Imeandikwa na Waandishi Wetu
SERIKALI imewasilisha mbele ya wabunge wote Mapendekezo ya Kiwango na
Ukomo wa Bajeti kwa mwaka 2016/2017, inayotarajiwa kuwa ya Sh trilioni
29.539. Kiasi hicho cha bajeti ya mwaka ujao wa fedha, kinatofautiana na
bajeti ya mwaka huu wa fedha unaomalizika kwa takribani Sh trilioni
tano.
Katika bajeti ya mwaka huu unaoishia, jumla ya Sh trilioni 22.495
zilitengwa kwa ajili ya bajeti nzima kutoka vyanzo vya ndani na nje.
Mapendekezo ya mwaka ujao, ambayo yametajwa na baadhi ya wadau wa
masuala ya siasa kuwa ni hatua kubwa na nzuri ya serikali, yanaonesha
Serikali inalenga kutumia Sh trilioni 15.105, sawa na asilimia 82 ya
mapato ya ndani. Mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ni Sh trilioni 2.693
na mapato kutoka halmashauri ni Sh bilioni 665.4.
Fedha za washirika wa maendeleo zinazotarajiwa ni Sh trilioni 3.600,
ambayo ni sawa na asilimia 12 ya bajeti yote. Akiwasilisha mapendekezo
ya ukomo wa bajeti hiyo katika mkutano wa wabunge wote jijini Dar es
Salaam jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango, alitaja
vipaumbele vya bajeti hiyo kuwa ni utekelezaji wa awamu ya pili ya
Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2016/2017 wa miaka mitano.
Viwanda, ulipaji madeni Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni viwanda
vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda,
kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu na mazingira
wezeshi kwa uendeshaji biashara.
Alisema bajeti hiyo, pia itaweka mkazo zaidi katika ukamilishaji wa
miradi inayoendelea, miradi mipya, ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa na
utekelezaji wa maeneo yote ya vipaumbele, yaliyoainishwa katika Mpango
huo wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.
Akizungumzia mfumo wa bajeti hiyo, Waziri huyo alisema pamoja na
michango ya ndani, pia washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh
trilioni 3.600 sawa na asilimia 12 ya bajeti yote ambayo ni misaada na
mikopo, inayojumuisha miradi ya maendeleo, mifuko ya pamoja ya kisekta
na ya kibajeti.
“Pia Serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 5.374 kutoka soko la
ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva
pamoja na mikopo mipya kwa ajili kugharimia miradi ya maendeleo ya
pamoja na kulipia malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa.
Mkopo nje “Vilevile ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu,
Serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 2.101 kutoka soko la nje kwa
masharti ya kibiashara,” alisisitiza Dk Mpango.
Akichanganua mapendekezo hayo ya bajeti, alisema kwa upande wa
matumizi katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inapanga kutumia Sh
trilioni 17.719 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh trilioni 11.820
kwa matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 40 ya bajeti yote. Aidha
kiasi cha Sh trilioni 8.702 ni kwa ajili ya fedha za ndani na Sh
trilioni 3.117 ni fedha za nje.
Bajeti inayomalizika Katika bajeti ya mwaka huu unaoishia, jumla ya
Sh trilioni 22.495 zilitengwa kwa ajili bajeti nzima kutoka vyanzo vya
nje na ndani. Jumla ya Sh trilioni 8.987 zilikuwa ni makusanyo ya ndani,
halmashauri zikijumuishwa, sawa na asilimia 97 ya makadirio ya
kukusanya Sh trilioni 9.281 katika kipindi hicho.
Dk Mpango alifafanua kuwa katika bajeti hiyo, mapato ya kodi yalikuwa
ni Sh trilioni 7.931 sawa na asilimia 99 ya lengo la kukusanya Sh
trilioni 8.016 kwa kipindi hicho.
Alisema mapato yasiyo ya kodi, yalikuwa Sh bilioni 786.1 sawa na
asilimia 86 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 916.1. Mapato
yaliyokusanywa na halmashauri, yalikuwa Sh bilioni 270 sawa na asilimia
78 ya makadirio ya Sh bilioni 347.9 kwa kipindi hicho.
Alisema kwa mujibu wa matarajio ya bajeti hiyo, washirika wa
maendeleo waliahidi kutoa Sh trilioni 2.322 kama misaada na mikopo
nafuu, lakini hadi kufikia Februari mwaka huu, walitoa jumla ya Sh
trilioni 1.017 ambazo ni sawa na asilimia 62.5 ya malengo.
