ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatano, 13 Aprili 2016

Rais Magufuli aongoza mamia kumuaga mbunge mstaafu

Imeandikwa na Mwandishi Wetu RAIS John Magufuli ameungana na mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Mbunge mstaafu wa Mkoa wa Singida, Marehemu Christina Lissu Mughwai katika ukumbi wa Karimjee, Jijini Dar es Salaam.
Mughwai aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, aliagwa jana kabla ya kusafirishwa kwenda kijiji cha Mahambe mkoani Singida kwa maziko.
Pamoja na Rais Magufuli na mkewe Mama Janeth, viongozi wengine waliohudhuria shughuli ya kuaga ni Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bunge, Freeman Mbowe.
Akitoa salamu kwa niaba ya Rais Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene aliwapa pole familia ya marehemu. Alisema katika kipindi chake cha ubunge, Mughwai alitoa mchango mkubwa kama mbunge na kama mtaalamu wa Uchumi.

Kutenguliwa Anne Kilango kwaendelea kuwa gumzo

KUTENGULIWA kwa uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela kumeendelea kuwa gumzo huku viongozi wengine wakiambiwa wawe macho kwa kuchukulia uamuzi huo wa Rais Magufuli, kama funzo la kutambua aina ya uongozi anaoutaka katika Serikali yake ya Awamu ya Tano.
Wakati viongozi hususani wa kuteuliwa wakitakiwa kuzingatia ukweli kwamba serikali ya awamu hii haihitaji wanaoficha mabaya wakitaka mazuri ndiyo yaonekane, baadhi wameshauri mfumo uliopo, hususani wa kupeana taarifa uangaliwe kwa kuwa una tatizo linalohitaji kufanyiwa kazi.
Miongoni mwa watu ambao gazeti hili lilizungumza nao jana kuhusu hatua hiyo ya Rais kutengua uteuzi wa Kilango, ni mwanasiasa mkongwe nchini, Paul Kimiti aliyetaka viongozi wengine kutambua kwamba, Magufuli ni kiongozi asiyependa unafiki.
“Uongozi wake tangu mwanzo umejidhihirisha wazi kuwa ni kiongozi anayependa uwazi na ukweli hataki short cut (njia za mkato),” alisema Kimiti. Kimiti aliyewahi kushika uwaziri katika Serikali zilizopita, alisema hatua hiyo ya Rais ni ishara na funzo kwa viongozi wengine hasa wale walio madarakani kuhakikisha kuwa wanawajibika ipasavyo kwa kufuata misingi ya uwazi na kutokimbilia njia za mkato.
Alisema kwa hali ilivyo, ni vyema viongozi waliopo wakaanza kufuata heshima na taratibu za kiongozi aliyewaweka madarakani, hali ambayo itawasaidia kutowajibishwa.
Mwanasiasa huyo ambaye alionesha kuguswa kwa mtazamo chanya na hatua anazochukua Rais, alisema kumekuwa na utaratibu wa watendaji kutoa taarifa zisizo sahihi na zisizo kamili kwa wakuu wao wa kazi kwa lengo la kuonesha kuwa mambo ni mazuri.
Alisema jambo hilo ni tatizo kubwa linalopaswa kukemewa. Utendaji wa kujikomba “Hii ni kero kubwa, watendaji wengi wanaficha taarifa za ukweli kwa wakuu wao ili kuonesha mambo ni mazuri, hili ni jambo baya kabisa kwani matokeo yake ndiyo haya; anakuja kuwajibishwa mtu mwingine ambaye huenda hakuhusika na taarifa hizo,” alisisitiza.
Alisema utendaji wa aina hiyo ni sawa na utendaji wa kujikomba ambao hauna tija, kwani pamoja na kuficha ukweli na uhalisia wa mambo, mwisho wake siku wananchi ndio waathirika na baadaye ukweli hufichuka.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja alisema kilichotokea ni funzo kubwa kwa viongozi wengine kuhakikisha kuwa kila taarifa wanayopatiwa lazima wanaifanyia kazi na kujiridhisha kabla ya kuitoa kwa umma.
“Mama Kilango kwa vyovyote vile bado ndio alikuwa anaanza kazi ya ukuu wa mkoa, hivyo lazima atakuwa amepatiwa taarifa aliyoitoa kwa umma na watendaji wake. Hii ilikuwa ni kawaida, viongozi wengi huuamini mfumo unaowapatia taarifa,” alisema Semboja.
Hata hivyo, alisema kiongozi huyo alipaswa baada ya kupatiwa taarifa ya awali, angewasiliana na vyanzo mbalimbali kupata uhakika kwa kutumia madaraka aliyonayo wakiwemo waajiri na wanaofanya malipo kujiridhisha.
Alisema anaamini hatua aliyoichukua Dk Magufuli ni ishara na njia yake ya kutambulisha kwa umma mtindo wa uongozi unaozingatia uwazi na uwajibikaji. “Hiki kwetu ni kitu kipya hatujakizoea, lakini sasa ni vyema kila kiongozi awe makini na kutambua kuwa akikosea lazima awajibike,” alisisitiza.
Mfumo uangaliwe
Pamoja na hayo, alimuomba Rais Magufuli awe mvumilivu na atambue kuwa huenda tatizo kubwa bado lipo kwenye mfumo uliopo wa kupeana taarifa ambao utahitaji kuangaliwa kwa umakini na kuchukuliwa hatua stahiki.
Alisema Dk Magufuli ni kiongozi anayefuata mfumo wa kisheria na kwamba hatua zote alizochukua zinatokana na nia njema aliyonayo kwa watanzania. “Huyu ni mtakatifu baada ya Mungu, ana moyo mzuri na nia njema kwa watanzania,” alisema Profesa Semboja.
Akizungumzia watumishi hewa, Profesa Semboja alishauri baada ya operesheni ya kuwatafuta upande wa rasilimali watu ndani ya utumishi wa umma lazima utoe taarifa nzima na kufafanua kilichotokea.
Kwa upande wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, alisema hatua aliyoichukua Dk Magufuli ya kumvua uongozi Kilango ni ishara kuwa anatoa kipaumbele katika suala zima la uwajibikaji lakini pia hapendi viongozi wasiojishughulisha.
“Inaonesha dhahiri Dk Magufuli katika masuala nyeti yanayogusa taifa hapendi majibu mepesi wala njia za mkato. Hii inamaanisha kuwa viongozi hawana budi kuzifanyia kazi taarifa wanazopewa na kujiridhisha kwanza,” alisema Dk Bana.
Awali gazeti hili lilizungumza na Kilango kwa njia ya simu ili kuweza kupata upande wake kuhusu nini kilitokea na kusababisha kutoa taarifa hiyo isiyo sahihi kuhusu watumishi hewa mkoani Shinyanga, ambapo mara baada ya salamu, mwandishi alipojitambulisha alikata simu.
Juzi Rais Magufuli alitengua uteuzi wa mkuu huyo wa mkoa baada kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari kuwa mkoani kwake hakuna watumishi hewa. Alisema baada ya taarifa hiyo, aliunda timu maalumu kwa ajili ya uhakiki wa watumishi hewa mkoani humo na ndani ya siku moja, walibaini kuwepo kwa watumishi hewa 45 waliokuwa tayari wamelipwa mishahara yenye gharama ya Sh milioni 339.9.

