OFISI ya Rais, Utumishi na Utawala Bora imesema katika mwaka ujao wa
fedha 2016/17 inatarajia kuajiri watumishi wa sekta ya afya 10,870 kwa
ajili ya kupunguza pengo la uhaba wa watumishi katika sekta hiyo.
Hayo yalisemwa bungeni Dodoma juzi na Waziri wa wizara hiyo, Angella
Kairuki, wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha
2016/17.
“Nimesikia katika michango mingi wabunge wamezungumzia sana tatizo la
uhaba wa watumishi wa sekta ya afya. Waheshimiwa wabunge katika mwaka
ujao wa fedha sekta ya afya wataajiriwa watumishi 10,870,” alisema
Kairuki.
Alisema muda wowote kuanzia sasa ndani ya mwezi huu, vibali vya ajira
hizo vitatoka na wizara ya afya, itaendelea kuwapangia watumishi sehemu
zao za kazi. Kairuki alisema katika mgawanyo huo wa watumishi 10,870,
watumishi 3,147 ni wa kada mbalimbali 10 zinazohusu masuala ya
mbalimbali ya utabibu, wauguzi 3,985 na kada nyingine za mama cheza,
wataalamu wa viungo na famasia.
Alisema katika kuangalia namna serikali imekuwa ikitoa kipaumbele
katika utoaji wa ajira kwenye sekta afya, ndani ya miaka mitano serikali
ilitoa vibali vya ajira 52,947 na kati ya vibali hivyo walioweza
kuajiriwa ni wataalamu 38,047.
Kairuki alisema kati ya waajiriwa hao, ambao hawakuripoti ni 14,860 ;
na asilimia 71.93 ndio walioweza kuripoti. “Ukiangalia takwimu za mwaka
jana 2014/15 pamoja kwamba ikama zimejazwa na halmashauri zetu, ziko
kada zaidi ya 12 zenye wataalamu 335 hazikuweza kupata watu kabisa,
ukiangalia kada hizo hata mafunzo yake hapa nchini hayatolewi, kwa mfano
wataalamu kutoka kada ya biomedical engineers na wengine wengi,”
alisema.
Aidha alisema katika mwaka 2014/15, Serikali ilitoa kibali cha
watumishi 8,345, lakini katika soko la ajira kulikuwa na ukosefu wa
wataalamu katika soko hilo 4,467. Alitoa mfano wahitimu wa mwaka 2015/16
ni wataalamu 10,000 wakati Serikali imetoa kibali cha ajira cha
wataalamu 10,870.
Alisema katika mwaka wa fedha 2010/11, Serikali katika sekta ya afya
ilianza na watumishi 7,300, lakini katika mwaka ujao wa fedha idadi hiyo
itaongezeka na kufikia 10,870. Kairuki alisema serikali itaangalia
namna ya kuwapanga watumishi hao kwa kuzingatia maeneo
MIEZI michache baada ya Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia
(MCC) kujitoa kusaidia Tanzania katika usambazaji wa umeme vijijini,
Serikali ya Uingereza kupitia taasisi yake ya Energy Africa Initiative,
imetangaza utayari wa kutoa msaada huo.
Waziri wa Uingereza wa Maendeleo ya Kimataifa, Justine Greening,
ameeleza utayari huo mwishoni mwa wiki, katika mazungumzo yake na Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, aliye nchini humo kumwakilisha Rais John
Magufuli, katika mkutano wa kimataifa wa kupambana na rushwa duniani.
Katika mazungumzo hayo, Greening alimhakikishia Waziri Mkuu Majaliwa,
kwamba nchi yake iko tayari kuisaidia Tanzania kwenye mpango wake wa
kupeleka umeme vijijini.
“Tuko tayari kuwasaidia kutekeleza mpango huu kupitia taasisi ya
Energy Africa Initiative ambayo inapata ufadhili kupitia Shirika la
Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID),” alisema. Pia Waziri huyo wa
Uingereza, alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya
Tano katika kupambana na rushwa na kwamba ndiyo maana Tanzania ilipewa
mwaliko maalumu wa kushiriki mkutano huo, kwa vile baadhi ya mataifa
yanaziona juhudi zinazofanywa na Serikali ya Rais Magufuli.
Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu kwa nia ambayo
Serikali ya Awamu ya Tano imeionesha katika kuwa na mpango wa kuendeleza
viwanda. Nguvu mpya Rea Hatua hiyo ya Uingereza, imekuja wiki moja
kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini Alhamisi
wiki ijayo, ambayo mjadala wake utafanyika kwa siku mbili za Alhamisi
na Ijumaa, unatarajiwa kuibua hoja ya kufutwa kwa msaada huo wa MCC wa
Dola za Marekani milioni 472, uliokuwa utumike kusambaza umeme vijijini.
