ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 6 Mei 2016

Farid Mussa afuzu majaribio Hispania

Imeandikwa na Mwandishi Wetu SASA ni dhahiri kwamba, winga mahiri nchini Farid Mussa anayeichezea Azam FC ya Dar es Salaam, ameingia katika anga za soka la kimataifa.
Hatua hiyo imekuja baada ya nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania kufaulu katika majaribio yake aliyokuwa anafanya katika klabu ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Hispania, Deportivo Tenerife.
Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi wa Azam FC, Yussuf Bakhresa akisema klabu hiyo sasa inatarajiwa kuingia katika mazungumzo na Azam juu ya kumnunua moja kwa moja mchezaji huyo, badala ya kumtwaa kwa mkopo kama walivyokuwa Wahispania hao.
Mtandao wa binzubeiry.co.tz, umemnukuu Bakhresa akisema; “Tunatarajia kuanza mazungumzo nao juu ya suala la Farid, ingawa wazo lao la awali ni kumchukua kwa mkopo wa miaka miwili. Sasa tunasubiri ofa yao rasmi, kisha Bodi ya Ukurugenzi itajadili na kutoa maamuzi.”
Naye Farid ameelezea kufurahia matokeo ya majaribio yake, akisema haikuwa kazi nyepesi kwake kuweza kuwaridhisha maofisa wa benchi la ufundi la Tenerife.
“Kwa kweli nimefurahi sana na ninamshukuru Mungu kwa kufuzu majaribio, ila haikuwa kazi nyepesi, mpira wa Ulaya mgumu,” alisema.
Awali, Farid ilikuwa apelekwe moja ya klabu za Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kama La Liga, kati ya Las Palmas na Athletic ya Bilbao kwa majaribio, lakini wakala wake akashauri mchezaji huyo aanzie timu ya Daraja la Kwanza Hispania ili kupata nafasi ya kucheza na kuinuka haraka.

Azam FC majanga, Yanga bingwa Jumapili?

Imeandikwa na Vicky Kimaro
KIMAHESABU Yanga tayari ni bingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara msimu wa 2015/2016, labda itokee miujiza ya kupoteza mechi zake zote tatu zilizosalia katika ligi hiyo, huku mahasimu wao Simba wakishinda mechi zote nne walizobakiwa nazo.
Lakini sare au kipigo kimoja tu kwa Simba kitaihakikishia Yanga taji la 26 katika ligi hiyo iliyoingia katika msimu wa 51 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965.
Hii ina maana kwamba, mbio za ubingwa kwa sasa zimebaki kwa Yanga na Simba tu, baada ya jana Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kuipoka Azam FC pointi tatu na mabao matatu, hivyo kuirudisha kutoka nafasi ya pili hadi ya tatu ikiwa na pointi 57.
Na hata kama ikishinda mechi tatu zilizosalia, itakuwa na jeuri ya kufikisha pointi 66 ambazo zimeshavukwa na Yanga yenye pointi 68.
Simba ina pointi 58 na ikishinda zote nne itakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 70, lakini wakati huohuo ikiomba Yanga ipoteze mechi zake zote tatu ili ubingwa huo utue Mtaa wa Msimbazi kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2011/2012.
Keshokutwa, Simba itacheza na Mwadui FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hivyo sare au kipigo kitapeleka chereko kwa Yanga, kwani huenda wakatangazwa mabingwa bila hata kugusa mpira katika siku husika.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alithibitisha jana kuwa, Azam imepokonywa pointi tatu na mabao matatu na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kosa la kumchezesha beki wake mahiri Erasto Nyoni akiwa na kadi tatu za njano katika mchezo dhidi ya Mbeya City mjini Mbeya.
“Azam wanatakiwa kutunza kumbukumbu za wachezaji wao, bodi imefikia uamuzi wa kuipokonya pointi tatu Azam FC baada ya kubaini ilimtumia Erasto Nyoni kinyume cha sheria,” alisema Lucas.
Katika mchezo huo, Azam ilishinda 3-0.
Kwa mujibu wa kanuni ya 37 (4) toleo la 2015 ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara juu ya udhibiti wa wachezaji; “mchezaji atakayeonywa kwa kadi tatu za njano katika michezo mitatu, basi atalazimika kukosa mchezo unaofuata wa timu yake.”
Aidha kanuni ya 14 (37) ya kanuni hiyo imempa ushindi wa mabao matatu na magoli matatu timu ya Mbeya City.
Kutokana na adhabu hiyo kwa Azam, ni wazi Yanga sasa imebakiza mechi moja kutwaa ubingwa msimu huu na huenda ikatangaza ufalme Jumanne ijayo mjini Mbeya itakayokwenda kupambana na Mbeya City. Ikishinda, itafikisha pointi 71 ambazo hazitafikiwa na Simba.
Msemaji wa Azam, Jaffari Maganga akizungumzia adhabu hiyo, alisema; “Tumesikia taarifa tu bado hatujapata barua rasmi ya kutujulisha kupokonywa pointi, tutakapoipata tutalizungumzia suala hili.”
Adhabu ya aina hii imewahi kuikumba Simba 2006 na 2007 na pia Yanga mwaka 2012 huku ligi ikielekea ukingoni. Ilivyokuwa; Mwaka 2006 Simba ilinyang’anywa pointi katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar, baada ya kudaiwa kumchezesha Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Mwaka 2007 Simba ikakutana tena na adha kama hiyo ikiwa imebakiza michezo minne mkononi kwa kupokwa pointi tatu na mabao matatu na ushindi kupewa Azam FC baada ya kumchezesha Haruna Moshi ‘Boban’ aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Mwaka 2012 Coastal Union ilinufaika kwa kupewa ushindi wa chee wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha mchezaji Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Machi 31 mwaka huo Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Bunge lachafuka, mbunge Waitara atolewa nje

