ya kufuatilia mita za maji na masharti waliyopewa mameneja wa
maeneo husika ya kampuni hiyo.
Dawasco hivi sasa ina wateja waliounganishiwa mita zaidi ya 151,000
na lengo lao ni kuongeza idadi ya wateja baada ya kuongeza uzalishaji na
usambazaji wa maji hasa baada ya kuimarika kwa mitambo miwili ya maji
ya Ruvu Chini na Juu.
TIMU ya soka ya Simba na Mbeya City leo zinashuka dimbani kwenye
viwanja viwili tofauti kusaka pointi tatu muhimu katika mfululizo wa
mechi za Ligi Kuu bara. Simba itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC kwenye
Uwanja wa Taifa Dar es Salaam wakati Mbeya City itakuwa mwenyeji wa
Stand United kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.
Wekundu hao wa Msimbazi huenda wakapanda kileleni tena iwapo
watafanikiwa kuwafunga Ndanda Fc katika mchezo huo kwa kuwa watafikisha
pointi 51 na kuishusha Yanga yenye pointi 50.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Simba ilikaa kileleni kwa siku mbili
kabla ya Yanga juzi kupanda na kumpiku kufuatia ushindi wake wa mabao
5-0 dhidi ya African Sports ya Tanga. Simba, Yanga na Azam FC
zinatofautiana kwa pointi chache kiasi kwamba mmoja akishinda, mwingine
anashuka.
Simba ina uwezekano wa kushinda mchezo wa Ndanda, kwani katika mchezo
wake wa raundi ya kwanza ilishinda bao 1-0 ugenini mjini Mtwara. Hali
itakuwa mbaya kwa Ndanda kama itakubali kichapo kwa mara nyingine kwani
licha ya kuwa katika nafasi ya nane, ina pointi 24 ambazo hazitoshi
kuihakikishia kubaki salama kwenye msimamo wa ligi kwa kuwa timu
zilizoko chini yake zinaweza kupanda kutokana na kutofautiana pointi
chache.
Kwa upande wa Mbeya City, huenda ikafanya vizuri leo baada ya
kuonesha kiwango bora chenye mabadiliko katika mchezo dhidi ya Simba
wiki iliyopita. Licha ya kufungwa mchezo huo, walicheza vizuri isipokuwa
inayumbushwa na ubutu wa safu yake ya ushambuliaji.
Pengine kwa vile inacheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wanaweza
kutumia faida hiyo katika kufanya vizuri na kufuta machungu ya kufungwa
na timu hiyo ya Shinyanga bao 1-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza.
HOMA ya pambano la raundi ya kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika kati
ya Yanga na APR ya Rwanda, imezidi kupanda, kiasi cha kila moja kutamba
kumshikisha adabu mpinzani wake.
Tayari makocha wa klabu hizo, Hans van der Pluijm wa Yanga na Nizar
Khanfir wa APR aliyeweka rekodi ya kuwa mwarabu wa kwanza kufundisha
soka Rwanda baada ya kuanza kazi rasmi jana, ameelezea utayari wake
kushinda mechi ya Jumamosi wiki hii huko Kigali, Rwanda.
Khanfir amekaririwa jana kuwa, ameshawaona Yanga kupitia video
mbalimbali na kwamba anataka kuwafunga Jumamosi. “Lengo letu ni kushinda
huo mchezo,”amesema na kuongeza; “Nimeona baadhi ya video zao na
tutaendelea kuwachambua katika siku chache zijazo kuelekea kwenye
mechi”.
Kwa ujumla, Khanfir amesema malengo yake makuu katika miezi sita ya
mwanzo ni kuiwezesha timu kutetea ubingwa wa Rwanda na pia kuifikisha
mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Mtaalamu huyo wa Tunisia aliongoza
mazoezi yake ya kwanza APR jana Uwanja wa Kicukiro akisaidiwa na kocha
aliyemkuta kazini, Emmanuel Rubona.
“APR ni timu kubwa Rwanda na ina heshima kubwa Afrika na pia ina
wachezaji wengi katika timu ya taifa, ambacho ndicho kilichonivutia mimi
kukubali kazi hii,” amesema Khanfir. “Wachezaji ni vijana wadogo na
timu ina uwiano mzuri ambao unafaa vizuri katika falsafa yangu.
Tunaitaka kuipeleka timu katika kiwango kingine.
Ni wajuzi na tunataka kuongeza ufundi zaidi, lakini zaidi ya hapo
nimevutiwa na timu kwa ujumla,” amesema. Wakati Khanfir akisema hayo,
Pluijm kwa upande wake amesema anatambua wanakwenda Kigali kwenye mchezo
mgumu wa ugenini dhidi ya APR, lakini watapambana wasipoteze.
