ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 14 Mei 2016

MAGAZETINI:#Yanga ni chereko tu leo

Imeandikwa na Vicky Kimaro.
YANGA inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo kupambana na Ndanda FC katika mechi ya duru la pili Ligi Kuu Tanzania Bara inayofikia tamati Mei 22 mwaka huu. Yanga inayonolewa na Mholanzi Hans Pluijm, itashuka dimbani ikiwa tayari imetetea ubingwa wake, ikiwa inaushikilia kwa mwaka wa pili mfululizo, ambapo leo mchezo huo utatumika kuikabidhi kombe lao.
Msimu uliopita wa ligi hiyo, Yanga ilitwaa ubingwa wakiwa na mechi mbili mkononi, lakini safari hii wamechukua wakiwa na mechi tatu. Hiyo inatokana na Simba kufungwa bao 1-0 na Mwadui FC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kitendo ambacho kiliisafishia njia Yanga kabla, kwani kulikuwa hakuna timu ambayo ingepata pointi 69 za Yanga.
Simba ingekuwa ikishinda mechi zake zilizobaki ingefikisha pointi 67. Lakini Yanga iliupamba maua ubingwa huo Jumanne baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-0 na kufikisha pointi 71, ambazo hakuna timu ya kuzifikia.
Yanga itaingia uwanjani leo, ikicheza kwa tahadhari kubwa kuhofia kupata majeruhi, kwani Jumatano ijayo, inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Esperanca ya Angola katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC).
Mara ya mwisho Yanga ilipocheza na Ndanda FC, Yanga ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0, lililofungwa na beki Kelvini Yondani. Kwa mazingira, ni wazi Ndanda hawatokubali kupoteza mchezo wa pili mbele ya timu hiyo, ambayo leo itakabidhiwa kombe lake la ubingwa.
Pluijm aliliambia gazeti hili kuwa licha ya kutumia mchezo wa leo kama maandalizi yake ya mwisho kabla ya kuivaa Esperanca, anaupa umuhimu mkubwa na wachezaji wake hawatabweteka katika mechi zote zilizosalia.
“Sijawahi kuidharau timu yoyote inayocheza Ligi Kuu, iwe ipo juu katika msimamo au inapigana kukwepa kushuka daraja, nimebakiwa na mechi mbili, mfumo wangu ni ule ule wa kushambulia na kufunga magoli mengi, kila timu nitahakikisha naifunga kwa idadi kubwa ya mabao,” alisema Pluijm.
Kwa upande wa kocha wa Ndanda, Abdul Mingange alisema kikosi chake ambacho ni wenyeji wa mchezo huo watahakikisha wanapata ushindi na kujiweka vizuri zaidi. Ndanda inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33.
Rekodi ya ubingwa Yanga
Yanga imefanikiwa kutwaa ubingwa wa 26 mwaka huu, ubingwa ambao tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu Tanzania Bara hakuna timu yoyote iliyofikia idadi hiyo.
Simba ya Dar es Salaam yenye upinzani na Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa imetwaa mara 18. Tambwe avunja rekodi Mrundi Amissi Tambwe amefunga mabao 21 hadi sasa katika ligi hiyo na kuvunja rekodi ya Abdallah Juma aliyefunga mabao hayo 20 ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Rekodi ya kufunga mabao mengi inashikiliwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyefunga mabao 24 katika ligi hiyo mwaka 1994. Tambwe pia ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni nchini kufunga zaidi ya mabao 20 katika ligi Tanzania.
Pia ameweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji mwenye mabao mengi zaidi Ligi Kuu Tanzania Bara ndani ya kipindi cha misimu mitatu tu baada ya kufunga mabao 54.

