Taarifa kwa vyombo vya habari!
Ndugu waandishi wa habari, Awali ya yote naomba nianze Kwa kumshukuru
Mungu Kwa kutujalia afya na uzima hata tukaweza kukutana hapa asubuhi ya
leo tukiwa salama. Pia tunamshukuru Mungu kwaajili ya ndugu zetu
waisilam kwa kufanikiwa kutimiza nguzo yao muhimu ya kiimani ya mfungo,
Hivyo tunawatakia sikukuu njema ya EID EL FITRI.
PILI, Naomba kwa moyo mkunjufu na wa dhati kabisa, kutumia fursa hii ya
kipekee kuwashukuruni ninyi waandishi wa habari kwa kukubali wito wetu
na kuja kutusikiliza. Ni matumaini yetu kuwa mtatusikiliza kwa makini na
kwa uhakika ili kuhakikisha ujumbe wetu unaifikia hadhira kubwa si tu
ya wana-Iringa bali watanzania wote na dunia kwa ujumla.
Aidha, Baraza la vijana la Chadema mkoa wa Iringa chini ya uongozi wa
BAVICHA mkoa iringa na viongozi wote wa baraza kwa ngazi zote za
wilaya, majimbo, kata, matawi na misingi tumekubaliana na kuunga mkono
kwa asilimia mia moja tamko la baraza la vijana Taifa lililotolewa na
makamu mwkt ndugu Patrick Sosopi la Tarehe 02/07/2016 la kukutana Dodoma
Tarehe 23/07/2016 ili kulisaidia jeshi la polisi kuwataka wenzetu CCM
kutii sheria bila shuruti.
Na kwa mantiki hiyo tunatangaza rasmi kuanzia leo tarehe 06-15/07/2016
zoezi la kuandikisha vijana kwa ngazi zote za uongozi litafanyika mkoa
wa Iringa na kwakuwa vijana wengi wamekuwa wakitupigia simu kuonyesha
utayari wao basi sasa tunawaalika rasmi kujiandikisha.
Ndugu, Wanahabari mtakumbuka mwkt wa kamati ya siasa ya CCM Iringa mjini
ndugu Kiponza aliwaita na kuzungumza nanyi, pamoja na mambo mengine
alieleza kile alichoita kuwa ndoto za bavicha kuzuia mkutano wa CCM
haziwezekani.sisi tunawaambia wenzetu waache kuweweseka na wasubiri
tarehe 23 ili wajue jinsi nguvu ya umma inavyoweza kusimamia amri ya
jeshi la police pamoja rais wao ya kuzuia shughuli za kisiasa mpaka 2020
. Pia watambue kuwa kupingana na bavicha ni sawa na kupingana na agizo
la mh. Rais tena aliyetokana na chama Chao, jambo ambalo si heshima kwa
kiongozi wetu wa nchi. Pia niwakumbushe ccm sisi bavicha mkoa wa Iringa
hatuendi Dodoma kufanya vurugu na uchochezi kama wanavyosema wao bali
tunaenda kuwasaidia police kuzuia mkusanyiko harama wa ccm
Ndugu Wanahabari, Naomba ieleweke kuwa ninyi wenyewe ni mashahidi wa
Tamko lilitolewa na mkuu wetu wa nchi ambalo lilikwenda sambamba na
tamko la jeshi la polisi kuvitaka vyama vyote vya siasa na wanasiasa
wasijihusishe na shughuli za kisiasa mpaka mwaka 2020 ili kuwapa fursa
viongozi waliochaguliwa kutekeleza ilani na ahadi zao kwa wananchi. Sasa
sisi tunajiuliza kwanini CCM wanataka kukaidi agizo hili wakati vyama
vingine vimekubali na kutii? Havana, ni lazima twende Dodoma tukawaambie
CCM wajifunze kutii maagizo ya vyombo vya dola na viongozi wa nchi.
KWANINI TUNAKWENDA DODOMA?
Ndugu Wanahabari tunakwenda Dodoma kwakuwa,
01. Mpaka sasa si rais wala jeshi la polisi aliyetengua kauai au tamko
la kuzuia shughuli za kisiasa kwa maana ya vikao vya ndani, makongamano,
mkutano ya hadhara au maandamano n.k
02. Haki ya kufanya shughuli za kisiasa haiwezi kuwa ya chama kimoja
kwenye nchi yenye mfumo wa vyama vingi tena unaotambulika kikatiba kama
Tanzania.
