WAFAMASIA wawili, mmoja wa hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Iringa na mwingine wa hospitali ya wilaya ya Mufindi pamoja na
watuhumiwa wengine wawili waliokuwa viongozi wa kijiji cha Ilula Mwaya wilayani
Kilolo wamefikishwa mahakamani kati ya Januari na Machi mwaka huu wakituhumia
kwa makosa mbalimbali ya rushwa.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi ya
kipindi hicho, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa
wa Iringa, Eunice Mmari alisema watuhumiwa hao wanne wamefikishwa mahakamani
kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Aliwataja wafamasia hao kuwa ni Lucas
Mwandi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na Selemani Fulano wa hospitali
ya wilaya ya Mufindi, na Deogratias Vangiliasas aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji
cha Ilula Mwaya na Robert Kisaka aliyekuwa afisa mtendaji wa kijijiji hicho.
Azungumza na wanahabari ofisini kwake
jana, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa
Iringa, Eunice Mmari alisema wafamasia hao wanashitakiwa kupitia kesi namba 53/2016
na kesi namba 39/2016 kwa makosa ya wizi wa mali ya umma wakiwa mtumishi wa
umma kinyume na kifungu cha 270 cha sheria ya kanuni ya adhabu iliyorekebishwa
mwaka 2002.
Kuhusu waliokuwa viongozi wa kijiji
hicho, alisema nao wanashitakiwa kwa makosa ya wizi wa mali za umma kupitia
kesi namba 23/2016, kinyume na sheria hiyo ya rushwa kifungu namba 28, 29, 30
na 31.
Mmari alisema katika kipindi hicho cha
Januari hadi Machi, Takukuru pia imepokea malalamiko 28 ya rushwa na 14 kati
yake yamefunguliwa majadala ya uchunguzi, malalamiko tisa yanafanyiwa uchunguzi
wa awali, huku malalamiko matano yakifungwa baada ya kukosekana kwa ushahidi.
Alikitoa mchanganuo wa mamalamiko hayo
alisema afya iliongoza kwa kuwa na malalamiko saba, serikali za mitaa, vijiji
na kata (6), elimu (3), ardhi (2), sekta binafsi (1), Tanroads (1), Ushirika na
Kilimo (2), Polisi (1), Ujenzi (1) na sekta binafsi (2).
Akizungumzia mwamko wa wakazi wa mkoa wa
Iringa kuyaripoti matukio ya rushwa katika taasisi yao, Mmari alisema; “mwamko
ni mdogo sana ikilinganishwa na mikoa mingine.”
Alisema Takukuru inaamini kuwepo kwa
makosa mengi yanayoangukia katika sheria ya rushwa lakini yemekuwa hayaripotiwi
katika taasisi yao jambo linalowaathiri wananchi wenyewe na uchumi wa Taifa.
Aliwataka wananchi hao kutoa taarifa kwao
wakati wowote wanapokosa huduma baada ya kudaiwa rushwa au pale wanapobaini
miradi ya maendeleo katika maeneo yanayowazunguka inafanywa chini ya kiwango.
Kwa kupitia elimu kwa umma, Mmari alisema
wananchi 4,957 wamepatiwa elimu ya rushwa katika kipindi hicho, wakiwemo
wanafunzi 3,693.
Alisema ofisi yao pia imefanya vikao
vinne vya kujadili dhibiti zilizofanyika ili kuziba mianya ya rushwa katika
usimamizi wa mali za vijiji, zabuni ya ununuzi wa pampu ya kusukuma maji katika
mji wa Mafinga, ajira za vibarua katika mamlaka ya maji Mafinga na taratibu za
kuchukua walimu wa kujitolea shule za msingi za mjini Iringa.