MAGAZETINI:#Serikali yasitisha ajira za majeshi

Imeandikwa na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imesitisha kwa muda ajira zote kwenye vyombo vya ulinzi na usalama vilivyomo ndani ya wizara hiyo, ikiwemo Jeshi la Polisi ili kupitia upya utaratibu wa kutoa ajira na kuondoa uwezekano wa watu wasio na sifa kujipenyeza.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema hayo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema), aliyetaka kufahamu ni kwa nini Serikali inasitisha ajira katika Jeshi la Polisi, wakati bado nchi inakabiliwa na uhaba wa askari ndani ya jeshi hilo wakiwemo askari wa kike.
“Tumesitisha kutoa ajira ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuondoa uwezekano wa watu wasio na sifa kujipenyeza na kupata ajira ndani ya vyombo vilivyo chini ya wizara hiyo,” alisisitiza.
Miongoni mwa vyombo hivyo vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mbali na Jeshi la Polisi ni Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uhamiaji. Mbali na Komu, Mbunge mwingine ambaye ni wa Viti Maalumu, Hawa Mwaifunga (Chadema), alitaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha askari wasio na sifa wanachukuliwa hatua, ambapo pia alitaka kufahamu utaratibu wa uhakiki vyeti vya askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi umefikia wapi.
Akizungumzia Jeshi la Polisi, Masauni alisema Jeshi la Polisi limo kwenye utaratibu wa kuwachukulia hatua za kisheria askari wachache, wanaochafua taswira na kazi nzuri inayofanywa na Polisi kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu kwa kujihusisha na vitendo vinavyokinzana na maadili.
Kuhusu uhakiki wa vyeti, waziri huyo alielezea kuwa, uhakiki huo unahusu askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi unaendelea na mpaka sasa, askari 19 wamechukuliwa hatua za kisheria baada ya kugundulika kuwa walipata ajira kwa njia zisizokubalika.
Kuhusu uhaba wa askari wa kike, Waziri huyo alikiri kuwa kuna uhaba wa askari wa kike katika Jeshi la Polisi na kutoa mwito kwa wanawake wahamasike zaidi kujiunga na vyombo vya usalama.
Mwaka jana Idara ya Uhamiaji iliyokuwa chini ya Wizara hiyo, ililazimika kufuta ajira mpya 200 za makonstebo na makoplo, baada ya kubaini upatikanaji wa ajira hizo, ulifanyika kwa upendeleo.

MAGAZETINI:#Mapato hospitali yanuka ufisadi

Imeandikwa na Halima Mlacha, Dodoma.