03.kwa mujibu wa katiba yetu ni wajibu wa kila raia kuhakikisha anatii
sheria za nchi, Hivyo sisi kama raia wema na tunaowapenda wenzetu
hatutaki wapigwe na kuumizwa na virungu vya polisi, tunakwenda
kuwasaidia na kuwakumbusha umuhimu wa kutii sheria bila shuruti (
Coercion without appliances)
04. Mkutano mkuu wa CCM huwakutanisha watu wengi sana na Hivyo jeshi la
polisi ambao kwa nchi nzima hawazidi 50,000 pekee yao hawataweza
kuwazuia. Tumejitolea hasa kwa kuzingatia ile dhana ya ulinzi shirikishi
ili wasipate kazi kubwa sana ya kufanya siku hiyo ya tarehe 23.
05.Tunakwenda Dodoma kusaidia utekelezaji wa kipaumbele muhimu sana
kwetu kama Chadema na ambacho kimekuwa hakitekelezwi kikamilifu na
kuleta matatizo mengi ambacho ni haki na usawa mbele ya sheria ( Law and
order before the law).
Ndugu wanahabari tangu kutolewa kwa tamko la viongozi wetu wa baraza
ngazi ya Taifa kumekuwepo na upotoshaji mkubwa eti bavicha wanakwenda
Dodoma kufanya fujo. Fujo! Kwanini tufanye Fujo? Tunasisitiza tunakwenda
Dodoma kama raia wema na lengo kuu ni kulisaidia jeshi la polisi ili
wasitumie nguvu kubwa kuwazuia CCM.Hivyo basi tunatoa wito kwa IGP Mangu
na RPC wa mkoa wa Dodoma kutupokea na kutupongeza kwa uzalendo wetu.
Mwisho ndugu wanahabari, nimalizie kwa kumnukuu aliyekuwa rais wa Kwanza
mweusi na baba wa Taifa la Afrika kusini Nelson Mandela aliwahi kusema "
mahali popote hakuna njia rahisi ya ukombozi na wengi wetu itabidi
tupitie, tena na tena kwenye bonde la uvuli wa Martin kabla ya kufikia
kilele cha mafanikio". Sisi vijana wa bavicha mkoa wa Iringa tuko tayari
kwa gharama kwenda Dodoma ili kusaidia kulinda sharia na katiba yetu
isifinyangle finyangwe na chama cha mapinduzi kwa kuamua kwa makusudi
kukiuka na kupuuza agizo la rais wetu na Jeshi la polisi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Imesomwa kwenu
Na, Jackson mnyawami
Katibu Bavicha Mkoa Iringa
Simu: 0762725088
0716884988
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezitoza faini ya
jumla ya Sh milioni 649 kampuni sita za simu nchini kwa kosa la kukiuka
masharti ya usajili na matumizi ya laini za simu.
Aidha, TCRA imetoa siku saba kwa kampuni za simu kuzima laini zote
zilizokiuka masharti ya usajili zilizoko sokoni ambazo zimewashwa na
kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wake kwa mamlaka hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James
Kilaba alisema hatua hiyo imetokana na mamlaka hiyo kufanya ukaguzi
katika mifumo ya usajili wa laini za simu na kugundua baadhi ya namba
kutolewa bila mteja kujisajili, kusajiliwa kwa majina, vitambulisho na
nyaraka za watu wengine.
“Pia TCRA imebaini baadhi ya kampuni kutofunga namba hadi usajili
ukamilike na kusajiliwa usajili wa awali ikiwa ni kinyume na Kanuni ya
33 ya Kanuni za Leseni za mwaka 2011 zilizotolewa chini ya Sheria ya
Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010,” alisema Kilaba.
Kampuni zilizopata adhabu hiyo ni Airtel Tanzania Limited, Benson
Informatics Limited, MIC Tanzania Limited, Viettel Tanzania Limited,
Vodacom Tanzania Limited na Zanzibar Telecom Limited.
Akifafanua adhabu hizo kwa kila kampuni, Kilaba alisema Airtel imetozwa faini ya Sh milioni 182.7.
