KATIKA
kutekeleza tamko la Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) la kufika
Dodoma kusaidiana na Jeshi la Polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Bavicha Dodoma wameanza maandalizi ya kupokea vijana
zaidi ya 2000.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Dodoma jana Malambaya Manyanya, Mwenyekiti
wa Bavicha Mkoa wa Dodoma alisema, kwa sasa viongozi wa mkoa wameanza
maadalizi ya kuwapokea wageni wao ambao wanatarajiwa kuanza kuwasili
tarehe 21 na 22 Julai mwaka huu.
Alisema,
maadalizi hayo ni ya kuwapokea vijana ambao watatoka katika mikoa yote
ya Tanzania kwa lengo la kutimiza tamko la Bavicha taifa la kushirikiana
na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kuzuia mikutano na vikao vya CCM.
Alisema,
kwa sasa mkoa tayari umeunda kikosi cha kufanya kazi ya maadalizi ya
ugeni huo ambapo kwa nia njema utafika mjini Dodoma kutekeleza kauli ya
Rais John Magufuli ya kuzuia vikao vyote na mikutano ya vyama vya siasa.
Alisema,
maadalizi hayo ya kuwapokea vijana hao ni pamoja na viongozi wa kitaifa
wa Bavicha kwa maana ya kutafuta mahali pa kulala na maandalizi ya
chakula.
“Wapo
watu ambao wanadhani Bavicha wana mpango wa kufanya fujo, sisi tunataka
kurejesha Demokrasia nchini na kutekeleza kauli ya mkuu wa nchi.
“Tumekuwa
tukiona jinsi mikutano ya Chadema inavyozuiliwa, na sasa msimamo wa
Bavicha ni kuzuia mkutano ya CCM unaotarajiwa kufanyika Julai 23 kwa
lengo la kubadilishana uongozi kati ya mwenyekiti wa sasa wa CCM na rais
msitaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete na Rais John Magufuli.
“Tumeandaa
vijana takribani 2000 kutoka mikoa yote nchini watakaokuja Dodoma
kusaidiana na Jeshi la Polisi kutawanya mkutano usio halali wa CCM.
“Kwa
sababau mkuu wa nchi ametoa tamko la kuzuia mikutano yote ya siasa
ikiwa ni pamoja na vikao vya ndani na mikutano ya hadhara hadi 2020.” Alisema Malambaya.
Alisema,
Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya vyama vya siasa vya upinzani na
mahafali ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Chadema (CHASO) na kuwa,
sasa wanashirikiana na polisi kuhakikisha mikutano ya CCM haitafanyika.