Mkataba wa Lugumi wawa kaa la moto

Imeandikwa na Mwandishi Wetu(Habari leo) BUNGE limetoa siku tatu kwa Jeshi la Polisi kuwasilisha kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) mkataba wa Kampuni Lugumi Enterprises wenye thamani ya Sh bilioni 37.
Hatua hii inakuja siku mbili baada ya jeshi hilo kudaiwa kukaidi agizo la kamati hiyo, iliyotaka likabidhi nyaraka za utekelezaji wa mkataba ufanyiwe tathmini kutokana na malalamiko yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) katika hesabu za mwaka 2013/2014.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Aeshi Hilaly alisema agizo la kamati la kutaka mkataba huo, lilitolewa wiki iliyopita kuwezesha wabunge kuangalia utekelezaji wake.
“Jana (juzi) ilikuwa siku ya mwisho kwa jeshi kuwasilisha mkataba huo ofisi za Bunge, lakini mpaka leo (jana) muda huu ninapozungumza nanyi (saa 7:30 mchana) walikuwa hawajawasilisha. “
Siku zote tumekuwa tukitoa maagizo kwa mdomo na taasisi nyingi zimekuwa zikitekeleza, lakini hili la mkataba wa Lugumi naona kwa wenzetu limekuwa gumu, hivyo tumeamua kuwakumbusha kwa maandishi,” alisema.
Alisema kamati hiyo imetoa siku tatu tangu barua itakapopelekwa na ofisi za Bunge, kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo ili kamati hiyo iweze kupitia utekelezaji wa mkataba huo na baadaye kupeleka mapendekezo kwenye Bunge.
“ Katika suala hili, Kamati haitarudi nyuma, hivyo tunawaomba wenzetu wa Jeshi la Polisi kutupa ushirikiano, si jambo la peke yangu kuamua, ni la Bunge, baada ya kupitia tunapeleka mapendekezo bungeni ambalo ndilo litakaloamua nini kifanyike,” alisisitiza.
Hata hivyo, habari zilizofikia HabariLeo jana zinasema jeshi hilo lilipeleka mkataba huo katika Kamati ya Mambo ya Nje na Usalama na juzi badala ya Kamati ya PAC iliyoagiza. “Kuna taarifa kuwa mkataba huo umepelekwa kwenye kamati ya Mambo ya Nje inayoongozwa na Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajabu,” kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo, Adadi aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) alikanusha madai hayo kwa kujibu kifupi kwa ujumbe wa simu kuwa, “suala hilo limepelekwa PAC.” Kamati ya PAC ilipokuwa ikipitia hesabu za Jeshi la Polisi, ilibaini kuwapo mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises .
Kupitia mkataba huo wa mwaka 2011, Kampuni ya Lugumi Enterprises ilipewa zabuni ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.
Inasadikiwa kampuni hiyo imekwishalipwa Sh bilioni 34 kati ya Sh bilioni 37 ikiwa ni sawa na asilimia 99 ya fedha zote, huku ikiwa imefunga mashine katika vituo 14 pekee katika jiji la Dar es Salaam, ambavyo pia inadaiwa havijulikani maeneo vilipo.

Magazeti ya Leo jumatano tarehe 13/04/2016

Headline za magazeti ya Leo zinaletwa kwenu Kwa hisani  ya New Mwalimu education centre inayopatikana eneo la ilula madizini _iringa Tanzania majengo ya kanisa catholic kigango cha madizini madizini













Jumanne, 12 Aprili 2016

Magazeti ya Leo jumanne ya tarehe 12/04/2016



Head line news za magazeti ya Leo zinaletwa kwenu Kwa hisani ya new Mwalimu tuition centre Inayopatikana ilula madizini kanisa la Romani catholic wanafundisha masomo ya ziada Kwa kidato cha kwanza mpaka cha sita na Kwa wanaotaka kurudia mitihani yao nyote mnakaribishwa Kwa mawasiliano zaidi piga
no 0629121512 elimu ni jitihada