ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 19 Mei 2016

MAGAZETINI:#RC awatuliza walimu kwa ‘kutemwa’ mabasi ya kasi

Imeandikwa na Sophia Mwambe
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewatoa hofu walimu wanaotumia mabasi ya haraka kuwa na subira ili waangalie utaratibu wa kuwasaidia walimu hao, ambao awali walikuwa wakipanda daladala bila kulipa nauli.
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu muafaka wa awali wa walimu kupanda bure daladala baada ya yeye (Makonda) na wamiliki wa gari hizo, kukubaliana kuwasafirisha bure.
Alisema sasa ni mapema kuanza kuzungumzia suala la walimu katika mabasi yaendayo haraka, hivyo aliwataka walimu wanaotumia usafiri huo kuwa na subira kwa kipindi hiki. “Mradi huu wa UDART ndio kwanza unaanza na bado una changamoto zake, hatuwezi kusema leo walimu waanze kupanda bure, mabasi haya pia yana uongozi wake na taratibu zake, lazima tukae tuzungumze nao ili tuone tutafanyaje kuhusu walimu,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa Serikali inamiliki kwa asilimia 49 katika UDART na wenye mradi huo wanamiliki asilimia 51, hivyo lazima kuwepo na utaratibu ambao pande zote kukubaliana kuhusu suala la walimu. Kauli hii ya Makonda imekuja baada ya mradi huo wa mabasi yaendayo haraka, kutoitambua ofa ya walimu hao kupanda bure.
Baada ya kauli hiyo ya Makonda, gazeti hili lilitembelea maeneo mbalimbali yanapopita mabasi hayo, kuangalia hali ya usafiri na changamoto zinazoukabili maradi huo. Gazeti hili lilipita katika vituo vya Feri, Kariakoo, Fire, Ubungo, Kimara na Morocco na kukuta wananchi wakiwa wanakata tiketi kwa foleni na kupanda katika mabasi hayo kwa utaratibu bila usumbufu.
Changamoto kubwa kwa mabasi hayo ni kuwa bado wamiliki wengine wa vyombo vya usafiri, ikiwemo pikipiki, magari madogo na maguta, wakiendelea kutumia njia hiyo ambayo wameonywa kuitumia.
Tatizo lingine ni ukosefu wa umeme katika daraja la juu lililopo Kimara, hivyo kusababisha abiria wengi kukataa kutumia daraja hilo. Wengi walishutumu wenye mradi huo, kushindwa kuweka taa kwenye njia ndefu za juu za daraja hivyo, hivyo kuwatia hofu abiria.
Tatizo lingine katika kituo hicho cha Kimara ni uchafu katika daraja hilo la juu, ambalo limejaa vumbi jingi na makaratasi. Uchafu huo hauzolewi na vumbi nalo halisafishwi na hakuna deki inayopigwa, hivyo vumbi imejaa kila kona. Pia, kituo hicho cha Kimara hakina maji hadi vyooni, hivyo hali ya usafi ni mbaya

MAGAZETINI:#Lowassa atajwa kununua nyumba ya serikali

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Dodoma.
MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM), Ritha Kabati amemtaja aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa kuwa alinunua nyumba ya serikali iliyouzwa mwaka 2002 yenye jengo namba 68.
Kabati alisema hayo wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano jana na kueleza kuwa katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni walieleza suala la ununuzi wa nyumba za serikali.
Alisema hotuba hiyo ilisema nyumba za serikali 7,921 ziliuzwa tangu mwaka 2002 hadi 2004 na kutaka serikali ya awamu ya tano kurejesha nyumba hizo kutokana na walionunua kukiuka mikataba na malengo ya mauzo.
“Naomba niwaambie ukiwa usiangalie boriti lililo katika jicho la mwenzako wakati kwako lipo, kwani hata mgombea wao wa urais Edward Lowassa alihusika kwa kununua nyumba ya plot namba 68 na Fredrick Sumaye alikuwa Waziri Mkuu na kuhusika kuuza nyumba hizo,” alisema Kabati.
Baada ya kueleza hayo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) aliomba kumpa taarifa mbunge huyo kuwa taarifa hiyo ni kwa maslahi ya taifa, hata kama mhusika atakuwa katokea kambi ya upinzani sheria itachukua hatua.
Awali katika michango mbalimbali ya wabunge wa upinzani wamekuwa wakilalamikia kuuzwa nyumba hizo za serikali na kudai kuwa watumishi wapya wengi walioajiriwa, wamekuwa wakikosa maeneo ya kuishi.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) akichangia mjadala huo alilalamikia kuuzwa kwa nyumba hizo pamoja na nyingine za Tazara zipatazo 500 na kuamua kumpatia Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano ripoti aliyodai inaonesha nyumba hizo zilivyouzwa.