MBUNGE wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) ametolewa nje ya Bunge baada ya kutaka kumkwida Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agustine Holle (CCM) aliyedai kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika wote wa Chadema kuwa wanaugua kichaa.
Waitara alionesha kukerwa na kauli hiyo hasa pale Holle alipokataa kufuta kauli yake, licha ya kutakiwa kufanya hivyo na Naibu Spika, Dk Tulia Akson.
Wakati Holle akichangia, Waitara alinyanyuka kwenye kiti chake na alipofika alipo mbunge huyo alimzungumzisha maneno ambayo hayakusikika na kuonesha kama kutaka kumpiga kabla ya kukaa kwenye kiti kilicho mbele yake ndipo, Holle alisikika akisema “wewe unataka nini” ndipo Naibu Spika alipogundua kuwa Waitara anataka kumpiga Holle na kumuamuru atoke nje lakini hakutii amri hiyo.
Kutokana na kutotii, Naibu Spika aliamuru askari wamtoe ndipo walipoingia zaidi ya askari watano na kutoka naye hadi nje ya geti kubwa la kuingilia bungeni.
Holle wakati anachangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017, alimtaja Lissu ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara hiyo kuwa ana taarifa kuwa Lissu amewahi kuugua ugonjwa wa kichaa na hadi sasa ana faili kwenye Hospitali ya Vichaa ya Mirembe iliyopo mkoani Dodoma.
Hata hivyo, alipopewa nafasi na Naibu Spika kufuta kauli yake akasema “nafuta kauli yangu lakini kwa taarifa zilizozagaa nimeamini ni kweli na mbona kwao(Chadema) wapo wengi hata Mnyika sasa hivi yupo Muhimbili anatibiwa kichaa”.
Kutokana na kauli hiyo, Lissu alisema licha ya kuifahamu Hospitali ya Mirembe, hajawahi hata kuingia kwenye geti la hospitali hiyo wala kuugua ugonjwa huo na kutaka kiti cha Naibu Spika kimtake Holle athibitishe ; na akishindwa kanuni zielekeze hatua za kuchukua kama zilivyowekwa.

