Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko

Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman (katikati), akipewa maelezo na
Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugeta (kulia) wakati alipotembelea
banda la mahakama hiyo kwenye Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya
Dar es Salaam yanayoendelea katika viwanja vya maonesho hayo, Barabara
ya Kilwa, Dar es Salaam, jana. Alifuatana na Jaji Kiongozi, Ferdinand
Wambali (kushoto), Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles
Mwijage (wa pili kulia) na viongozi wengine. (Picha na Yusuf Badi).
JAJI Mkuu, Mohammed Chande Othman, amesema Mahakama Maalumu ya
Uhujumu Uchumi na Ufisadi itaamua kesi kwa muda usiozidi miezi tisa na
kwamba itaanza na majaji 14.
Aidha, wameandaa kozi maalumu kwa majaji 14 watakaofanya kazi katika
mahakama hiyo itakayoanza Julai 11 hadi 15, mwaka huu, kwenye Chuo cha
Mahakama Lushoto mkoani Tanga, ili kupeana mwongozo juu ya uendeshaji wa
mahakama hiyo.
Jaji Mkuu alisema, kesi zitakazoendeshwa katika mahakama hiyo ni zile
ambazo upelelezi wake umekamilika ili uamuzi utolewe mapema. Kwa mujibu
wa Jaji Mkuu, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupambana na
uhalifu huo.
Aliyasema hayo jana wakati alipotembelea Maonesho ya 40 ya Kimataifa
ya Biashara ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu
Nyerere vilivyopo katika Barabara ya Kilwa, ambayo alisema yamezidi kuwa
bora kuliko miaka mingine. Alisema baada ya sheria hiyo ya uhujumu
uchumi kupitishwa na Bunge, imekuwa na marekebisho mengi na kuboreshwa
kwa kiasi kikubwa.
Jaji Mkuu alisema pia, hatua inayofuata ni Rais kutoa idhini ya
sheria hiyo na baadaye kupitishwa kwa kutangazwa katika Gazeti la
Serikali ili ianze kutumika.
Alieleza kuwa baada ya kutangazwa katika Gazeti hilo la Serikali,
Jaji anatakiwa kutunga kanuni mbalimbali, mojawapo ikiwa ya kulinda
mashahidi kutokana na kuwa sheria hiyo inahusu makosa makubwa na hatari
ya ugaidi, rushwa na uhujumu uchumi.
“Tuko mbioni kutunga kanuni hizo na kuhakikisha mashahidi wanalindwa.
Jengo la mahakama hii litakuwa katika Chuo cha Sheria karibu na Mlimani
City na tayari tumepeleka wasajili watendaji,” alisema.
Mwishoni mwa wiki, Jaji Mkuu huyo alisema kuwa majengo ya mahakama
hiyo yatakabidhiwa leo. Kutokana na maelezo yake, Mahakama iko tayari
kuendesha divisheni hiyo, baada ya kukabidhiwa majengo hayo.
Alisema wataanza kutoa semina kwa majaji na watumishi wengine wa
mahakama hiyo juu ya namna divisheni hiyo itakavyoendesha shughuli zake.
Aidha, aliweka wazi kuwa hadi sasa hakuna kesi hata moja
iliyokwishatambuliwa kwamba itashughulikiwa na mahakama hiyo.