MAGAZETINI:#Mamia wafurika Moro kortini kesi ya waliorekodi video ya ngono


Imeandikwa na John Nditi, Morogoro

WATUHUMIWA sita kati ya 11 wa udhalilishaji, ubakaji na usambazaji wa picha za video, zikimwonesha msichana mwenye umri wa miaka 21, akilazimishwa kufanya mapenzi eneo la Dakawa, Morogoro wamepandishwa kizimbani. Imebainika kuwa miongoni mwa makosa yanayowakabili, lipo pia la kulawiti.
Mamia ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro walifurika katika jana katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, kushuhudia watuhumiwa hao wakipandishwa kizimbani. Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na walisomewa mashitaka yao na mahakimu wawili tofauti katika vyumba vya mahakama hiyo.
Wawili katika watuhumiwa hao, wanakabiliwa na shitaka la kubaka , kulawiti na kupiga picha za video za kujamiiana na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii. Walioshitakiwa kwa kosa kumlawiti na kumbaka msichana huyo kisha kupiga picha za video wakati wakifanya tendo la kujamiiana kwa lengo la kuzisambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii, ni Idd Adamu (32) mkazi wa Makambako, mkoani Iringa na Zuberi Thabiti (30) mkazi wa Mbalali, mkoani Mbeya.
Ulinzi katika viwanja vya mahakama hiyo, uliimarishwa huku wananchi na waandishi wa habari, wakizuiwa kuingia kusikiliza kesi hiyo ikisomwa ndani ya mahakama. Hali hiyo ilielezwa na uongozi wa mahakama kuwa inatokana na matakwa ya sheria ya makosa ya ubakaji na ulawiti, kuzuia kesi hiyo kusomwa hadharani.
Watu walijaa kila kona na ilielezwa kuwa kesi hiyo ni ya aina yake, kutokana na kugusa hisia za wengi. Baadhi ya watu nje ya mahakama, walionekana wakilia na miongoni mwao walidai wanamuonea huruma msichana aliyetendewa unyama huo, kwani baadhi ya wahusika waliosambaza picha hizo mitandaoni, wana undugu na msichana huyo.
Akisoma shtaka linalowakabiliwa watuhumiwa wawili wa makosa ya ubakaji, ulawiti na kupiga picha za video wakati wakifanya tendo la kujamiiana kwa lengo la kuzisambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii, Wakili wa Serikali, Gloria Rwakibalila mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa, Mary Moyo, alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Aprili 27, mwaka huu.
Alidai watuhumiwa walitenda kosa hilo Aprili 27 , mwaka huu majira ya jioni katika nyumba ya kulala wageni iliyofahamika kwa jina la Titii iliyopo Dakawa wilayani Mvomero. Aidha, watuhumiwa hao wawili waliunganishwa na watuhumiwa wengine wanne waliofikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Ivan Msack kwa kosa la kusambaza picha za video za kujamiiana kwenye mitandao ya kijamii, ikiwamo ‘WhatsApp’, jambo ambalo ni kosa chini ya Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015 Kifungu Namba 14 (1b) na (2b).
Washtakiwa hao ni Rajabu Salehe (30), Ramadhan Ally (26), Musini Ngai (36) na John Peter (26), wote wakiwa ni wakazi wa Dakawa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Alidi kuwa washitakiwa hao wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo katika nyakati tofauti kati ya Aprili 28 hadi 30, mwaka huu, ambapo walisambaza picha hizo huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, ambapo wote walikana, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Gloria Rwakibalila, Edga Bantulaki na Calstus Kapinga, uliwasilisha mahakamani hapo hati ya zuio la dhamana kwa washtakiwa hao.
Katika hati hiyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa endapo washtakiwa hao watakuwa nje kwa dhamana, wataharibu upelelezi wa kesi hiyo na pia kutahatarisha usalama wa mlalamikaji na washtakiwa hao, kutokana na kesi hiyo kuvuta hisia za watu wengi.
Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni Mosi mwaka huu, itakapotajwa tena na kusikiliza suala la dhamana, kufuatia maamuzi ya maombi hayo ya pande mbili. Washitakiwa wote sita walirudishwa rumande.
Wakati kesi ikiendelea mahakamani hapo baadhi ya watu waliokuwemo waliangua kilio huku baadhi yao walisikika wakidai kuwa baadhi ya washitakiwa waliosambaza picha wanauhusiano wa kindugu na binti huyo.
Katika hatua nyingine, kabla ya kufikishwa watuhumiwa hao mahakamani, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alikutana na waandishi wa habari na alisema kuwa kati ya watuhumiwa 11 waliokuwa wamekamatwa, sita upelelezi wake ulikamilika. Alisema watuhumiwa wengine watano, upelelezi unaendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani.