Akichanganua faini hiyo ya Airtel, alisema Sh milioni 74 ni kwa
kuruhusu kuuzwa kwa laini 148 bila kutumia kitambulisho halisi cha
mnunuzi, Sh milioni 33.5 kwa kuruhusu laini 67 ziuzwe bila kujaza fomu,
Sh milioni 32.5 kwa kuruhusu laini 65 ziwashwe kabla ya kuuzwa na Sh
milioni 42.5 kwa kuruhusu laini 85 zifanyiwe usajili wa awali na
kutumika kwenye mtandao wake.
Alisema kwa upande wa Benson Informatics Limited imetozwa faini ya Sh
milioni 17. Sh milioni saba kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 14 bila
kitambulisho halisi, Sh milioni saba kwa kuruhusu laini 14 ziuzwe bila
kujaza fomu na Sh milioni tatu kwa kuruhusu laini sita ziwashwe kabla ya
kuuzwa.
Kilaba alisema kwa Kampuni ya MIC Tazania Limited, imetakiwa kulipa
faini ya Sh milioni 189 ikiwa ni Sh milioni 93.5 kwa kuruhusu kuuzwa kwa
laini 187 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi, Sh milioni 43.5
kwa kuruhusu laini 87 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili, Sh milioni 41
kwa kuruhusu laini 82 ziwashwe kabla ya kuuzwa na Sh milioni 11 kwa
kuruhusu laini 22 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao
wake.
Alisema Viettel Tanzania Limited wametozwa faini ya Sh milioni 107
ikiwa ni Sh milioni 36.5 kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 73 bila kutumia
kitambulisho halisi cha ununuzi, Sh milioni 36 imeruhusu laini 72 ziuzwe
bila kujaza fomu ya usajili na Sh milioni 34.5 kwa kuachia laini 69
ziwashwe kabla ya kuuzwa.
Alisema Vodacom Tanzania Limited imetozwa faini ya Sh milioni 96.5
ikihusisha Sh milioni 49 kwa kuacha laini 98 zisajiliwe bila kutumia
kitambulisho halisi cha mnunuzi, Sh milioni 24 kwa kuruhusu laini 38
ziwashwe kabla ya kuuzwa na Sh milioni 4.5 kwa kuruhusu laini tisa
zifanyiwe usajili wa awali kwa kutumika kwenye mtandao wake.
Alisema kwa upande wa Zanzibar Telecom Limited imetakiwa kulipa faini
ya Sh milioni 57 ikiwa ni Sh milioni 36.5 kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini
73 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi, Sh milioni 11.5 kwa
kuruhusu laini 23 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili na Sh milioni saba
kwa kuruhusu laini 14 ziwashwe kabla ya kuuzwa na Sh milioni mbili kwa
kuruhusu laini nne zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao
wake.
“Kabla ya kutolewa hukumu hii, tuliziita kampuni za simu
zilizogundulika kutenda makosa hayo na kutakiwa kutoa utetezi wao kuhusu
ukiukwaji wa masharti ya usajili wa namba za simu. “Ikumbukwe kuwa
Aprili 2013, TCRA na kampuni walikubaliana kuondoa kasoro zilizojitokeza
katika usajili wa namba za simu kwa kutowezesha laini kutumika kabla ya
usajili kukamilika na taarifa za mteja kuhakikiwa na kutofanya kile
kinachoitwa usajili wa awali,” alisema.
Sheria ya EPOCA ya 2010 inataka kampuni za simu kusajili laini ili
kumlinda mtumiaji kutokana na matumizi mabaya ya huduma za mawasiliano,
kuwezesha kuwatambua watumiaji wa huduma za ziada za simu na kuimarisha
usalama wa taifa.
Pia kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano kuwafahamu wateja wao na
kuwa na taarifa za matumizi ya simu za mkononi kwa ajili ya mipango ya
maendeleo.
Akizungumzia ukomo wa matumizi ya simu bandia na uanzishwaji wa
rajisi kuu ya namba tambulishi, Kilaba alisema mpaka sasa namba
tambulishi ambazo hazikidhi viwango 1,713,337 na zilizonakiliwa 117,389
zimezimwa.
