Imeandikwa na Grace Mkojera na Mohamed Akida
JIJI la Dar es Salaam jana lilisimama kwa muda, wakati mabingwa wa
Tanzania, Yanga walipowasili wakitokea Angola walikofuzu hatua ya
makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC).
Mamia ya mashabiki wa Yanga walianza kumiminika Uwanja wa Ndege wa
Julius Nyerere, Dar es Salaam kuanzia saa tano asubuhi na hadi kufikia
saa nane mchana hali uwanjani hapo ilikuwa si ya kawaida.
Pia mashabiki wa Yanga walijipanga barabarani katika maeneo
mbalimbali kuanzia Uwanja wa Ndege, Kipawa, Vingunguti na Tazara, ambapo
mara kadhaa msafara wa basi la wachezaji wa Yanga uliokuwa ukiongozwa
na bodaboda kadhaa ulilazimika kusimama mara kwa mara sababu ya
mashabiki walikuwa wanataka kuwaona.
Kivutio kikubwa katika mapokezi hayo alikuwa kipa Deogratius Munishi
‘Dida’ aliyepangua penalti ya dakika ya 90, ambaye mashabiki walikuwa
wakimgombea kutaka kumbeba.
“Ahsanteni, nimefurahishwa na mapokezi, tulienda kufanya kazi ngumu,
tunawaahidi raha zaidi,” alisema Dida na kuungwa mkono na Haruna
Niyonzima kiungo mahiri wa Yanga na kiungo mwingine, Thabani Kamusoko.
Shamrashamra zilizopambwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali na
vijembe, sambamba na ngoma za singeli kwa mashabiki wa Yanga,
vilitawala.
Mashabiki walionekana karibu na lango la kutokea wageni mashuhuri
‘VIP’ wakisubiri kwa hamu kuwaona wachezaji ambapo saa 8.50 ndege yao
ilitua ikitokea Afrika Kusini na baada ya taratibu walitoka nje ya
uwanja na shangwe za: ‘Dida..Dida.. Dida’ zilisikika.
Mashabiki walikuwa wenye uso wa furaha wakizingira wachezaji
waliokuwa wakielekea kwenye gari lao, na bado utitiri ulisindikiza
msafara huo na kusalimiana na mashabiki, ambao walikuwa wakitembea kwa
miguu na wengine kwenye magari hadi kwenye Ofisi za Mwenyekiti wa Yanga,
Yusuf Manji Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam eneo la Banda la Ngozi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua, Kocha Msaidizi wa
Yanga, Juma Mwambusi alisema ushindi huo wametoa zawadi kwa Watanzania
wote.
Alisema wanashukuru sehemu ya mafanikio hayo yametokana na Mwenyekiti
Manji ambaye amekuwa akishirikiana nao katika kuhakikisha timu inafanya
vizuri.
Naye nahodha wa Yanga, Nadir Haroub alisema mechi ilikuwa ngumu kwani
hata waamuzi walionekana kuibeba timu pinzani, lakini wao walijua
kilichowapeleka na kupigana kwa ajili ya kufanya vizuri.
Wachezaji hao walizungumza na Mwenyekiti Manji kwa dakika kadhaa,
ambapo waandishi hawakuruhusiwa kuingia na baada ya kikao hicho Mkuu wa
Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema kila
mchezaji ameahidiwa gari.
“Wachezaji wamezungumza na Mwenyekiti na amewaahidi kuwapa kila mmoja
gari kwa hatua hii waliyofikia. Sasa ni gari gani hiyo itakuwa siku
nyingine. “Lakini nataka kuwahakikishia kwamba mtawaona wachezaji
wanabadilisha maisha yao muda si mrefu. Ila ninachotaka kuwaambia sasa
ni kwamba kila mchezaji ameahidiwa kupewa gari kwa kutinga hatua hii ya
makundi na amewataka wasibweteke. “Pia amewataka wasibweteke kwa kutinga
makundi, bali wapambane zaidi na hata msimu ujao wacheze makundi Ligi
ya Mabingwa Afrika,” alisema Muro.
Timu hiyo ilitarajiwa kuondoka jana jioni kwa ndege ya kukodi
kuelekea Songea ambako Jumapili itacheza na Majimaji katika kumaliza
Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga Jumatano ilifuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho
kutokana na matokeo ya mchezo wa uliofanyika mjini Dundo, Angola dhidi
ya Sagrada Esperanca ya huko, ambapo Yanga ilifungwa bao 1-0.
Kutokana na matokeo hayo, Yanga imefuzu kwa jumla ya mabao 2-1 baada
ya mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga
kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kwa kuingia hatua ya makundi, Yanga imeandika historia mpya katika
soka nchini kwa kuwa klabu ya kwanza Tanzania kufuzu hatua hiyo katika
mashindano hayo, lakini ni mara ya pili kufuzu hatua ya makundi kwa
mashindano makubwa Afrika baada ya kufanya hivyo mwaka 1998 katika Ligi
ya Mabingwa Afrika.
Simba ya Dar es Salaam nayo ilifuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa
Afrika mwaka 2003 kwa kuitoa Zamalek ya Misri. Yanga iliangukia Kombe
la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC), baada ya kutolewa na Al Ahly ya
Misri hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2,
ililazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-1
Alexandria, Misri.
Yanga sasa inaungana na miamba mingine saba Afrika na inasubiri droo
ya upangaji wa makundi wiki ijayo ili ijue itakuwa kundi gani.
Timu nyingine zilizofuzu hatua ya makundi na nchi zao katika mabano
ni MO Bejaoa (Algeria), Al Ahli Tripoli (Libya), FUS Rabat (Morocco),
Kawkab (Morocco), ES Sahel (Tunisia), Medeama (Ghana) na TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)