Walimu wagoma, kisa mwenzao kuzabwa kofi darasani 
Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga
WALIMU wa shule ya msingi Kianda wameanza mgomo wa siku mbili wa kutofundisha shuleni hapo huku wakilaani kitendo cha Ofisa Elimu (Shule za Msingi) wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Peter Fusi kumshambulia na kumpiga makofi mwalimu mwenzao akiwa darasani mbele ya wanafunzi wake.
Makamu Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Flora Kipesha alisema wameitisha mgomo huo wa siku mbili kupinga kitendo cha Fusi kumshambulia na kumpiga makofi mwalimu mwenzao Jacob Msengezi (25) ambaye anafundisha somo la Hisabati Darasa la Saba shuleni hapo.
“Licha ya kulaani vikali kitendo hiki cha udhalilishaji alichofanyiwa mwalimu mwenzetu na Ofisa Elimu (DEO) wetu (Peter Fusi) kumcharaza makofi mbele ya wanafunzi wake akiwa darasani ….
Ametudhalilisha sote yaani hata hamasa ya kufundisha imetoweka ….. “Sasa hatutaingia darasani kufundisha kwa siku mbili tukimshinikiza Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (Adam Missana) achukue hatua dhidi ya ofisa huyo wa elimu ……yaani tunadhalilishwa hivi mbele ya wanafunzi wetu wenyewe wakati kazi hii tumeisomea na tuna vyeti halali ….
Tukiwa na sifa stahiki za taaluma ya ualimu,” alieleza Kipesha. Akifafanua, alisema walimu hawataingia kufundisha kwa siku hizo mbili na watakuwa ofisini wakiandaa mitihani huku wanafunzi wakiendelea kuhudhuria shuleni hapo kama kawaida.
Naye Mwalimu Msengezi alilieleza gazeti hili kwa njia ya simu akiwa shuleni Kianda kuwa juzi Jumatano Ofisa Elimu, Fusi alitembelea shuleni hapo saa tatu asubuhi akikagua mazingira ya shule.
“Mie wakati huo nilikuwa darasani na wanafunzi wa darasa la saba nikisahihisha madaftari yao kwani tayari kipindi changu kilianza saa 2:00 na kumalizika 2:40 asubuhi … Hivyo kwa kuwa mwalimu wa somo la Kiingereza alikuwa ‘busy’ akitunga mitihani niliamua niutumie muda huo kubaki darasani humo nikisahihisha madaftari,” alieleza Msengezi Kwa upande wake, Katibu wa CWT Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Vicent Ndewele akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alikiri kutokea kwa tukio hilo huku akisisitiza kuwa chama hicho kitatoa msimamo wake leo.

‘JK hajakataa kukabidhi uenyekiti’

Imeandikwa na Mwandishi Wetu
Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakuna mgogoro wowote katika mchakato wa kukabidhi kijiti cha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho kutoka kwa Mwenyekiti wa sasa Jakaya Kikwete kwenda kwa Rais John Magufuli.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Msemaji wa CCM Taifa, Christopher ole Sendeka ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) ilieleza taarifa hizo zinazushwa na baadhi ya vyombo vya habari visivyozingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
“Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vinatoa taarifa potofu kuhusu mchakato wa Mwenyekiti wa sasa wa CCM Dk Jakaya Kikwete kukabidhi kijiti cha uongozi wa CCM kwa Rais John Pombe Magufuli kama ilivyo mila na desturi ya CCM. “Yamekuwapo madai eti Mwenyekiti amekataa au anachelewesha kukabidhi kijiti.
Habari hiyo si kweli kabisa na ni kinyume chake, kwani Dk Kikwete amekuwa akisisitiza kukabidhi madaraka mapema iwezekanavyo. “Kwa ajili hiyo kwenye kikao cha Mei 3, 2016 alikataa kusiongezwe ajenda nyingine ambazo zitalazimisha Mkutano Mkuu Maalumu kuchelewa kufanyika kwa sababu ya kukamilisha maandalizi ya ajenda hizo na alisisitiza ajenda iwe moja tu,” ilieleza taarifa hiyo ya CCM.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ole Sendeka, dhamira ya kufanyika Mkutano Mkuu Maalum Juni, 2016 iko pale pale na kwamba kilichoelezwa kwenye kikao ni kutaka kukamilisha utaratibu wa kupata fedha za kugharimia mkutano huo.
“Taratibu zikikamilika tarehe itapangwa. Mipango ya kutafuta pesa inaendelea na ikikamilika tarehe itatangazwa,” alisema Msemaji huyo wa CCM Taifa. Aliwataka wana-CCM wasihamanike wala kubabaishwa na taarifa za upotoshaji zinazofanywa na watu wenye nia mbaya na chama hicho, akisema watu hao ni wale ambao wamekuwa wakiiombea mabaya CCM bila ya mafanikio.
“Pia tunapenda kukanusha madai ati kuwa Mwenyekiti Kikwete aliwatahadharisha wajumbe wa Kamati Kuu kuhusu ukimya wa Edward Lowassa. Hakuna wakati wowote kauli kama hiyo aliitoa. Ni uzushi mtupu. Jina la Ndugu Lowassa halikutajwa kabisa,” alisema.
Katika hatua nyingine Ole Sendeka alikanusha madai ya kufanyika mkutano baina ya Mwenyekiti Kikwete, Rais Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, kuhusu uchaguzi wa Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM.