WAKUU wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
nchini wameagizwa kujiandaa kuwapokea vizuri wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha tano na kuwaandalia chakula wanafunzi wa bweni
kabla shule hazijafunguliwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, George Simbachawene alisema hayo jana mjini hapa
wakati akizungumzia maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano
mwaka 2016 kwenye shule mbalimbali walizopangiwa.
Wanafunzi hao wanatakiwa kuripoti shule walizopangiwa Julai 11, mwaka
huu. Alisema ni vizuri kwa watendaji hao kujipanga ili wanafunzi
wanapofika kwenye shule walizopangiwa wakute mazingira mazuri. Alisema
wanafunzi hao wamepangwa katika shule 329 zote za kidato cha tano na
sita nchini, na kati ya hizo 50 ni mpya.
Simbachawene alisema wanafunzi wa awamu ya kwanza waliopangwa
kujiunga na kidato cha tano ni 65,720 kati ya 90,248 na awamu ya pili
inasubiri nafasi zitakazojitokeza kutokana na wanafunzi watakaoacha
kuripoti kwa kupelekwa na wazazi wao kwenye shule za binafsi.
Alisema chimbuko la kuanzisha shule mpya za kidato cha tano 50
imetokana na maombi ya mikoa kwenye maeneo yao ili kuendana na lengo la
serikali la kuongeza shule za kidato cha tano na sita hapa nchini.
Alisema wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa mamlaka za serikali
za mitaa wana wajibu wa kuzihudumia shule hizo kwa karibu, na pia
kuhakikisha miundombinu yote inakamilika ikiwemo mabweni, madarasa,
vyoo, maabara, samani, huduma za maji na umeme.
Wakati huo huo, Waziri Simbachawene amesema kuanzia sasa shule zote
za serikali zifungwe na kufunguliwa siku moja tofauti na sasa kila shule
imejiwekea utaratibu wake.
OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumioshi wa Umma na Utawala Bora
imejaza nafasi zilizokuwa wazi za Makatibu Tawala wa Wilaya (Ma-DAS)
katika wilaya mbalimbali nchini.
Kujazwa kwa nafasi hizo kumetokana na sababu mbalimbali ikiwemo
baadhi ya Ma-DAS kustaafu, kufariki pamoja na kupoteza sifa za kuendelea
kuwa makatibu tawala wa wilaya hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angellah Kairuki alisema, baadhi ya wilaya zimeachwa wazi ambapo uteuzi
wa Ma-DAS utafanyika baadaye kwa ajili ya kujaza nafasi hizo.
Kairuki alizitaja wilaya hizo na mikoa yake kwenye mabano kuwa ni
Newala (Lindi), Makete (Njombe) pamoja na Kisarawe iliyopo mkoa wa
Pwani.
“Makatibu ambao waliokuwepo wataendelea na kazi kama kawaida lakini
kwa wale wapya walioteuliwa wafike ofisi za Utumishi wakiwa na CV
(wasifu zao pamoja na nakala za vyeti vyao,” alisema Kairuki.
Ma-DAS walioteuliwa na Wilaya na Mikoa yao kwenye mabano ni David
Mwakiposa (Arusha), Amos Siyantemi (Monduli), Adam Mzee (Arumeru), Abas
Kayanda (Karatu), Lamuel Kileo (Ngorongoro) na Toba Nguvila (Longido,
Arusha).
Kwa mkoa wa Dar es Salaam walioteuliwa ni Edward Mpogoro (Ilala),
Omary Mhando (Kigamboni), Mtela Mwampamba (Ubungo), Hashimu Komba
(Temeke) na Gift Msuya (Kinondoni). Dodoma walioteuliwa ni Kasilda Mgeni
(Bahi), Athanasia Kabuyanja (Mpwapwa), Juliana Kilasara (Chamwino),
Audiphace Mushi (Kongwa), Winnie Kijazi (Kondoa), Jasinta Mboneko
(Dodoma) na Ally Chilukile (Chemba).
Geita walioteuliwa ni Thomas Dime (Geita), Paul Cheyo (Bukombe),
Eliasi Makory (Chato), Reuben Mwelezi (Nyang’wale) na Christopher Bahali
(Mbogwe). Iringa ni Allan Mwella (Mufindi), Joseph Chitika (Iringa) na
Yusuph Msawanga (Kilolo).
