ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumanne, 28 Juni 2016

KUTOKA TAIFA: YANGA 0 VS TP MAZEMBE 1 (FULL TIME)



MPIRA UMEKWISHAAAAA
-SUB, Mazembe wanamuingiza Badibake
-KADI Assale analambwa kadi ya njanoDAKIKA 4+ ZA NYONGEZA
KADI Dk 89 Ulimwengu analambwa kadi ya njano
Dk 85 na 86, TP Mazembe wanaonekana kuupoza mchezo taratibu kama wameridhika na bao moja. Lakini Yanga wawe makini na mashambulizi ya kushitukiza

Dk 84, Ulimwengu anawatoka  Twite na Bossou na kupuga kupiga shuti, Yanga washukuru unatoka juu kidogo. Ilikuwa hatari sana
Dk 82, Kamusoko anapiga faulo safi kabisa hapa...goal kick
Dk 80, Niyonzima anaangushwa nje ya eneo la hatari, mwamuzi anasema faulo. Si mbali sana na lango la Mazembe
SUB Dk 78 Mazembe wanamtoa Adama Traore na nafasi yake inachukuliwa na Deo Kanda
Dk 76, Ulimwengu anaingia vizuri hapa anapiga shuti linakuwa butu
GOOOOOOOOOO Dk 73, Bope anaukwamisha mpira wavuni baada ya kujichanganya kuokoa baada ya mpira wa faulo
KADI Dk 72 Yondani analambwa kadi ya njano

Dk 72, Yondani anamuweka Ulimwengu chini hapa, inakuwa ni ni, faulo nje kudogo ya eneo la hatari
SUB Dk 71 Yanga wanamtoa Chirwa anaingia Simon Matheo
Dk 70, Assale tena, anaingia vizuri na kupiga shuti kali kabisa hapa
SUB Dk 69 Yanga wanamtoa Mahadhi aliyeumia na nafasi yake inachukuliwa na Mwashiuya
Dk 69, Ulimwengu anajaribu hapa shuti, goal kick
Dk 68, Ulimwengu anamtoka hapa Yondani lakini Kamusoko anawahi na kuokoa

KADI Dk 66, Twite anakuwa mchezaji wa kwanza kulambwa kadi ya njano
Dk 60 na 61, mashambulizi ya zamu kwa kila mlango, lakini hakuna shambulizi kali kwa kuwa mabeki wanaokoa kwa urahisi kabisa
Dk 59, kona inachongwa, Yanga wanachelewa kuokoa lakini Nekandio anashindwa kulenga lango na kuwa goal kick
Dk 58, pasi nzuri ya Mahadhi lakini Asale anatoa na kuwa kona, inachongwa, Koulibaly anaokoa

Dk 55, Kasusula anamuangusha Mahadhi hapa, mwamuzi anasema faulo, anaichonga faulo Niyonzima, lakini laini kabisa
Dk 53, Asalle akiwa nje ya 18 ya Yanga anaachia shuti kali lakini anashindwa kulenga lango
Dk 51 hadi 52, Yanga wanamiliki mpira kwa dakika mbili zote, hata hivyo mipango ya umaliziaji inaonekana bado
Dk 50, MAzembe wanapata kona, inachongwa na Asale, hatari hapa lakini Twite anaokoa
Dk 47, Mazembe wanaonekana kuanza kufanya mashambulizi na Yanga wanapaswa kuwa makini na mipira ya juu
Dk 45 Kipindi cha pili Yanga wanaonekana kuanza kwa kasi kabisa hapa. Ngoma anakwenda chini baada ya kuumizwa

MAPUMZIKO
-Nafasi nyingine bora kabisa, Yanga wanapoteza, Kaseke na Ngoma wanashindwa kuwa na mawasiliano ndani ya 18 ya Mazembe hapa

