Wabunge wa Ukawa wamemtaka Rais John Magufuli kutoa tamko juu 
ya uvunjifu wa haki za binadamu Zanzibar na kwamba wana mpango wa 
kumpeleka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wakidai 
yanayotokea visiwani humo yana baraka zake. 
Katika mkutano wao na 
wanahabari jana, wabunge hao wamemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu
 Nchemba kwenda Zanzibar kujionea hali halisi badala ya kupata taarifa 
kutoka kwa wasaidizi wake. 
Hata hivyo, CCM imesema kuwa inalaani tamko 
hilo na kuwa kama Ukawa wanaona kuna masuala yanayohitaji kurekebishwa 
na kuhitaji hatua za haraka za Serikali watumie vyombo vinavyotambulika 
kisheria kama Bunge badala ya kuishia kulalamika “vichochoroni”. 
Akitoa 
tamko la wabunge hao jana, Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi) alieleza kuwa 
hali ya kiusalama inazidi kuwa mbaya Pemba na Unguja baada ya uchaguzi 
wa marudio wa Machi 20 kutokana na baadhi ya wananchi kupigwa na vikosi 
alivyodai ni vya usalama. 
Mbatia alisema kuwa vikosi vya ulinzi 
hususani jeshi la polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo vya 
ukiukwaji wa haki za raia Pemba kwa zaidi ya miezi miwili kwa polisi 
kupiga mabomu ya machozi, kuwakamata ovyo wananchi, kuwapiga na kuwatesa
 na kisha kuwafungulia mashtaka bandia. 
Kutokana na vitendo hivyo, 
Mbatia alisema wabunge wa Ukawa wanapenda kusikia kauli ya wazi ya Dk 
Magufuli juu ya uonevu huo uliodumu kwa muda mrefu dhidi ya Wazanzibari 
na kutoheshimiwa haki za binadamu zikiwamo za kutoa maoni na 
kujikusanya. 
Mbatia, ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, alisema 
Rais anapaswa kutimiza wajibu wake kuhakikisha usalama wa raia kama 
anavyotakiwa kikatiba na kuhakikisha polisi wanawalinda wananchi na siyo
 kuwaonea. 
  
“Ukawa inasema wazi kuwa inaendelea
 kukusanya taarifa za vitendo vya ubakaji wa demokrasia na haki za 
binadamu ili kupata ushahidi wa kutosha wa kumfikisha Dk Magufuli ICC 
akajibu makosa hayo,” alisema Mbatia. 
Katika mkutano huo uliohudhuriwa
 na wabunge 66 waliosaini tamko hilo, Mbatia alisema Ukawa inamtaka Mkuu
 wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu kuitoa amri ya kusitishwa kwa 
matendo hayo na achukue hatua dhidi ya askari wake ambao huwatesa raia 
ili kurudisha imani kwa wananchi. 
Alisema wananchi wa Pemba na Unguja 
waendelee kuikataa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa amani na pia 
wadumishe utaratibu wa kuheshimu sheria na kujizuia kufanya vitendo vya 
kukinzana na sheria. 
Lakini alipotakiwa kuzungumzia tamko hilo, Naibu 
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alitupa lawama zote kwa 
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad. 
Alisema kuwa ndiye adui 
mkubwa wa Ukawa baada ya kususia uchaguzi wa marudio na kuhamasisha 
wananchi wasiitambue Serikali na sasa wafuasi hao wanatekeleza maagizo 
hayo kwa kukata mazao na kuleta fujo kwa wananchi wenzao. 
“Kazi ya dola 
ni kuhakikisha mtu havunji amani. Watu wanaofanya vitendo hivyo 
washughulikiwe ipasavyo na vyombo vya dola,” alisema Vuai. 
Alisema 
hakuna sababu ya kumpeleka Rais Magufuli katika mahakama ya ICC kwa kuwa
 anafanya kazi nzuri ya kuongoza nchi na kwamba kauli zilizotolewa na 
Ukawa ni za kitoto. 
Alivisihi vyombo vya dola kuendelea kuimarisha 
usalama visiwani humo ili watu wenye nia mbaya wasizoroteshe amani 
kutokana na matakwa ya viongozi wao. 
Awali katika mkutano huo, Mbunge wa
 Malindi (CUF), Ally Saleh alisema wameamua kutoa tamko hilo kutokana na
 hali kuzidi kuzorota Pemba na kwamba ni lazima Serikali itekeleze 
wajibu wake kuzuia machafuko zaidi. 
Kuhusu mipango yao ya kumshtaki 
Rais, alisema kesi hiyo haina haraka kwa kuwa hata wajukuu zao wanaweza 
kuifungua kwa kuwa makosa ya jinai hayafi. 
“Baada ya kukusanya ushahidi wa kutosha na kujiridhisha kufanya hivyo, tutafanya. Tanzania siyo 
kisiwa ulimwengu mzima unaangalia nini kinaendelea Zanzibar, hivyo 
tusipowajibika, dunia itatuwajibisha,” alisema Saleh. 
Mbunge wa Chambani
 (CUF), Yusuph Salim Hussein alisema vyombo vya usalama vimekuwa 
vikiwatuhumu wafuasi wa CUF kufanya vurugu hizo lakini tangu zianze 
tuhuma hizo hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kushtakiwa kwa uharibifu 
mali au fujo. 
“Tangu mwaka 1992 hizo tuhuma kuwa sasa hakuna mtu 
aliyewahi kushtakiwa mahakamani na kutiwa hatiani. Ni wao (Serikali) 
ndiyo wanawaonea wananchi,” alisema. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya 
Nchi, Hamad Yusuph Masauni alisema ni jambo la kusikitisha kuona 
viongozi wanawalinda wahalifu badala ya kuhimiza amani na usalama. 
Masauni alisema baada ya uchaguzi wafuasi wetu ndiyo wanafanya fujo hadi
 Machi 20 hali ilikuwa shwari Pemba laki ni viongozi wa CUF ndiyo 
chanzo cha matukio ya uhalifu unaoendelea Pemba baada ya Maalim Seif 
kwenda visiwani huko na kuwataka wasiitambue Serikali. 
“Hivi kabla ya 
tamko la Maalim Seif vikosi vya ulinzi na usalama havikuwapo ili 
vikakate mikarafuu na kuchoma nyumba za watu? Askari wetu wamefunzwa 
vizuri, wamekula kiapo kulinda usalama wa raia wote bila kujali chama,” 
Alisema nchi haiwezi kuendeshwa kwa kuacha watu wavunje amani na 
kwamba vyombo vya usalama vitamshughulikia mtu yeyote atakayekiuka 
sheria bila kujali chama.