SAKATA la rushwa ya Dola za Marekani milioni 600, linalohusisha Benki
ya Standard ya London Uingereza, jana lilichukua sura mpya baada ya
kufikishwa mahakamani kwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Harry Kitilya, akikabiliwa na mashitaka mbalimbali,
ikiwemo utakatishaji wa fedha.
Washitakiwa wengine waliounganishwa katika kesi hiyo ni pamoja na
mrembo wa zamani wa Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Uwekezaji wa Benki ya
Stanbic, Shose Sinare na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa benki
hiyo, Sioi Graham Solomon. Mashitaka mengine yanayowakabili katika kesi
hiyo mbali na kutakatisha fedha, ni pamoja kutumia nyaraka za kughushi
na za uongo kujipatia isivyo halali Dola za Marekani milioni 6, sawa na
Sh bilioni 12 za Tanzania.
Mbele ya Hakimu Mwandamizi, Emilius Mchauru washitakiwa hao walikana
mashitaka hayo na kurudishwa rumande mpaka Aprili 8 mwaka huu, wakati
mahakama itakapokutana kusikiliza shauri kuhusu dhamana yao. Upande wa
utetezi, ukiwakilishwa na mawakili Dk Ringo Tenga na Semu Anney,
waliomba mahakama itoe dhamana kwa wateja wao.
Hata hivyo, upande wa Mashitaka ukiwakilishwa na wanasheria
waandamizi wa Serikali; Oswald Tibabyekomya na Christopher Msigwa pamoja
na Mwanasheria wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru),
Stanley Luwoga walipinga dhamana hiyo kwa madai kuwa kesi za
utakatishaji fedha hazina dhamana.
Awali upande wa mashitaka uliieleza mahakama kwamba, katika tarehe
tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013, katika Jiji la Dar es Salaam,
washitakiwa hao watatu walipanga pamoja kwa kushirikiana na watu
wengine ambao hawakufikishwa mahakamani hapo, kutenda kosa la kujipatia
fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.
Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 katika Makao Makuu ya Benki ya
Stanbic Tanzania Limited yaliyopo wilayani Kinondoni, mshitakiwa Sinare
akiwa na nia ovu, alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya Benki ya
Standard ikiwa na tarehe ya Agosti 2, 2012.
Kwa mujibu wa madai hayo, Sinare alieleza katika maombi hayo kuwa
Benki ya Standard ya London kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic ya
Tanzania, watatoa mkopo unaofikia Dola za Marekani milioni 550 kwa
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa gharama ya asilimia
2.4 ya mkopo huo, wakati akijua kuwa gharama hiyo si kweli.
Mahakama ilielezwa kuwa Agosti 13, 2012, mrembo huyo wa zamani wa
Tanzania, aliwasilisha taarifa hiyo ya kughushi katika Wizara ya Fedha
iliyopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam. Imedai kuwa Septemba 20, 2012
katika Benki ya Stanbic, Sinare alitengeneza barua ya uongo ya kuelezea
mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550, ikieleza kuwa Benki ya
Standard PLC kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic, zitatoa mkopo huo kwa
Serikali kama wakikubaliwa.
Upande huo wa mashitaka uliendelea kudai kuwa, Sinare aliwasilisha
barua hiyo ya uongo katika Wizara ya Fedha kwa lengo hilo hilo. Kwa
mujibu wa madai hayo, Novemba 5, 2012 katika Benki ya Stanbic jijini Dar
es Salaam, washitakiwa wote watatu, wakiwa na nia ovu, walitengeneza
makubaliano ya uongo kwa lengo la kuonesha kuwa benki imeipa kampuni ya
Enterprise Growth Market Advisors (EGMA) Limited, kazi ya kushughulikia
mkopo huo.
Lengo la washitakiwa hao kwa mujibu wa madai hayo, lilikuwa
kufanikisha mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya
Tanzania, ambapo EGMA alitarajiwa kuonekana kuwa muongozaji wa
mazungumzo ya kupata mkopo huo. Upande huo wa mashitaka ulidai kuwa
Machi 2013 jijini Dar es Salaam, Kitilya, Sinare na Sioi, wakiwa na
lengo ovu walifanikiwa kupata Dola za Marekani milioni 6, sawa na Sh
bilioni 12, wakidai kuwa fedha hizo ni malipo ya kazi iliyofanywa na
EGMA Limited.
Utakatishaji fedha Watatu hao pia wameshitakiwa kwa utakatishaji
fedha unaodaiwa kufanyika kati ya Machi 13 na Septemba mwaka jana.
Wanadaiwa kushiriki kutakatisha Dola za Marekani milioni sita kwa
kuzihamisha kwenda katika akaunti tofauti, kuzitoa katika akauti hizo na
kuziweka katika akauti zingine tofauti zinazomilikiwa na EGMA Limited
katika Benki ya Stanbic Tanzania Limited na Benki ya KCB Limited.
Mahakama imeelezwa kuwa hivi karibuni Benki ya Standard imelipa Dola
za Marekani milioni 33 baada ya kukiri kushindwa kuzuia rushwa katika
suala hilo. Mbunge kortini Katika hatua nyingine, Takukuru jana
ilimfikisha Mahakamani Mbunge wa Sumwe, Richard Ndassa (pichani), ambaye
pia ni mjumbe wa Kamati Mtaji na Uwekezaji kwa kosa la kushawishi na
kuomba rushwa ya Sh milioni 30, kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15 (i)(a) na (2).
Taarifa ya Takukuru kwa vyombo vya habari, imedai kuwa Mbunge huyo
akiwa mjumbe wa Kamati hiyo, alimwomba rushwa hiyo Mtendaji Mkuu wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Felchesmi Mramba ili amsaidie
kuwashawishi wajumbe wengine wa Kamati Mtaji na Uwekezaji kupitisha bila
kipingamizi taarifa ya Tanesco kwa mwaka 2015/16.
Mbunge huyo amefunguliwa kesi namba 118/2016 na alisomewa mashitaka
hayo na Wakili wa Takukuru, Dennis Lekayo akishirikiana na Emmanuel
Jacob katika Mahakama ya Kisutu mbele ya. Hakimu Emirius Mchauro.
Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kupata mdhamini mmoja na
kulipa Sh milioni 10 na uchunguzi wa shauri hilo bado unaendelea huku
kesi ikitarajiwa kutajwa tena Aprili 18, 2016.