DAKIKA 1+ YA NYONGEZA
Dk 45, Asale anachonga kona nyanya kabisa hapa, inakuwa goal kick
Dk 44 KAsusula anaichonga vizuri, Dida anawahi kuanguka lakini anaugusa na kuwa kona, inachongwa Twite anaokoa, kona tena
Dk 43, Asale alikuwa anakwenda hapa lakini Mahadhi anamwangu na kuwa faulo
Dk 42 Ulimwengu anaingia vizuri akiwa amebanwa na Yondani lakini anafanikiwa kupiga shuti, si kali sana

Dk 39 hadi 41, bado hakuna ubunifu sana kwa kipa upande na muda huu wote mpira umechezwa katikati
Dk 37 na 38, TP wanaonekana kuupoza mpira huku wakijipanga kwa pasi za taratibu. Lakini mabeki wanafanya kosa hapa na kipa anatoka na kuokoa
Dk 36, Twite anapiga shuti kali la mpira wa adhabu...goal kick

KADI 35 Mpeko analambwa kadi ya njano kwa kumuangusha Chirwa
Dk Dk 34, krosi nzuri ya Juma Abdul, Ngoma anaukosa mpira akiwa hatua tatu kutoka langoni. Hii ni nafasi nzuri zaidi ambayo Yanga wamepoteza
Dk 30, Kaseke anaingia vizuri, kona. Inachongwa vizuri na Niyonzima lakini Mazembe wanaokoa hapa
Dk 28, Kamusoko anafanya kazi ya ziada kuondoa mpira miguuni mwa Traore, agauke na mpira na kuondosha
KADI Dk 27, Adama Traore wa MAzembe analambwa kadi ya njano kwa kumuangusha Juma Abdul

Dk 23 hadi 24, Yanga ndiyo wanaonekana kuucheza sana mpira, lakini bado hawana mipango ya umaliziaji
Dk 22 Chirwa anawatoka mabeki wa TP, kwake Ngoma, anapiga krosi safi, Mahadhi hatari hapa. Mpira anauwahi Niyonzima unarudi na kukumuta Juma Abdul, anapiga shuti linaokolewa, anapiga tena TP wanaokoa hapa

Dk 20, Traore anaingia tena kwenye lango anaingia na kupiga krosi safi, Dida anaokoa na Bossou anatoa na kuwa kona...
Dk 15, Niyonzima anaingiza krosi safi kabisa lakini kipa anatoka na kuokoa. ...faulo
Dk 12, Yondani anashika, mwamuzi anasema faulo kwenda Yanga, anapiga Kasusula, hovyoooo kabisa
Dk 11, hatari hapa, Chirwa anaingia lakini Mazembe wanaokoa, Mahadhi anaingia tena, kona. Inachongwa lakini haina matunda

Dk 9, Juma Mahadhi anaingia vizuri kabisa lakini MAzembe wanatoa na kuwa kona. Inachongwa, Bossou hatariiiii lakini inakuwa goal kick
Dk 7, Kipa Guela anafanya kazi ya ziada kuokoa mpira wa faulo wa Kamusoko na kuwa kona. Inachongwa vizuri hapa, goal kick..
Dk 5, Traore anaingia kwa kumtoka Juma abdul, anapiga krosi safi kabisa, kona. Inachongwa na Asale, off side
Dk 4, Mazembe wanagongeana vizuri na kuingia kwenye hatari la Yanga, mpira unatoka na kuwa goal kick lakini wachezaji wa TP wanalalamika kuwa ni kona

Dk 3, Yanga wanakuwa wa kwanza kujaribu, Juma Abdul anapiga shuti kali la mpira wa adhabu....juuu
Dk 2, hakuna timu iliyofanikiwa kugusa kwenye lango la mwenzake hadi dakika 2 na nusu za mchezo



