ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 30 Juni 2016

Wabunge watatu chadema wasimamishwa vikao, bunge laahirishwa

Imeandikwa na Jeremiah Vitalis
Wabunge watatu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamesimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge kwa muda tofauti kuanzia Juni 30, 2016.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi amesimamishwa kuhudhuria vikao 10 vya Bunge kufuatia kitendo cha kuonyesha kidole cha kati bungeni.
Joseph Mbilinyi alitenda kosa hilo alipokuwa akitoka nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kile alichoelezwa kuwa kuna mbunge wa CCM aliyemtusi mama yake.
Hukumu hiyo imesomwa na Naibu Spika wa Bunge Dr Tulia Ackson baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Bunge kueleza kuwa kamati hiyo ilijiridhishwa kuwa kitendo hicho ni kosa.
Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea na Mbunge  wa Simanjoro, James Ole Millya, Simanjiro wamesimamishwa kuhudhuria vikao vitano kila mmoja kwa makosa ya kusema uongo bungeni.
Wakati huo huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameahirisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja lililojadili na kupitisha bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2016/17.

Tundu Lissu apandishwa kizimbani, apata dhamana....Kesi yaahirishwa hadi Agosti 2

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjhSRStajo84WUxLUNtLDKwqUcTBXNNFEYRs83DD7FumyFSykojzJPvwubC60ceh-eiBWNs-5-11EGfIbj5_Su_NX8oD_eG09AzrYY3vPQKlNQR0ob1_cTVoPwKEo5byqvhPsZQUQc1UCQ/s1600/3.jpg

Tundu Lissu (48) amesomewa mashtaka ya kutoa lugha ya uchochezi ikiwemo kudharaulisha watanzania dhidi ya mamlaka halali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lissu alisomewa mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Juni 30, 2016.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Bernad Kongola akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga na Salum Mohammed.

Kongola alidai kuwa Juni 28,2016 eneo la Mahakama ya Kisutu Ilala Dar es Salaam mshtakiwa alitamka maneno ya dhihaka  kwa nia ya kushawishi na kudharaurisha watanzania dhidi ya mamlaka halali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alinukuu maneno ya Lissu kwamba"Mamlaka ya Serikali mbovu ya kidikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila mtanzania kwa nguvu zote, huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia  ndani ya giza nene"

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo.Upande wa jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na uliomba tarehe ya kusikilizwa maelezo ya awali.

Upande wa utetezi ukiongozwa na jopo la mawakili 11 akiwemo Michael Ngalo, Peter Kibatala na wenzao uliomba dhamana kwa mshtakiwa kwa kuwa ni mbunge atakuwa mwaminifu hataacha kufika mahakamani.

Hakimu Yongolo alisema mshtakiwa atakua nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya sh milioni 2.

Tundu Lissu alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhama, atasomewa maelezo ya awali Agosti 2,2016.

Magazeti ya Leo Alhamisi ya tarehe 30/06/2016























Jumatano, 29 Juni 2016

UKAWA Watishia Kumpeleka Rais Magufuli Katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC)


Wabunge wa Ukawa wamemtaka Rais John Magufuli kutoa tamko juu ya uvunjifu wa haki za binadamu Zanzibar na kwamba wana mpango wa kumpeleka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wakidai yanayotokea visiwani humo yana baraka zake. 

