ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatatu, 18 Aprili 2016

Mwenge wa Uhuru kuwashwa leo

Imeandikwa na John Nditi, Morogoro

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan leo atawasha Mwenge wa Uhuru na kuzindua rasmi mbio zake ili kukimbizwa katika halmashauri za wilaya na Manispaa zipatazo 179 za mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani.
Uzinduzi huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambao utatanguliwa na shamrashamra za halaiki kutoka kwa vijana zaidi ya 1,000 na vikundi vya utamaduni kutoka wilaya za Morogoro na nje ya mkoa huo.
Katika uzinduzi huo, viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na vyama vya siasa wamealikwa kushiriki wakiwemo pia mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Miongoni mwa mawaziri ambao hadi jana walikuwa tayari wamewasili mkoani hapa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, Sera, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mouldine Castico.
Mawaziri hao jana waliungana na Makamu wa Rais kutembelea mradi wa vijana wajasiriamali wa mafundi seremala eneo la Mtaa wa Betero, Kata ya Sabasaba, Manispaa ya Morogoro. Kaulimbiu za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni “Vijana ni Nguvu kazi ya Taifa, Washirikishwe na Kuwezeshwa.”
Baada ya kuwashwa leo, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kuhitimishwa wilayani Gairo ambako Aprili 25, mwaka huu utakabidhiwa mpakani mwa wilaya hiyo na Kilindi ya Mkoa wa Tanga ili kuendelea na mbio zake.
Kwa mujibu wa ratiba ya mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu, utakimbizwa katika Halmashauri na Manispaa zipatazo 179 na kilele cha mbio hizo ni Oktoba 14, mwaka huu katika Mkoa wa Simiyu.
Mwenge wa Uhuru uliwashwa kwa mara ya kwanza Desemba 9, 1961 kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro, kutimiza ahadi ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kudai Uhuru wa Tanganyika.

DC aagiza kusakwa aliyempa mimba mwanafunzi

Imeandikwa na Angela Sebastian, Bukoba MKUU wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Jackson Msome ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kumsaka na kumtia mbaroni kisha kumfikisha mahakamani mtu aliyempa mimba mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Karabagaine iliyoko wilayani humo.
Msome alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati alipofanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo na kupewa taarifa kuwa mwanafunzi huyo ni mjamzito.
“Vyombo vya ulinzi na usalama kaeni na mwanafunzi huyo anamtambua aliyempa mimba, mhoji na hakikisheni mnamkamata mtu huyo kisha afikishwe mahakamani kujibu tuhuma hiyo,” alisema na kuongeza: “Pia jamii fichueni wale wanaowapa mimba watoto wetu wa kike, wanaowaoa na kuwaozesha waweze kutiwa mbaroni na kupambana na mkono wa sheria.”
Alisema kutokana na tabia hizo, watu wawili wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuwapa wanafunzi mimba katika shule za sekondari za Nyakibimbili ambako wanafunzi wawili wa kidato cha kwanza, Alicia Vedasto na Dominatha Jacob wamepewa ujauzito.