Mechi ndiyo imeanza na kila upande unaonekana kuanza kwa umakini kabisa



Serikali mbioni kuruhusu matangazo ‘live’ redioni

Imeandikwa na Katuma Masamba

SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kuviruhusu vituo vya redio nchini, kurusha matangazo ya vikao vya Bunge moja kwa moja.
Hatua hiyo imekuja baada ya serikali kupokea maoni ya wadau mbalimbali ikiwemo wanahabari waliokwenda Dodoma, kuonana na Uongozi wa Bunge kujadili suala hilo la matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa studio ya kuzalishia vipindi ya Mtandao wa Redio za Jamii nchini (COMNETA) iliyopo Chuo Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam.
“Jambo moja ni kwamba kupitia studio za Bunge matangazo yatarushwa moja kwa moja na redio zote zinaweza kupokea matangazo hayo na zenyewe zikarusha. Hii itasaidia hata kupunguza gharama kwa sababu zamani ilikuwa ni lazima utume wa waandishi upeleke vifaa, sasa hii redio nyingi hasa hizi za kijamii haziwezi kumudu,” alisema Nape.
Alisema jambo hilo ni jipya na kwa sababu ni jipya, litakuwa na mapungufu mengi na kadri siku zinavyoenda lazima kuna wadau watakaojitokeza kwa ajili ya kuelezea mapungufu hayo, ambayo serikali itakuwa ikiyafanyia kazi.
Nape alisema serikali iko tayari kukaa katikati ya Bunge, wananchi na wadau wengine kwa ajili ya kuhakikisha wanapata haki yao ya kupata taarifa.
Hata hivyo, Nape aliwataka waandishi wa habari kuongeza uzalendo kwa nchi, kwani wanatakiwa kutambua kuwa mambo wanayoyaandika mwisho yanakuwa na matokeo chanya au hasi.
Akizungumzia studio hiyo, Nape alisema redio za jamii, zina mchango mkubwa hasa katika kukuza demokrsaia nchini na kuongeza uelewa kwa wananchi katika masuala mbalimbali.
Aliongeza kuwa uwekaji wa studio hiyo, utawasaidia hata wanafunzi wanaosomea fani ya uandishi wa habari katika chuo hicho, kuitumia katika kujitolea ili kuongeza uelewa wao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sanyasi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodriguez alisema, shirika hilo linafurahishwa na maendeleo ya redio hizo nchini.
Alisema, wamefurahishwa na jinsi serikali ilivyorudisha heshima kwa kuzitumia redio hizo katika kutoa taarifa mbalimbali bkwa wananchi na hata katika kipindi cha uchaguzi hilo lilionekana.
“…tunapongeza hilo lakini tunaiomba serikali iendelee kuzitumia redio hizi za kijamii ili kuifikia idadi kubwa ya wananchi hasa wale walioko pembezoni, sisi UNESCO tunaunga mkono redio hizi,” alisema Rodriguez.

Atakayempachika Mimba Mwanafunzi Kifungo cha Miaka 30 Jela

BUNGE limepitisha kwa kauli moja Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo mengine, imeongeza adhabu kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na mwanafunzi, sasa watafungwa jela miaka 30.

Sheria hiyo ilipitishwa jana bungeni mjini Dodoma baada ya Muswada kuwasilishwa Juni 24, mwaka huu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambao baadhi ya wabunge walipata fursa ya kuuchangia.

Muswada huo ulilenga kufanya marekebisho katika sheria 21 kwa lengo la kuondoa mapungufu yaliyobainika wakati wa utekelezaji wa sheria hizo na umepitishwa kuwa sheria.

Sheria zilizopendekezwa kurekebishwa na sheria hiyo ni pamoja na ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu; Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Binadamu; Kanuni za Madai; Usajili wa Makandarasi; Elimu; Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria ya Taasisi za Kazi.

Muswada huo uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju unatamka adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela katika marekebisho ya Sheria ya Elimu kwa watakaompa mimba, kumuoa au kuolewa mwanafunzi.

Awali adhabu iliyotamkwa katika sheria hiyo ya elimu ni mshitakiwa akibainika kuwa na kosa kutozwa faini ya Sh 500,000 na iwapo ni kosa la pili anatozwa faini ya Sh 500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu.

Akiizungumzia sheria hiyo inayosubiriwa kusainiwa na Rais John Magufuli, Masaju alisema inawalinda watoto wote chini ya miaka 18 walioko na wasio shuleni na kuwa kosa hilo likifanywa na mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto.