Katika mkutano wao na wanahabari jana, wabunge hao wamemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kwenda Zanzibar kujionea hali halisi badala ya kupata taarifa kutoka kwa wasaidizi wake. 
Hata hivyo, CCM imesema kuwa inalaani tamko hilo na kuwa kama Ukawa wanaona kuna masuala yanayohitaji kurekebishwa na kuhitaji hatua za haraka za Serikali watumie vyombo vinavyotambulika kisheria kama Bunge badala ya kuishia kulalamika “vichochoroni”. 
Akitoa tamko la wabunge hao jana, Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi) alieleza kuwa hali ya kiusalama inazidi kuwa mbaya Pemba na Unguja baada ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20 kutokana na baadhi ya wananchi kupigwa na vikosi alivyodai ni vya usalama. 
Mbatia alisema kuwa vikosi vya ulinzi hususani jeshi la polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo vya ukiukwaji wa haki za raia Pemba kwa zaidi ya miezi miwili kwa polisi kupiga mabomu ya machozi, kuwakamata ovyo wananchi, kuwapiga na kuwatesa na kisha kuwafungulia mashtaka bandia. 
Kutokana na vitendo hivyo, Mbatia alisema wabunge wa Ukawa wanapenda kusikia kauli ya wazi ya Dk Magufuli juu ya uonevu huo uliodumu kwa muda mrefu dhidi ya Wazanzibari na kutoheshimiwa haki za binadamu zikiwamo za kutoa maoni na kujikusanya. 
Mbatia, ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, alisema Rais anapaswa kutimiza wajibu wake kuhakikisha usalama wa raia kama anavyotakiwa kikatiba na kuhakikisha polisi wanawalinda wananchi na siyo kuwaonea. 
 
“Ukawa inasema wazi kuwa inaendelea kukusanya taarifa za vitendo vya ubakaji wa demokrasia na haki za binadamu ili kupata ushahidi wa kutosha wa kumfikisha Dk Magufuli ICC akajibu makosa hayo,” alisema Mbatia. 
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wabunge 66 waliosaini tamko hilo, Mbatia alisema Ukawa inamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu kuitoa amri ya kusitishwa kwa matendo hayo na achukue hatua dhidi ya askari wake ambao huwatesa raia ili kurudisha imani kwa wananchi. 
Alisema wananchi wa Pemba na Unguja waendelee kuikataa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa amani na pia wadumishe utaratibu wa kuheshimu sheria na kujizuia kufanya vitendo vya kukinzana na sheria. 
Lakini alipotakiwa kuzungumzia tamko hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alitupa lawama zote kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad. 
Alisema kuwa ndiye adui mkubwa wa Ukawa baada ya kususia uchaguzi wa marudio na kuhamasisha wananchi wasiitambue Serikali na sasa wafuasi hao wanatekeleza maagizo hayo kwa kukata mazao na kuleta fujo kwa wananchi wenzao. 
“Kazi ya dola ni kuhakikisha mtu havunji amani. Watu wanaofanya vitendo hivyo washughulikiwe ipasavyo na vyombo vya dola,” alisema Vuai. 
Alisema hakuna sababu ya kumpeleka Rais Magufuli katika mahakama ya ICC kwa kuwa anafanya kazi nzuri ya kuongoza nchi na kwamba kauli zilizotolewa na Ukawa ni za kitoto. 
Alivisihi vyombo vya dola kuendelea kuimarisha usalama visiwani humo ili watu wenye nia mbaya wasizoroteshe amani kutokana na matakwa ya viongozi wao. 

Awali katika mkutano huo, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh alisema wameamua kutoa tamko hilo kutokana na hali kuzidi kuzorota Pemba na kwamba ni lazima Serikali itekeleze wajibu wake kuzuia machafuko zaidi. 
Kuhusu mipango yao ya kumshtaki Rais, alisema kesi hiyo haina haraka kwa kuwa hata wajukuu zao wanaweza kuifungua kwa kuwa makosa ya jinai hayafi. 

“Baada ya kukusanya ushahidi wa kutosha na kujiridhisha kufanya hivyo, tutafanya. Tanzania siyo kisiwa ulimwengu mzima unaangalia nini kinaendelea Zanzibar, hivyo tusipowajibika, dunia itatuwajibisha,” alisema Saleh. 
Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuph Salim Hussein alisema vyombo vya usalama vimekuwa vikiwatuhumu wafuasi wa CUF kufanya vurugu hizo lakini tangu zianze tuhuma hizo hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kushtakiwa kwa uharibifu mali au fujo. 
“Tangu mwaka 1992 hizo tuhuma kuwa sasa hakuna mtu aliyewahi kushtakiwa mahakamani na kutiwa hatiani. Ni wao (Serikali) ndiyo wanawaonea wananchi,” alisema. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni alisema ni jambo la kusikitisha kuona viongozi wanawalinda wahalifu badala ya kuhimiza amani na usalama. 
Masauni alisema baada ya uchaguzi wafuasi wetu ndiyo wanafanya fujo hadi Machi 20 hali ilikuwa shwari Pemba laki ni viongozi wa CUF ndiyo chanzo cha matukio ya uhalifu unaoendelea Pemba baada ya Maalim Seif kwenda visiwani huko na kuwataka wasiitambue Serikali. 
“Hivi kabla ya tamko la Maalim Seif vikosi vya ulinzi na usalama havikuwapo ili vikakate mikarafuu na kuchoma nyumba za watu? Askari wetu wamefunzwa vizuri, wamekula kiapo kulinda usalama wa raia wote bila kujali chama,” 
Alisema nchi haiwezi kuendeshwa kwa kuacha watu wavunje amani na kwamba vyombo vya usalama vitamshughulikia mtu yeyote atakayekiuka sheria bila kujali chama.