“APR ni timu nzuri na watakuwa wamejiandaa vizuri, lakini sisi tuko
vizuri, tutakwenda kupambana tusipoteze mchezo, ili tumalizie vizuri
mchezo wa nyumbani,”amesema. Yanga SC inatarajiwa kuondoka leo nchini
kwenda Kigali kwa ajili ya mchezo huo, unaotarajiwa kuwa mkali na wa
kusisimua.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezeshwa na marefa wa Malawi Jumamosi
Uwanja wa Amahoro, Kigali Rwanda. Duncan Lengani anatarajiwa kupuliza
filimbi, wakati washika vibendera watakuwa Clemence Kanduku na Jonizio
Luwizi.
Mchezo wa marudiano wiki moja baadaye Dar es Salaam, utachezeshwa na
marefa wa Shelisheli; katikati Bernard Camille na pemebeni watakuwapo
Eldrick Adelaide na Gerard Pool.
Mchezo wa kwanza utafanyika mjini Kigali, Rwanda Machi 12 kabla ya
timu hizo kurudiana Dar es Salaam Machi 19 na mshindi wa jumla atakutana
na mshindi wa mchezo mwingine wa raundi ya kwanza, kati ya Al Ahly ya
Misri na Recreativo de Libolo ya Angola mwezi ujao.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako ameingilia kati mgogoro wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St.
Joseph Dar es Salaam, waliogomea kufanya mitihani na kuwataka warejee
madarasani wakati matatizo yao yakishughulikiwa.
Wanafunzi hao walikuwa katika siku ya tatu ya mgomo wao jana ambapo
pamoja na mambo mengine walikuwa wakilalamikia mapungufu yaliyopo chuoni
hapo, ikiwa ni pamoja na maabara za kufanyia mafunzo kwa vitendo,
matatizo ya kiutawala, mitaala ya kufundishia pamoja na ada.
Profesa Ndalichako aliwasili chuoni hapo jana asubuhi na kukagua
mazingira ya kufundishia ya chuo hicho kwa kutembelea maabara zote
chuoni hapo na kisha kwenda kuzungumza na utawala, Serikali ya wanafunzi
na mwisho alihutubia wanafunzi wote.
Ndalichako baada ya kuzungumza na pande zote mbili aliagiza wanafunzi
hao warejee madarasani kuendelea na mitihani yao na kuutaka uongozi wa
chuo uyafanyie marekebisho mapungufu ya kiutawala yaliyojitokeza.
Aidha ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), chini ya Katibu
Mtendaji wake, Profesa Yunus Mgaya kufuatilia na kuchunguza kwa makini
madai ya wanafunzi hao juu ya kuwepo kwa wahadhiri wasio na sifa
zinazotakiwa.
RAIS John Magufuli amesema anatamani mafanikio ya nchi ya Vietnam
kiuchumi na kubainisha kuwa ziara ya Rais wa nchi hiyo, Truong Tang Sang
nchini, ni fursa na changamoto kwa watanzania kujifunza mambo mengi,
yatakayosaidia kukuza pia uchumi wa Tanzania.
Aidha amehamasisha Watanzania kuchangamkia fursa na rasilimali
zilizopo nchini katika kujiinua na kuimarisha nchi yao kiuchumi. Alisema
Tanzania ni miongoni mwa nchi tajiri kwa rasilimali na fursa nyingi,
ingawa bado iko nyuma kimaendeleo. Kwa upande wake, Rais Sang amesema
nchi yake na Tanzania zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya
biashara, kilimo, viwanda na uvuvi lengo likiwa ni kuhakikisha nchi zote
zinanufaika kwenye ushirikiano huo.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari na marais hao Ikulu
Dar es Salaam jana, Dk John Magufuli alisema ni wakati sasa wa Tanzania
kujifunza kutoka kwa nchi hiyo ya Vietnam ambayo pamoja na kukabiliwa
na vita ya muda mrefu, imefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi
wa kati. “Ukweli ni kwamba ziara ya Rais Sang nchini kwetu ni muhimu
sana na imekuja kwa wakati muafaka.
Mwaka 1976 Rais wa Vietnam alikuja nchini na alichukua mbegu ya
korosho na kuipeleka nchini kwake, na leo hii Vietnam ni moja ya nchi
zinazoongoza kwa kuzalisha korosho duniani,” alisema. Alitaja mafanikio
mengine ya nchi hiyo ni pamoja na kuwa na uchumi wa kati, licha ya
kukabiliwa na mapigano ya muda mrefu. Ilipata uhuru wake mwaka 1945 na
ilidumu kwenye mapigano hadi Julai 2, mwaka 1976.
Alisema mwaka 1977 mapato ya kila raia wake yalikuwa ni dola 100,
lakini sasa imefanikiwa kupandisha mapato hayo na sasa kila raia wa nchi
hiyo mapato yake ni dola 2000 kwa mwaka na imepunguza kiwango cha
umasikini kwa asilimia 50. “Sisi tangu mwaka 1960 bado tuko kwenye nchi
masikini, kwa hiyo hii ni changamoto kwa nchi yetu. Tunatakiwa kujifunza
kuondokana na hali hii.