UFUNGAJI wa vifaa vya kielektroniki katika hospitali za Serikali katika mikoa mbalimbali, umeibua fukuto la ufisadi mkubwa, uliokuwa ukifanywa katika makusanyo ya fedha wanazolipa wagonjwa kwa ajili ya huduma.
Akizungumza bungeni mjini hapa jana katika kipindi cha maswali na majibu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema tangu mfumo huo wa kielektroniki uanze kutumika katika hospitali nyingi nchini, mapato yameongezeka.
Jafo alisema mafanikio hayo ya ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa elektroniki, yamesababisha katika sekta ya afya kwa sasa ajenda kuu iwe kuongezea mapato ya hospitali zote nchini, kuendane na utoaji wa huduma bora.
Hospitali ya Rufaa Mbeya Akitoa mfano wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Jafo alisema kabla ya kufungwa kwa vifaa hivyo, ilikuwa ikikusanya Sh milioni 70 kwa mwezi, lakini baada ya kufungwa vifaa hivyo, mapato yameongezeka zaidi ya mara saba na kufikia Sh milioni 500 kwa mwezi.
Taarifa zinaonesha pamoja na ongezeko hilo la mapato, bado hospitali hiyo iliendelea kukosa vifaa muhimu vya tiba, ikiwemo mashine ya CT-Scan, kiasi cha kusababisha mwanzoni mwa mwaka huu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla kuwajia juu watendaji wake.
Dk Kigwangalla alielezea kushangazwa kuona hospitali hiyo ikikusanya Sh milioni 500 kwa mwezi, huku ikidai kukosa CT-Scan na kutoa siku 60 kifaa hicho kifungwe. Katika maelezo aliyopewa, Dk Kigwangalla alielezwa kuwa ingawa ni kweli hospitali hiyo inakusanya Sh milioni 500 kwa mwezi, lakini mahitaji ya dawa pekee yanachukua zaidi ya Sh milioni 300, kabla ya gharama nyingine ikiwemo za usafiri wa magari.
Alielezwa kuwa hospitali hiyo imejipanga kuchukua mkopo kutoka Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF), kwa kuwa ili kupata mashine hiyo, wanapaswa kuwa na kuanzia Sh milioni 800 mpaka Sh bilioni 1.2.
Sekou Toure Mbali na Mbeya, katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure kwa mujibu wa Jafo, kabla ya kufungwa kwa vifaa hivyo, ilikuwa ikikusanya kati ya Sh 150,000 mpaka 200,000 tu kwa siku.
Jafo alisema baada ya kufungwa vifaa hivyo, mapato hayo yaliongezeka mpaka karibu mara 21 na kufikia Sh milioni 3.2 kwa kila siku. Hospitali ya Tumbi Mbali na Mwanza, Naibu Waziri huyo wa Tamisemi, alisema mkoani Pwani katika Hospitali ya Tumbi, nako kabla kufungwa vifaa hivyo, makusanyo yalikuwa Sh 200,000 kwa siku lakini baada ya kufungwa, mapato yakaongezeka mara 20 na kufikia Sh milioni nne kwa siku.
Kutokana na mafanikio ya hospitali hizo, Jafo aliwataka wabunge wote kufuatilia kwa makini hospitali katika halmashauri zao za wilaya, ili kila moja iweke mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kukusanya mapato katika huduma ya afya.
Aliwataka wabunge hao kuweka kipaumbele katika kuhakikisha hospitali zote katika maeneo yao, zinafungwa mifumo hiyo ya kielektroniki, ili fedha zikusanywe kusaidia katika kuboresha huduma za afya katika maeneo hayo.
“Tusipozingatia haya, hata tukipeleka fedha bado tutakuwa na matatizo, ndio maana ajenda yetu kuu ni kutumia mifumo ya kielektroniki, ili kuongeza mapato katika sekta ya afya,” alisisitiza.
Awali Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM), alitaka kufahamu kama Serikali haioni umuhimu wa kuiongezea fedha Hospitali ya Mji wa Mafinga, ili ihudumie kwa ufanisi idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudhuria hospitali hiyo.
Pia Mbunge huyo alitaka kufahamu kama Serikali iko tayari kuiongezea hospitali hiyo watumishi mara mbili zaidi ya kiwango inachopata, ili iwe na uwezo wa kutosha kukabiliana na mzigo wa kazi.
Akijibu maswali ya mbunge huyo, Jafo alisema Serikali imekuwa ikiipatia Hospitali ya Mji wa Mafinga Sh milioni 90 kwa ajili ya maendeleo na Sh milioni 90 kwa matumizi mengineyo ; na kwamba inaweza kuongezewa fedha hizo kulingana na wigo wa upatikanaji wa fedha.
Kuhusu watumishi, alisema hospitali hiyo ina watumishi 209 na upungufu uliopo ni wa watumishi 95, sawa na asilimia 31.3 na kwa mwaka wa fedha 2016/17 imeidhinishiwa kuajiri watumishi 18.