Mahakama Kuu Arusha Yatengua ushindi wa Mbunge wa Longido, Onesmo Ole Nangole (CHADEMA), yaamuru kurudiwa uchaguzi katika jimbo hilo.

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgrIdlmr5RmpF25JWE6c3WcIlh1AhlBRxiNlq7huVQNEeCf2nz5JGgwlVfqyLLL6x14JA1rJqrWdPGqluIuO562uHcPmQvE7wHt9NxNX3f_AIJupEO-e1ycneRx1QIT2-4eMJar0GiXyY4/s1600/1.jpg

Kesi iliyokuwa inaunguruma kuanzia tarehe 29.02.2016 katika mahakam kuu jijini Arusha imetolewa hukumu leo hii

Katika shauri hilo aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM jimbo la Longido Dr KIRUSWA alifikisha mahakamni shauri hilo la kupinga matokeo ya ushindi dhidi ya mbunge wa Longido mh ONESMO NANGOLE

Akisoma hukumu hiyo,Jaji MWAGESI alisema kwamba mlalamikaji ndugu Kiruswa aliwakilishwa na Wakili Dr.Masumbuko Lamwai na Wakili Haraka.

Katika shauri hilo,dai la msingi la mlalamikaji bwana Kiruswa lilikua ni
1.Kutumika kwa lugha ya matusi na kashfa wakati wa kampeni kutoka kwa mh Onesmo Nangole
2.Kuwepo kwa wapiga kura kutoka nchi jirani ya Kenya walioletwa na Mh Nangole
3.kutumika kwa magari ya Chadema kwenye kusindikiza na kubebea masanduku ya kupigia kura
4.Mkurugenzi wa Uchaguzi kutangaza matokeo baada ya mgombea wa CCM kutolewa nje.
5.kutokea kwa vurugu ndani ya chumba cha kuhesabu matokeo

Kutokana na madai hayo na kwa kuzingatia kanuni,sheria na ushahidi uliotolewa pamoja na vielelezo na mashahidi wa pande zote mbili,Jaji kutoka mahakama kuu Bukoba Mh.Jaji Mwagesi alisema;
 
“Kutokana na kuzingatia viini vyote vya shauri hili kama vilivyosikilizwa na kwa mujibu wa sheria,Natamka kwamba;

Mahakama hii imetengua shauri hili na kwa kujirisha kwamba mchakato mzima haukuwa wa haki."

Magazeti ya Leo jumatano ya tarehe 29/06/2016













Pamoja tunasonga na kikoti.com





Jumanne, 28 Juni 2016

#WAZO LANGU# pongezi mliochaguliwa kidato cha tano lakini............