Wao uzalishaji kwa mchele wanalima mara tatu kwa mwaka, sisi tunalima
mara moja tu na inawezekana uzalishaji wetu ni mdogo sana,” alisema.
Alisema nchi hiyo pamoja na kuchukua mbegu ya korosho nchini, ndio nchi
inayoongoza kwa kuzalisha korosho duniani, wakati Tanzania ndio iliyotoa
mbegu hiyo, zao hilo badala ya kuzalishwa kwa wingi ndio uzalishaji
wake unafifia.
“Samaki sina uhakika kama walichukua huku, lakini leo hii Vietnam ni
wazalishaji wa samaki wakubwa sana. Lakini kwa nchi yetu ambayo ina
maziwa 21 na mito kila mahali na bahari lakini uzalishaji wa samaki uko
chini…” “Tuna ng’ombe zaidi ya bilioni 22 hadi bilioni 23 nafikiri
tunaweza kuwa wa pili barani Afrika baada ya Ethiopia, lakini ngozi zetu
za viatu hapa tunaagiza nje.
Kwa hiyo kwa hili watanzania tunatakiwa tusiogope kujifunza kwa wale
waliotutangulia ili na sisi nchi yetu iweze kufika mahali pazuri,”
alisisitiza Dk Magufuli. Alisema ujio wa Rais Sang pamoja na ujumbe wake
wa zaidi ya mawaziri takribani 20 na wafanyabiashara ni wakati pekee wa
Watanzania na wa Vietnam, kuimarisha ushirikiano uliokuwepo kwa zaidi
ya miaka 50 sasa kuhakikisha uhusiano unaleta maendeleo kwa pande zote.
“Ziara hii ni muafaka kwetu sisi watanzania kujenga uhusiano mzuri na
nchi ya Vietnam ili kuweza kujifunza na sisi tuweze kufikia lengo letu
la kuwa nchi ya kipato cha kati,” alisema. Pamoja na hayo, Rais Magufuli
alisema katika mazungumzo yake na Rais wa Vietnam alipata mwaliko wa
kutembelea nchi hiyo mwakani. “Kwa kweli mwaliko huu nimeupokea na
ninajisikia kuthaminiwa na kuheshimiwa sana,” alisema.
Kwa upande wake, Rais Sang alisema anajisikia fahari kuona uhusiano
kati ya Tanzania na nchi yake unaimarika. Alisisitiza kuwa uhusiano na
ushirikiano huo utaleta maendeleo ya dhati baina ya nchi hizo mbili.
Alipongeza serikali kupambana dhidi ya umasikini kwa kusisitiza kuwa
inafanya vizuri kiuchumi kwani ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo
uchumi wake unakua kwa kasi.
“Kama rafiki wa karibu tunavutiwa na maendeleo yenu hasa katika
kupambana na umasikini lakini pia ukuaji wa kasi wa uchumi wenu. Katika
mazungumzo yetu na Rais Magufuli tumezungumzia masuala mbalimbali ya
maendeleo, ikiwemo kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kilimo,
biashara na viwanda,” alisema rais huyo. Aidha, alisema uhusiano wa nchi
hizo mbili ni wa muda mrefu, kwani pamoja na umbali wa kijiografia
Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na
Vietnam.
Alisema ziara hiyo ni moja ya njia za kudumisha na kuboresha zaidi
uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili. Rais huyo alisema
kwenye mazungumzo yake na Magufuli, wamekubaliana kushirikiana katika
maeneo yatakayonufaisha nchi zote. Maeneo hayo ni kilimo, biashara,
viwanda na mawasiliano. Pia walisaini mikataba ya kutowatoza kodi mara
mbili wawekezaji na wafanyabiashara wanaowekeza katika nchi hizo.
Aidha Rais huyo alisema katika kikao chake na Rais Magufuli pamoja na
mawaziri wa nchi zote mbili wamekubaliana kuanzisha tume ya pamoja
itakayosimamia masuala ya uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo
mbili. Aidha marais hao walizungumzia masuala ya kimataifa ambapo wote
kwa pamoja walikubaliana suala la kuhakikisha amani na utulivu linapewa
kipaumbele na mataifa yote duniani.
“Tulikubaliana kuwa nchi zote zina wajibu wa kuhakikisha suala la
amani linapewa kipaumbele, ikiwemo na mataifa ya kimataifa kuwa mstari
wa mbele katika kuhamasisha na kutuliza vurugu zinazoibuka katika nchi
mbalimbali,” alisema. Alisisitiza kuwa amemwalika Rais Magufuli
kutembelea Vietnam wakati wowote. Tayari Marais wastaafu Benjamin Mkapa
na Jakaya Kikwete, walishafanya ziara katika nchi hiyo wakati wa utawala
wao.
Rais Sang aliyeongozana na ujumbe wa watu 51 ataendelea kuwepo nchini
kwa ajili ya kumalizia ziara yake katika maeneo mbalimbali, ikiwemo
kutembelea Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).