Alisema Serikali ilitarajia kukopa mikopo yenye masharti nafuu ya
kibiashara kutoka vyanzo vya nje na ndani jumla ya Sh trilioni 6.175.
Alisema kutofikiwa kwa malengo ya mikopo ya kibajeti, kulitokana na
baadhi ya washirika wa maendeleo kupunguza ahadi zao, kuweka masharti
mapya na wengine kuamua kutotoa fedha walizoahidi kwa sababu ya
kubadilika kwa sera za ndani za nchi zao zinazohusu misaada kwa nchi
zinazoendelea.
Aidha alisema hadi kufikia Februari mwaka huu, Serikali ilishakopa
cha Sh trilioni 3.688 ikiwa ni asilimia 101 ya kiasi kilichopangwa
kukopwa katika kipindi hicho.
Kati ya kiasi hicho Sh trilioni 2.133 zilikopwa kwa ajili ya kulipia
amana za Serikali zilizoiva na mikopo mipya ilikuwa ni Sh trilioni 1.554
sawa na asilimia 101 ya kiasi kilichopangwa kukopwa.
Akizungumzia mgawanyo wa fedha za bajeti hiyo inayoishia, Dk Mpango
alisema Serikali ilitoa mgawo wa Sh trilioni 13.152 kwenda kwenye
mafungu mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti hiyo sawa na
asilimia 92 ya makadirio ya bajeti hiyo.
Alisema jumla ya Sh trilioni 10.595 zilitolewa katika eneo la
matumizi ya kawaida, linalojumuisha mishahara na malipo ya deni la taifa
wakati jumla ya Sh trilioni 2.557 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo.
Dk Mpango alisema hadi kufikia Februari mwaka huu, deni la taifa
linalojumuisha Serikali na sekta binafsi, lilifikia dola za Marekani
milioni 19.9 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 19.6 kwa kipindi
kinachoishia Juni mwaka jana.
Alisema kati ya kiasi hicho, dola za Marekani milioni 17.5 zilikuwa
ni deni la Serikali na dola za Marekani milioni 2.3 ni deni la sekta
binafsi hivyo deni la Serikali liliongezeka kwa asilimia nne.
Aliyataja mafanikio ya bajeti hiyo kuwa ni kuendelea kukua kwa uchumi
kwa asilimia saba, kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya ndani hadi
kufikia asilimia 99 ya lengo, kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei na
kufikia asilimia 5.6 na kutia kwa wakati fedha za miradi ya maendeleo
yenye vyanzo mahsusi kama vile mfuko wa barabara, wakala wa nishati,
mfuko wa maji na reli.
Mafanikio mengine ni kuendelea kujenga miundombinu katika sekta za
nishati, barabara, mawasiliano na uchukuzi, kufanikisha uchaguzi mkuu
mwaka jana kwa kutumia fedha za ndani, kupunguza malimbikizo ya madai ya
watumishi, wazabuni na wakandarasi na kuongeza idadi ya wanafunzi
wanaonufaika na mikopo waliohakikiwa.
Waziri Mpango alisema katika mwaka ujao wa fedha Serikali imelenga
kuhakikisha kuwa pato halisi la taifa linakua kwa asilimia 7.2 kutoka
asilimia saba, kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei, ukusanyaji wa mapato
ya ndani na halmashauri kuongezeka na kufikia asilimia 14.8 na mapato ya
kodi kufikia asilimia 12.6.
Aidha alisema pia Serikali inatarajia kuongeza matumizi kutoka
asilimia 23.9 ya pato la taifa hadi kufikia asilimia 27 na kuwa na akiba
ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa
bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
“Katika Serikali ya awamu ya tano tunatarajia mapato ya Serikali
yataongezeka na kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo nafuu kutoka
kwa washirika wa maendeleo ambayo imekuwa haitabiriki kwa siku za
karibuni,” alisisitiza.
Alisema katika mwaka ujao wa fedha Serikali itasimamia nidhamu ya
matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria ya bajeti na maelekezo
ya viongozi wa juu wa Serikali, lengo likiwa ni kupunguza matumizi
yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma.
Alisema ili kufanikisha azma hiyo, Serikali imepanga kuwianisha
matumizi na mapato halisi yatakayopatikana kwa kila mwezi, kuimarisha
ufuatiliaji wa matumizi ya Serikali ili yatumike kama ilivyokusudiwa,
kusimamia maagizo yaliyotolewa na Serikali kama ununuzi wa samani na
magari, kuziunganisha halmashauri zote katika mfumo wa malipo ya
kibenki.