Kifungu cha 60 A (i) kimeeleza kuwa itakuwa kinyume cha sheria katika mazingira yoyote yale kwa mtu yeyote kumuoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya sekondari au ya msingi na atakayekiuka atafungwa jela miaka 30.

Katika Sheria ya Taasisi za Kazi inataka mwajiri anapokiuka masharti ya sheria ya kazi, ikiwa ni pamoja na kuchelewesha michango ya waajiriwa, kutoza faini na Ofisa wa Kazi ya papo kwa hapo isiyopungua Sh 100,000.

Wakichangia muswada huo, wabunge wameonesha furaha yao juu ya Sheria ya Elimu inayohusu adhabu ya miaka 30 jela. Hata hivyo, pamoja na furaha hiyo, baadhi ya wabunge wametoa angalizo la kutaka kupimwa kwanza DNA kabla ya kutoa hukumu huku wengine wakitaka kuwapo kwa nyongeza ya viboko.

Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM) alipongeza marekebisho hayo na kutaka adhabu ya miaka 30 iongezwe na kuchapwa viboko 12 kila mwezi mpaka aliyehukumiwa anamaliza kifungo kutokana na wahalifu hao kuwa na mazoea ya kuzoea gereza.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Subira Mgalu (CCM) alisema pamoja na serikali kuja na marekebisho hayo pia waangalie namna ya kukabiliana na utoro shuleni ili kuwafanya wanafunzi kupata elimu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Njombe Kusini, Edward Mwalongo (CCM) alitaka sheria imtake anayekutwa na kosa hilo kuacha fedha za fidia ambazo mama atazitumia wakati mwanaume akiwa jela.

Akijibu hoja ya kutumika kwa vipimo vya vinasaba (DNA), Masaju alisema kwa sasa utaratibu wa vipimo hivyo utatumika mahakamani na waendesha mashitaka kuhakikisha hawaachi shaka kwenye ushahidi kutokana na Tanzania kutokuwa na uwezo wa kumpima DNA mtoto akiwa tumboni.

Kuhusu Sheria ya Taasisi za Kazi, Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Chakoma (CCM), alitaka adhabu hiyo kuongezwa ili sheria kuleta tija na kutaka kazi ya kutoza faini hiyo isifanywe na Ofisa wa Kazi kama ilivyotamkwa katika sheria badala yake ifanywe na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA) kutokana na mifumo mizuri ya ufuatiliaji.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema serikali imekuja na sheria hiyo ili kuwabana waajiri wanaochelewesha michango ya waajiriwa na kuwa katika kutekeleza sheria waziri ataweka makundi na kuwa kampuni zenye kipato kikubwa adhabu yao itakuwa kubwa zaidi.

Magazeti ya Leo jumanne ya tarehe 28/06/2016
















Tumeweza kupanua wigo Kwa wasomaji wetu endelea kua nasi







Jumatatu, 27 Juni 2016

Madiwani Mwanza wapitisha mpango kabambe wa jiji


Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Mwanza

MADIWANI wa Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela wamepitisha Mpango Kabambe wa Jiji la Mwanza.
Mpango huo utahakikisha jiji na manispaa, zimepangwa kisasa kuondoa migogoro na kuongeza kasi ya ukuaji wa kiuchumi.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa wadau wa mpango huo hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema kuwa rasimu ya mpango huo, inahusisha mikakati na mapendekezo kutoka sekta tatu za maendeleo ya mji ambazo ni matumizi ya ardhi, usafirishaji na miundombinu.
“Huu ni mkutano wa sita wa mapendekezo ya rasimu ya mpango kabambe wa jiji la Mwanza na wa mwisho ili kuwa mpango kamili utakaotumika katika jiji la Mwanza kama sheria,” alisema Mongela.
Mongela alisema mpango huo wa kina wa matumizi ya ardhi, utatumiwa kama kichocheo cha kujumuisha ardhi inayohitajika kwa mapendekezo ya maendeleo mbalimbali katika sekta za usafirishaji na miundombinu.