                                                      TANGAZO
                            NEW  MWALIMU EDUCATION CENTRE
Mahali: Ilula madizini katika majengo ya kanisa katoriki kigango cha madizini karibu na soko la TASAF.
Inawatangazia kuwa inaendelea na utoaji wa huduma (tuition) kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita: tuition hii ni mahususi kwaajili ya likizo ya mwezi wa sita itaanza usajiri wake kuanzia tarehe 30/05/2016.
Ada ni shilingi Elfu kumi(10,000) kwa muda wote wa likizo
- kwa wanafunzi wa kidato cha nne(form 4) tutafanya solving ya past paper na maswali mbalimbali
pia mwanafunzi atapewa peni bure na notes zilizo andaliwa na walimu mahili mara tu baada ya kufanya usajiri. Nyote mnakaribisha kwa mawasiliano piga simu no +255769694963 au +255784428256.

MAGAZETINI:#Zitto, Mdee, Heche wawekwa kitimoto

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo) na wenzake wawili, jana wamehojiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika kwa kufanya fujo bungeni kuhusu suala la Bunge kutorushwa ‘live’.
Mbali na Zitto, wengine waliohojiwa ni pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema). Wabunge hao walihojiwa kwa tuhuma za kufanya fujo bungeni wakati ilipotolewa hoja ya Bunge kutorushwa moja kwa moja ‘live’, akiwa pamoja na wabunge wawili; Mdee na Heche.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya kamati hiyo, kimesema Zitto alihojiwa na kamati hiyo kwa muda wa zaidi ya saa moja kwa makosa mbalimbali, ikiwamo kufanya fujo bungeni Januari 27, mwaka huu.
Taarifa hizo zilieleza kuwa Zitto alifanya fujo hizo baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, kuahirisha kujadili hoja ya serikali iliyowasilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kuhusu Bunge kutorushwa ‘live’.
Hatua hiyo inatokana na hoja iliyowasilishwa na Zitto aliyetaka kuahirishwa kujadili hotuba ya Rais kutokana na kauli ya Waziri Nape ya kutorushwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.
Zitto, alihojiwa na kamati hiyo ya Mkuchika kwa kilichoelezwa alisimama na kuomba mwongozo kuhusu jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi kinyume na Kanuni ya 72 (1) na 68 (10 ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016.
Mbali na hilo pia anadaiwa kusimama na kuzungumza bila utaratibu kinyume na Kanuni ya 60 (2) na 12 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, jambo ambalo lilileta fujo na kuvunja shughuli za Bunge.
Katika barua za mwito zilizosainiwa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah, Mei 12, mwaka huu, inaelezwa kwamba pamoja na mambo mengine na Mwenyekiti wa Bunge kumsihi mbunge huyo bado aliendelea kuzungumza na kusimama ikiwa ni kuonesha dharau kwa mamlaka ya Spika na shughuli za Bunge kinyume na kifungu namba 24 (d) na (e) cha Sheria ya Kinga na Haki za Bunge.
Barua hiyo ilieleza kuwa kutokana na vitendo hivyo vinavyokiuka Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, Sura namba 296 na Kanuni za Bunge, wabunge hao walionywa kuwa endapo wasingefika mbele ya kamati hiyo jana hatua za kisheria zingechukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa kifungu cha 15 na 31 (1)(a) na sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge.