Mbali na mjadala huo ambao unatarajiwa kung’ang’aniwa na Kambi ya
Upinzani Bungeni, hatua hiyo ya Uingereza itaongeza nguvu katika
jitihada za Serikali zilizokwishaanza kwa mafanikio za kuwapatia
Watanzania umeme wa uhakika. Taarifa za Wakala wa Umeme Vijijini (Rea)
zinaonesha kuwa, pamoja na MCC kujitoa Machi mwaka huu katika usambazaji
umeme, Serikali katika Bajeti ya 2015/ 2016 inayoisha Juni mwaka huu,
ilikuwa imeshatenga Sh bilioni 950 kwa ajili ya mradi wa Rea Awamu ya
Pili.
Mradi huo wenye lengo la kufikisha umeme kwa vijiji 2,500 na
kuunganishia nishati hiyo wateja 250,000 nchi nzima, unatarajiwa
kukamilika Juni 30, mwaka huu na kupisha kuanza kwa Rea Awamu ya Tatu,
ambayo itaanza Julai mosi na kumalizika baada ya miaka miwili. Jitihada
zote hizo, lengo lake ni kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ya 2015-2020, ambayo inataka hadi ifikapo mwaka 2020, wananchi
waliounganishwa na umeme wafikie asilimia 60 na kiwango cha uzalishaji
kifike megawati 4,915.
Mbali na malengo ya Ilani hiyo, jitihada hizo pia zitachangia katika
kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa inayotaka Tanzania iwe nchi ya
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, ambayo imeweka lengo la usambazaji
umeme liwe asilimia 50 mwaka huo mwaka 2025 na asilimia 70 mwaka 2033.
Tayari Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
ameshaelezea nia ya Serikali kutaka sekta ya nishati itoe mchango mkubwa
kufikia uchumi huo wa kati, kwa kuwa rasilimali za kufikia lengo hilo
kupitia nishati zipo na kinachotakiwa ni dhamira na kasi ya kutekeleza.
Katika kusisitiza kasi na dhamira hiyo ya Serikali, Waziri huyo
amekuwa akielezea mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa dira
hiyo, iliyotaka ifikapo mwaka 2015 uunganishaji umeme uwe umefikia
asilimia 30. Lakini, kutokana na utekelezaji madhubuti wa dira hiyo,
kiwango hicho kilivukwa lengo na kufikia asilimia 40 mwaka 2015.
JPM na Marekani Mbali na msaada huo wa Uingereza katika kusambaza
umeme vijijini, Serikali ya Marekani pia imeelezea kuvutiwa na utendaji
wa Rais Magufuli katika kupambana na rushwa, hatua iliyoanza kuvutia
wawekezaji wa nchi hiyo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Masuala ya
Kimataifa, Sarah Sewall, katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu Majaliwa
nchini Uingereza katika mkutano huo wa kimataifa, ameipongeza Tanzania
kwa kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa.
Alisisitiza kuwa kampuni nyingi za Marekani, zimeonesha nia ya kuja
kuwekeza Tanzania. “Ninaamini uwekezaji huu utasaidia kuleta maendeleo
ya kiuchumi na kijamii kwa watu. Tunampongeza Rais Dk Magufuli kwa
juhudi anazofanya na nipende kusisitiza kwamba ushirikiano baina ya
Tanzania na Marekani utaendelezwa katika maeneo yetu ya siku zote,”
alisema.
Majaliwa ashukuru Akizungumza katika kikao chake na Waziri Sewall,
Waziri Mkuu Majaliwa alimsisitiza asiache kusaidia kuwahimiza Wamarekani
wengi waje kutalii Tanzania na wawekezaji zaidi waje kuwekeza nchini
katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uanzishaji wa viwanda, uongezaji
thamani kwenye mazao yanayozalishwa nchini.
Alimhakikishia kuwa Watanzania wamekuwa wakijifunza teknolojia mpya
na za kisasa. Kuhusu mafanikio katika mapambano na rushwa, Majaliwa
alisema mkutano huo wa kimataifa, uliojadili jinsi ya kupambana na
rushwa duniani, ni kiashiria tosha kwamba tatizo la rushwa ni kubwa na
linataka juhudi za pamoja katika kukabiliana nalo.
Akizungumza na mawaziri hao, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwamba
viongozi wa Serikali wa Awamu ya Tano, wameamua kwa dhati kupambana na
kila ovu, linalotokana na janga la rushwa na wameamua kuwajibika na
kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
“Sasa hivi nchi yetu ina utamaduni mpya wa kufanya kazi na tumeamua
kufanya kazi kwelikweli na siyo tena kwa mazoea, tumeamua kuweka
utamaduni mpya wa kupiga vita rushwa, ili kuleta uwajibikaji na uwazi
miongoni mwa watu wetu,” alisema.