MAGAZETINI:#Rais ashtukiza uwanja wa ndege Dar

Imeandikwa na Mwandishi Wetu

RAIS John Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja dhidi ya dosari za ukaguzi zilizopo katika kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal One) jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa ilisema Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana, alipofanya ziara ya kushtukiza katika uwanja huo na kubaini kuwa mashine za ukaguzi za sehemu ya kuwasili abiria na mizigo, hazifanyi kazi kwa muda mrefu.
Maofisa wa uwanja huo waliokuwa wakitoa maelezo juu ya hali ya kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika uwanja huo, walikuwa wakitoa taarifa zinazotofautiana kuhusu utendaji kazi wa mashine za ukaguzi, hali iliyosababisha Rais Magufuli aamue kuiagiza wizara husika kwa kushirikiana na vyombo vya dola, kuchukua hatua mara moja.
“Unajua mimi sipendi kudanganywa, ni vizuri uzungumze ukweli tu, kwa nini nimeanzia hapa huwezi ukajiuliza? Eeeh sasa sipendi kudanganywa, ukinidanganya nitachukia sasa hivi, wewe umenidanganya kwamba hiyo ndio mbovu na hii ndio nzima, nikawaambia muiwashe hiyo nzima, akaja huyu mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema hii ni mbovu kwa miezi miwili.
“Kwa hiyo mizigo inayoingia humu huwa hamuikagui kwa namna yoyote ile, kwa hiyo mtu nikiamua kuja na madawa yangu ya kulevya, nikaja na dhahabu zangu, na almasi zangu na meno ya tembo kwa kutumia hizi ndege ndogondogo napita tu,” alisema Rais Magufuli kwa maofisa hao wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Rais Magufuli alifanya ziara hiyo ya kushtukiza baada ya kuwasili katika uwanja huo akitokea jijini Kampala nchini Uganda, ambako juzi alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni

MAGAZETINI:# Marais duniani wavutiwa na vita ya ufisadi Tanzania

Imeandikwa na Mwandishi Maalum, London

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema viongozi wakuu wa nchi na washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Rushwa, wamevutiwa na jitihada ambazo Tanzania imezichukua kukabiliana na janga hilo.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ushiriki wake kwenye mkutano wa siku moja wa wakuu wa nchi, ulioitishwakujadili suala la kupambana na rushwa duniani uliofanyika Lancaster House, jijini London, Uingereza.
Waziri Mkuu alisema katika kikao cha kwanza, kilichohudhuriwa na wakuu wa nchi na viongozi wa kitaifa wapatao 20, alipata fursa ya kuelezea jinsi Tanzania ilivyoweza kupambana na rushwa kwa kuzingatia vigezo vikuu vinne.
Waziri Mkuu alivitaja vigezo hivyo kuwa ni kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria zinazohusu masuala ya rushwa; uanzishwaji wa mahakama maalum ya mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi Julai, mwaka huu; mikakati ya udhibiti wa fedha za miradi ya wananchi na utaratibu wa kubaini wala rushwa kwa kushirikisha jamii ikiwemo kutunza siri za watoa taarifa.
“Ziko sheria ambazo zinafanyiwa kazi hivi sasa ambazo ni lazima zipitishwe na Baraza la Mawaziri kabla mahakama hii haijaanzishwa, zikishapitishwa na Baraza ndipo zitaanza kutumika,” alisema.
Akifafanua kuhusu mikakati ya udhibiti wa fedha za miradi ya maendeleo, Waziri Mkuu alisema kwamba katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imeongeza kiasi cha fedha zilizotengwa kwa shughuli za maendeleo kutoka asilimia 27 hadi kufikia asilimia 40.
Waziri Mkuu alisema alipata fursa ya kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron ambaye mbali na kupongeza juhudi za Serikali ya Rais John Magufuli katika kupambana na rushwa, pia aliahidi kutoa mwaliko ili Tanzania iweze kushiriki kwenye mkutano mwingine wa masuala ya rushwa utakaofanyika Japan, Julai mwaka huu.

Magazeti ya Leo jumamosi ya tarehe 14/05/2016

Usikose kusoma taarifa zilizotufikia punde "kunani kitaa" kila siku upate taarifa yakinifu zitajazokufundisha na kukuelimisha
Kikoti m blog tunakuletea unachokihitaji kwenye simu yako kwa hisani ya Airtel jipimie kifurushi unachokihitaji























Ijumaa, 13 Mei 2016

Maisha ni mipango - Chinga Wa DUCE aliyepata mafanikio kimaisha kupitia kazi ya kushona viatu



Picha : fundi viatu maalufu kama Chinga panda za DUCE




Tazama video ya kijana shupavu aliejiajiri Kwa kuchona Viatu vya wanachuo DUCE na kupata mafanikio makubwa