Imeandikwa na Ikunda Erick

UPO usemi usemao, Elimu ni Ufunguo wa Maisha. Usemi huu unatumika kama msisitizo wa umuhimu wa elimu kwa wale wanaopenda mafanikio katika maisha. Juzi mjini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene alitangaza matokeo ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo mbalimbali vya ufundi nchini.
Katika matokeo hayo, jumla ya wanafunzi 90,248 wamechaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2016, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.1 ikilinganishwa na wanafunzi 55,003 waliochaguliwa mwaka jana.
Mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka jana ni kwamba jumla ya watahiniwa 393,734 walihitimu kidato hicho, hii ina maana kwamba waliopata nafasi ya kuendelea kidato cha tano kupitia mfumo wa serikali ni hao wateule 90,248.
Hii ina maana kubwa kwa wale walio makini kufuatilia masuala ya elimu. Kwanza kwa wanafunzi waliopata nafasi watambue kuwa wamechaguliwa wao kutokana na bahati, kwani waliofaulu ni zaidi ya hao, ila uwepo wa nafasi ni chache.
Hivyo ni vyema, wanafunzi hao wakatumia nafasi hiyo kikamilifu kwa kuongeza juhudi kwenye masomo na kutilia mkazo elimu kwa sababu wakiichezea, watajuta na hivyo kuwa mwanzo wa kuharibu maisha yao ya baadaye.
Kama nilivyotangulia kusema, Elimu ni Ufunguo wa Maisha, ni wazi kwamba wale waliopata nafasi ya kuendelea kusoma ama kidato cha tano au chuo cha ufundi, kinachohitajika ni kutia nia, kusoma kwa bidii na kujiepusha na makundi mabaya ambayo yanaweza kuwapoteza na kuishia kuingia kwenye makundi yasiyofaa.
Ikumbukwe kwamba wapo kundi kubwa waliokosa nafasi ya kuendelea na masomo hayo sio kwamba wamefeli, la hasha bali ni kutokana na uhaba wa nafasi na kwamba huenda wakaishia hapo kutokana na sababu tofauti zikiwemo za wazazi kushindwa kumudu gharama za kuwasomesha shule binafsi za sekondari.
Sasa basi, rai yangu kwa waliopata nafasi, msiichezee na jambo la msingi kwa wazazi na walezi ni kuwa karibu na wanafunzi hao na kuwaeleza ukweli wa maisha yalivyo kwamba wajibu wao ni kusoma na sio kucheza na maisha.
Kwa wale watakaotia nia na kujituma ni wazi kwamba watafika mbali kielimu na wanaweza kuwa ufunguo huo waliopata wa kidato cha tano, ndio unaoweza kuwa ufunguo wa kuendelea hadi ngazi ya chuo kikuu na kuja kuwa na wasomi wenye ujuzi wa kujiajiri au kubahatika kuajiriwa, hivyo wasome kwa bidii badala ya kubweteka kwa kuamini hayo ndiyo mafanikio ya juu kielimu kwao.
Pia jambo muhimu kwa jamii yetu ni kwamba tushirikiane sote katika kuhakikisha kila tarafa katika maeneo yetu inakuwa na shule ya kidato cha tano na sita, ili kutoa nafasi ya wanafunzi wengi zaidi kuchaguliwa kuendelea na masomo hayo.
Kama kila mkoa, mji, wilaya na kata kwa ushirikiano wa viongozi wake wataweka msisitizo kwenye ujenzi wa madarasa kwa ngazi hizo, na jamii ikishirikishwa, ni wazi kwamba idadi ya wanafunzi watakaochaguliwa kuendelea na masomo hayo itaongezeka.
Mwito ni kwa jamii mzima kuona umuhimu wa kuchangia sekta ya elimu, ambayo hivi sasa agizo la Rais John Magufuli ni kwamba kila mkoa uhakikishe shule zilizopo kwenye maeneo yao zinakuwa na madawati ya kutosha, sambamba na vyumba vya madarasa.
Agizo hilo, linapaswa kutimia ifikapo Julai mwaka huu na lengo la Rais ni kuona sekta hiyo inakua na kwa kuanza tumeona juhudi zilizofanywa kwa serikali kufuta ada katika shule za msingi na sekondari, jambo ambalo limeongeza idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza.
Sasa basi, ongezeko hilo liwe na tija kwa kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake, kama mzazi kuhakikisha unafuatilia maendeleo ya watoto na kama mwanafunzi kusoma kwa bidii na walimu nao watimize wajibu wao kwa kutoa elimu stahiki. Kwa kufanya hivyo ni wazi kwamba tutajenga taifa lenye wasomi na kuondokana na uwepo wa watu wasio na elimu, ambao ni chanzo kimojawapo cha umasikini.