Makinda: Wanawake viongozi kuweni chachu kwa wengine


Imeandikwa na Mwandishi Wetu

WANAWAKE waliopata nafasi za uongozi katika Bodi za Wakurugenzi kwenye mashirika na kampuni mbalimbali nchini, wamehimizwa kuonesha umahiri katika kazi ili kuwavutia wanawake wengine kufuata nyayo zao.
Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda, alisema wanawake katika ngazi za juu wana nafasi nzuri kuonesha njia kwa wenzao kufikia mafanikio.
Alikuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya Madola uliolenga kujadili na kushawishi wanawake kuingia kwenye uongozi.
“Ingawa katika nafasi za siasa na bunge hali si mbaya, takwimu zinaonesha wanawake wenye nafasi za uongozi kwenye Bodi za Wakurugenzi nchini ni ndogo,” alisema.
Alisema, jambo la msingi kwa waliopata fursa ni kufanya kazi vizuri na kuwa chachu kwa wengine kujitokeza na kuingia katika nafasi hizo.
Aliitaka Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania itumike kuwaelimisha na kuwashawishi wanawake wengine wasio viongozi kufikia nafasi hizo.
“Kwa sasa wanawake wengi wana elimu ya kutosha, lakini bado wana tatizo la kujiamini,” alisema na kuongeza kuwa, mikutano kama hiyo inawapa moyo wa kujiamini na kutaka kushika nafasi hizo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania, Said Kambi alisema, mkutano huo ulikuwa wa mafanikio makubwa na ulichokoza majadiliano na midahalo ya wanawake hapa nchini.
Alisema, wameanzisha kikosi kazi ambapo majumuisho yote yatapelekwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ili yafanyiwe kazi na kuongeza kuwa taasisi hiyo itashirikiana kwa karibu na kikosi kazi hicho.
Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Uratibu Uwezeshaji wa Wanawake katika fursa za uongozi Tanzania, Margareth Chacha, alisema wamejiandaa kuweka mikakati ya kuwaondolea woga wanawake na kuwasaidia katika nyanja mbalimbali.
Naye mmoja wa wajumbe, Dk Marina Njelekela alisema bado kazi kubwa inatakiwa kufanywa ili kuongeza mchango wa mwanamke katika maendeleo ya uchumi.
Mkutano huo uliandaliwa na Jumuiya ya Madola kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Watoto, Mamlaka ya Hisa na Uwezeshaji Mitaji na Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania.

Maeneo korofi kufikishiwa simu kwa satelaiti



 SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kutumia mtambo wa satelaiti, kufikisha huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo korofi nchini.
Maeneo hayo ni yaliyo kwenye changamoto za kijiografia yaliyopo maeneo ya mabondeni na milimani, ambako watoa huduma za simu wameshindwa kuyafikia kutokana na kutokuwa na mvuto wa kibiashara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustin Kamuzora alisema hayo mkoani Morogoro akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa minara ya simu ya Vodacom na Tigo katika kata za Kanga na Maskati wilayani Mvomero.
Mvomero ipo katika mradi wa mawasiliano vijijini wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Ziara hiyo iliongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Peter Ulanga na wahandisi wa minara hiyo kutoka kampuni za Tigo na Vodacom.
Profesa Kamuzora alisema ameridhishwa na kazi ya miradi hiyo baada ya kuikagua na kubaini mawasiliano yanapatikana. Alitaka kampuni zilizo kwenye mradi huo, kuhakikisha zinatatua changamoto ndogo zilizopo miradi hiyo iwe endelevu.
“Inabidi sasa kuangalia suala la matumizi ya satelaiti kwa maeneo ambayo jiografia yake ni ngumu, hasa kwa watu wanaokaa mabondeni. Nimeridhishwa na mradi hasa kwa namna walivyoamua kutumia teknolojia ya umeme wa jua katika minara yote,” alisema hayo akiwa kwenye mradi wa Maskati, uliopo kilometa 110 kutoka Morogoro mjini.