Magazeti ya Leo Alhamisi ya tarehe 19 may 2016

                              NEW  MWALIMU EDUCATION CENTRE
Mahali: Ilula madizini katika majengo ya kanisa katoriki kigango cha madizini karibu na soko la TASAF.
Inawatangazia kuwa inaendelea na utoaji wa huduma (tuition) kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita: tuition hii ni mahususi kwaajili ya likizo ya mwezi wa sita itaanza usajiri wake kuanzia tarehe 30/05/2016.
Ada ni shilingi Elfu kumi(10,000) kwa muda wote wa likizo
- kwa wanafunzi wa kidato cha nne(form 4) tutafanya solving ya past paper na maswali mbalimbali
pia mwanafunzi atapewa peni bure na notes zilizo andaliwa na walimu mahili mara tu baada ya kufanya usajiri. Nyote mnakaribisha kwa mawasiliano piga simu no +255769694963 au +255784428256.




















Jumanne, 17 Mei 2016

Yanga yatua Angola, yaahidi ushindi kesho

Imeandikwa na Zena Chande TIMU ya soka ya Yanga, imetua salama Angola huku kocha wake mkuu, Hans van Pluijm akiahidi kuwaangamiza wenyeji wao Sagrada Esperanca katika mchezo wa marudiano wa mtoano kuelekea hatua ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kesho.
Yanga ambayo mwishoni mwa wiki ilisherehekea kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara 26, ikiwa ni rekodi kwa klabu za Tanzania, iliondoka nchini jana mapema asubuhi.
Akizungumza na gazeti hili juzi kabla ya kuondoka nchini, Pluijm alisema anatambua ugumu wa mechi hiyo hasa kwa vile watacheza ugenini, lakini akaahidi ushindi ni lazima.
“Tunakwenda kucheza ugenini mechi itakuwa ngumu kwa vile wenzetu wanacheza kwao, lakini nafurahi kitu kimoja kwamba wachezaji wangu wanakwenda wakijiamini zaidi kutokana na kutwaa ubingwa, sidhani kama watakubali kufungwa kirahisi, bado wana morali ingawa najua wanaweza kuja na mbinu mpya, lakini hata sisi tumejiandaa,” alisema.
Yanga inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa mbele kwa mabao 2-0 iliyoyapata katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuhitaji ushindi au sare ya aina yoyote kuweza kuandika historia ya kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo inayokwenda sambamba na utajiri mkubwa wa fedha, kwani ukiachilia mbali kitita cha dola za Marekani 150,000 kwa kila timu itakayofuzu hatua hiyo, timu zitaogelea fedha ikiwa ni pamoja na bingwa kutwaa dola 625,000 (Sh bilioni 1.36), wakati mshindi wa pili atapata dola 432,000 (Sh milioni 907).
Mbali ya morali ya ushindi katika mchezo wa kwanza, Yanga inakwenda ikiwa na nguvu ya ziada ya nyota wake wawili, mshambuliaji Donald Ngoma na kiungo Thabani Kamusoko ambao walioukosa mchezo wa kwanza kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja.

Mahausigeli 15 waliokuwa wakipelekwa Oman wanaswa

Imeandikwa na Sophia Mwambe JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata wasichana 15 katika nyumba iliyopo maeneo ya Ukonga, waliokuwa tayari kusafirishwa kwenda Oman kufanya kazi za ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Simon Sirro, alisema wasichana hao walikamatwa baada ya Polisi kupata taarifa toka kwa msiri kuwa kuna mtu amewaweka wasichana kwa ajili ya kuwasafirisha.
Sirro alisema Polisi walifuatilia na kufika katika eneo hilo na kufanikiwa kuwakuta katika nyumba ya Hadija Mohamed (40) wakiwa wamegawanywa katika vyumba viwili.
Alisema uchunguzi wa awali, umebaini kuwa mwanamke huyo anashirikiana na mwenzake Salma Habibu (43) mkazi wa Temeke kuwatafutia masoko nchini Oman na wao ni mawakala wanaoletewa kutoka mikoani na kuwapokea kwa ajili ya kuwasafirisha.
Aidha alisema watuhumiwa hao watapelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Pia ametoa onyo kwa watu wenye tabia hiyo kuacha, kwani wasichana hao wakifikishwa nje ya nchi hufanyiwa vitendo vya kikatili na unyanyasaji.
Katika tukio jingine, Polisi kanda hiyo imewakamata vijana 75, ikiwa ni muendelezo wa msako wa vijana wanaofanya matukio ya wizi wa majimbani nyakati za usiku.