Bajeti ya Magufuli kusomwa Juni 9

Imeandikwa na Mwandishi Wetu KWA mara ya kwanza Bajeti ya Serikali ya Rais John Magufuli inatarajiwa kuwasilishwa Juni 9, mwaka huu, kwenye Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11, unaoanza mjini Dodoma kesho.
Bajeti hiyo itawasilishwa rasmi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango saa 10 kamili jioni siku ya Alhamisi baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Hali ya Uchumi wa Nchi asubuhi siku hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha Bunge jana, ilieleza kuwa baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, ambayo mapendekezo yake ya awali kwa wabunge yalibainisha kuwa itakuwa ni ya Sh trilioni 29, wabunge wataijadili kwa muda wa siku tisa kuanzia Juni 13 hadi Juni 21, mwaka huu.
Pamoja na bajeti hiyo, pia Dk Mpango atawasilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2015/16 hadi 2020/21.
“Baada ya kuwasilishwa kwa mpango huo, Bunge pia litapokea na kujadili utekelezaji wa bajeti kwa wizara zote kwa mwaka wa fedha 2015/16 na makadirio ya matumizi ya Serikali 2016/17, kazi itakayofanyika kuanzia Aprili 22 hadi Juni 2, mwaka huu,” ilieleza taarifa ya Bunge.
Hivi karibuni, Dk Mpango aliwasilisha mapendekezo ya ukomo wa bajeti hiyo ya mwaka 2016/17 mbele ya wabunge jijini Dar es Salaam, na kubainisha kuwa inatarajiwa kuwa ya Sh trilioni 29.539 sawa na ongezeko la asilimia 31.32 ya bajeti iliyopita ya mwaka 2015/2016.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya bajeti hiyo, Serikali inalenga kutumia Sh trilioni 15.105 sawa na asilimia 82 ya mapato ya ndani, mapato ya kodi na yasiyo na kodi na mapato kutoka halmashauri Sh trilioni 2.693 na Sh bilioni 665.4 na washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.600 ambayo ni sawa na asilimia 12 ya bajeti yote.
Akichanganua mapendekezo hayo, alisema kwa upande wa matumizi katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inapanga kutumia Sh trilioni 17.719 kwa matumizi ya kawaida na Sh trilioni 11.820 kwa matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 40 ya bajeti yote.
Aidha, alitaja vipaumbele vingine kuwa ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu na mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara.
Pamoja na kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, pia katika Mkutano huo Tatu wa Bunge unaoanza kesho, pamoja na kuwasilishwa hati za mezani, Bunge pia litapokea Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15 ambayo hivi karibuni ilikabidhiwa kwa Rais Magufuli.
“Pia Bunge litapokea majibu ya Serikali kuhusu hoja zilizotolewa na CAG kwa hesabu za mwaka wa fedha 2014/15,” ilisema taarifa hiyo ya Kitengo cha Mawasiliano cha Bunge.
Taarifa hiyo ilisema pia katika mkutano huo, Bunge litajadili na kupitisha miswada miwili ambayo ni Muswada wa Sheria ya Matumizi wa Mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2016.
“Vilevile inategemea kuwa Serikali itawasilisha bungeni miswada ya Sheria kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa bungeni mara baada ya shughuli ya kupitisha bajeti kukamilika,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, katika mkutano huo kutakuwa na shughuli ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge kwa ajili ya kuziba nafasi iliyoachwa wazi baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kufanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge. Nafasi hiyo imeachwa wazi na Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa.
Aidha, wabunge wapya wanne ambao ni Shamsi Vuai Nahodha wa Jimbo la Kijitoupele, Ritha Kabati na Oliver Semguruka wote Viti Maalumu CCM na Lucy Owenya wa Viti Maalumu Chadema, wanatarajiwa kuapishwa rasmi.

Makonda atangaza neema kwa walimu

Imeandikwa na Sophia Mwambe MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameahidi kutoa zawadi ya fedha kwa mwalimu atakayefaulisha mwanafunzi katika somo lake la sayansi, lengo likiwa ni kutoa motisha kwa walimu.
Makonda aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akizindua programu ya kuwasaidia wanafunzi waliotoka katika familia masikini iliyoandaliwa na shule za Feza.
Feza wametoa Sh milioni 37.5 kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi 150 wanaotoka katika familia masikini.
Makonda alisema atatoa Sh milioni 15 kwa mwalimu wa sekondari atakayefaulisha mwanafunzi katika masomo ya Sayansi na Sh milioni 10 kwa mwalimu wa kidato cha pili atakayefaulisha mwanafunzi katika masomo ya sayansi na Sh milioni tano kwa mwalimu wa shule ya msingi atakayefaulisha mwanafunzi.
“Niseme sitaishia kwenye kutoa fedha pekee, mwalimu huyo na familia yake watachagua mbuga yoyote ya wanyama watakayoitaka na nitagharamia kila kitu, naamini kwa kufanya hivyo kutajenga motisha hata kwa walimu wengine kuongeza jitihada na kuhakikisha anafaulisha wanafunzi,” alisema Makonda.
Aidha, Makonda amewashukuru Feza kwa kuamua kuwasaidia wanafunzi hao na amewataka wazazi kuhakikisha wanasimamia vyema fedha hizo ili zifanye kazi iliyokusuduwa.
“Sitopenda kusikia mama ametumia fedha hizo tofauti na nyinyi wanafunzi muwalipe wafadhili hawa kwa kusoma kwa bidii, hakuna mtu atakubali kuendelea kutoa msaada kwa mtu ambaye haoneshi juhudi,” aliongeza Makonda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule hizo, Isa Otcu alisema shule hizo zimeamua kutoa msaada huo kwa ajili ya kumuunga mkono Rais John Magufuli katika harakati zake za elimu bure.
Alisema programu hiyo itatoa kiasi cha Sh 250,000 kwa kila mwanafunzi na tayari wameshaweka kiasi cha Sh 100,000 katika akaunti za wanafunzi hao kuanzia Januari mpaka Aprili.
Aliongeza kuwa wameamua kuwateua kina mama kwa ajili ya kusimamia fedha hizo ambazo zitawekwa katika akaunti zao za benki, kwani wanaamini mama ana uwezo wa kuhifadhi kwa faida ya watoto wake.