Alipoulizwa nini kimechangia kufanya Tanzania ing’are kimataifa
katika vita hiyo, Waziri Mkuu alijibu kwamba Tanzania imetumia mambo
manne ambayo ni kuzuia rushwa isitolewe ama kupokelewa, kampeni za
kuelimisha jamii, kufanya mapitio ya sheria na kuwepo kwa utashi wa
kisiasa.
“Serikali inachukua hatua za kiutawala na kisheria, kama vile
kuanzisha Mahakama Maalumu ya Mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi
Julai mwaka huu,” alisema Waziri Mkuu.
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amefichua kuwa amekuwa
akipigiwa simu na baadhi ya wafanyabiashara vigogo wenye nia ya kutaka
kupunguza makali ya operesheni inayofanywa na wilaya yake dhidi ya
waficha sukari.
Kwamba simu hizo amekuwa akipigiwa hadi usiku wa manane na huku
wengine wakimtumia ujumbe mfupi wa simu wa maandishi (SMS). Amekemea
wafanyabiashara hao na kutaka waache mara moja mchezo huo, kwani vyombo
vya dola vinaendelea kuwafuatilia.
Hapi alisema hayo jana wakati akizungumzia suala la Uadilifu kwenye
Mkutano wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini na
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wanaotokana na
shirikisho hilo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alibainisha kwamba amekuwa hapokei
simu hizo na SMS hizo za wafanyabiashara wakubwa kutokana na sababu
mbalimbali. “Sababu ya kwanza sina sababu ya kuzipokea, lakini pili
nahofia nikizipokea nitarekodiwa na wafanyabiashara hao na sauti yangu
itasambazwa kwenye mitandao, kuonesha nipo pamoja nao.
“Wakati mwingine mpaka usiku wa manane wanapiga simu na kutuma meseji
na wengine wanajitambulisha. Lakini huwa namuonyesha mke wangu na
kumwambia sina sababu ya kuzipokea, kwani naweza nikapokea lakini katika
mazungumzo yetu nikasema neno ‘sawa’, kisha neno hilo linaweza
kusambazwa katika mitandao kuonyesha kwamba nia yetu ni moja ya kuficha
sukari”, alisema Hapi.
Alisema hao wafanyabiashara wanaoficha sukari, wanaleta madhara
makubwa kwa jamii na uchumi wa nchi, kama vile kuua viwanda vya sukari
nchini. Alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakiweka ‘oda’ katika
viwanda vya sukari kuchukua bidhaa hiyo, lakini hawaendi kuichukua kwa
madai ya kwenda kuichukua siku za baadaye, lengo likiwa kuificha. Hapi
aliwaomba wakazi wa wilaya ya Kinondoni, kuendelea kuisaidia serikali
kufichua watu wote walioficha sukari.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye (aliyevaa tai) akiwa katika picha ya pamoja na
baadhi ya wamiliki wa Blogs (Bloggers) aliowaalika wakati wa
kuwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa
mwaka wa Fedha wa 2016/2017, bungeni Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa
wizara hiyo,Annastazia Wambura. Baadhi ya Bloggers wakiwa bungeni wakati wa Bajeti ya wizara hiyo Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi 'Mr Sugu' akisoma taarifa
ya maoni ya upinzani kuhusu wizara hiyo.
KLABU ya soka ya Azam FC ya Dar es Salaam imepata makocha wawili
kutoka klabu ya Deportivo Tenerife ya Hispania. Makocha hao Zebensul
Hernandez Rodriguez ambaye atakuwa Kocha Mkuu na Jonas Garcia Luis kocha
wa viungo, waliwasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam
jana na kupokewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Saada Kawemba.
Kwa mujibu wa Kawemba watafanya mazungumzo na makocha hao na kama
watakubaliana watawachukua ili wainoe timu yao. Kocha wa sasa wa Azam
FC, Muingereza Stewart Hall amesema ataondoka katika klabu hiyo mwishoni
mwa msimu wa ligi.
“Wamekuja kwa ajili ya mazungumzo, tukikubaliana tutawachukua kwa
ajili ya timu yetu,” alisema Kawemba. Kwa upande wake Rodriguez alisema
amefurahi kuja nchini kwani anaamini kuna vipaji vya soka kwa jinsi
walivyomuona mchezaji Farid Mussa wa Azam ambaye anafanya majaribio
katika timu yao.
Farid Mussa ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania
‘Taifa Stars’ amefuzu majaribio katika klabu hiyo iliyopo Ligi Daraja la
Kwanza nchini Hispania na kilichobaki ni mazungumzo baina ya Azam na
klabu hiyo kuhusu mauzo ya mchezaji huyo.