Atuhumiwa kumuua mkewe na mtoto kwa wivu wa mapenzi

POLISI mkoani Pwani inamshikilia Frowin Mbwale (26) mkazi wa Kawe jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuwaua kwa kuwachinja; mkewe Oliver Erasto (23) na mtoto wake, Emmanuel (3) kutokana na kilichodaiwa ni wivu wa mapenzi.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi, alisema mauaji hayo yalifanyika juzi saa 10.30 jioni eneo la Zinga katika kata ya Dunda , tarafa ya Mwambao wilayani Bagamoyo.
Mushongi alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida juzi siku ya tukio mtuhumiwa akiwa na mwenzake aliyejulikana kwa jina la Rajabu Juma (20) mkazi wa Makongo jijini Dar es Salaam waliwaua watu hao kwenye vichaka vilivyopo kwenye eneo hilo la Kaole.
Juma pia anashikiliwa na Polisi. “Muda huo mtuhumiwa akiwa na mwenzake alimhadaa mke wake kuwa waende kwenye nyumba yao ambayo inaendelea kujengwa kwa lengo la kuitazama ambapo mke wake alikubali na kumbeba na mtoto wao na kwenda huko ambako aliwachinja shingoni,” alisema Kamanda Mushongi.
Alisema mtuhumiwa kumbe lengo lake halikuwa kuangalia ujenzi wa nyumba yao huko Kaole bali alikuwa na lengo lingine la kufanya unyama huo ambao aliutekeleza akiwa na rafiki yake huyo ambaye walishirikiana kumchinja mke na mtoto wake.
“Chanzo cha mauaji hayo ni mtuhumiwa huyo alikuwa akimtuhumu mke wake kuwa ana uhusiano na mwanamume mwingine aitwaye Hamza mkazi wa Kawe jijini Dar es Salaam na kusababisha mauaji hayo ya kusikitisha ambayo yamewaumiza watu wengi,” alisema Mushongi.
Alibainisha kuwa miili ya marehemu hao ilikutwa ikiwa imechinjwa na watu hao umbali wa mita 100 kutoka barabara ya magari itokayo Kaole kwenda eneo la Mbegani. Alisema watuhumiwa hao walikamatwa saa 3.30 usiku baada ya wananchi Zinga kuwatilia shaka walipokuwa wakijaribu kutaka kutoroka na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika. Miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kusubiri ndugu kwa ajili ya maziko.

Magazeti ya Leo ijumaa ya tarehe 06/05/2016

Magazeti haya ya Leo yanaletwa kwako Kwa hisani kubwa ya Airtel jisevie kifurushi lwa kubonyeza *149*99#. Airtel tumekufikia na techno simu iliyoimara na Kwa bei nafuu