Katavi ni Epaphras Tenganamba (Mlele), Mahija Nyembo (Mpanda) na
Mwashitete Geogrey (Tanganyika). Kagera ni Gread Ndyamukama (Bukoba),
Joel Mwakabibi (Biharamulo), Josephat Tibaijuka (Ngara), Mwakasyege
Richard (Muleba), Godfrey Kasekenya (Misenyi), Weka Ng’olo (Karagwe) na
Haji Godigodi (Kyerwa).
Kigoma ni Muguha Muguha (Kasulu), Kwame Daftari (Kigoma), Ayubu
Sebabili (Kibondo), Zainab Mbunda (Kakonko), Upendo Marango (Uvinza) na
Peter Masindi (Buhigwe).
Kilimanjaro ni Heri James (Hai), Abubakari Asenga (Rombo), Mabenga
magonera (Same), Yusufu Kasuka (Mwanga), Leornad Maufi (Moshi) na
Nicodemus John (Siha).
Lindi ni Thomas Safari (Lindi), Lameck Lusesa (Liwale), Athanas
Hongoli (Kilwa), Husna Sekiboko (Nachingwea) na Twaha Mpembenwe
(Ruangwa). Manyara ni Ndaki Mhuli (Kiteto), Zuwena Omary (Simanjiro),
Mkumbo Barnabas (Hanang), Cade Mshamu (Babati) na Samuel Gunzar (Mbulu).
Mara ni (Justin Manko (Musoma), Masalu Kasasila (Bunda), John Mahinya
(Tarime), Cosmas Qamara (Serengeti), Mirumbe Daudi (Rorya) na Credo
Lugalila (Butiama). Mbeya ni Anold Mkwawa (Mbeya), Moses mashaka
(Rungwe), Ezekia Kilemile (Mbarali), Sostenes Mayoka (Chunya) na Godfrey
Kawacha (Kyela).
Morogoro ni Alfred Shayo (Morogoro), Michael Maganga (Mvomero),
Stanslaus Nyanga (kilosa), Linno Mwageni (Kilombero), Abraham Mwaikwila
(Ulanga/ Mahenge) na adam bibangamba (Gairo). Mtawara ni Teoford Ndomba
(Mtwara), Benaya Kapinga (Masasi), Azizi Fakili (Tandahimba) na Michael
Matomola (Nanyumbu).
Mwanza ni Kazeri Japhet (Misungwi), Solomon Ngiliule (Magu), Andrea
Ng’hwani (Kwimba), Allan Muhina (Sengerema), Yonas Alfred (Nyamagana),
Focus Majumbi (Ukerewe) na Tryphone Mkorokoti (Ilemela). Njombe ni
Joseph Chota (Njombe), Stephen Ulaya (Ludewa) na Edward Manga
(Wanging’ombe).
Pwani ni Erica Yegella (Bagamoyo), Sozi Ngate (Kibaha), Gilbert
Sandagila (Mafia), Severine Lalika (Mkuranga) na Maria Katemana
(Rufiji).
Rukwa ni Festo Chonya (Nkasi), Christina Nzera (Sumbawanga) na Juma Seph Kalambo.
Ruvuma ni Aden Nchimbi (Namtumbo), Gilbert Sinya (Mbinga), Ghaibu
Lingo (Tunduru), Pendo Daniel (Songea) na Richard Mbambe (Nyasa).
Simiyu ni Albert Tuihwa (Bariadi), Rutaremwa Rutangumirwa (Maswa),
Chele Ndaki (Meatu), Helman Tesha (Itilima) na Sebastian Masanja
(Busega). Shinyanga ni Timonth Ndaya (Kaham), Shadrack Kengese ()
Kishapu) na Boniface Chambi (Shinyanga).
Singida ni Pius Songoma (Iramba), Deusdedith Duncun (Manyoni), Wilson
Shimo (Singida), Flora Yongolo (Ikungi) na Omar Kipanga (Mkalama).
Songwe ni Johari Samizi (Songwe), Mary Marco (Ileje), Tusibetege Tengela (Mbozi) na Mathias Felix (Momba).
Tabora ni (Sweetbert Nkuba (Tabora), Moses Pesha (Uyui), Paschal
Byemelwa (Urambo), Godslove Kawiche (Igunga), Onesmo Kisoka (Nzega),
Renatus Mahimbali (Sikonge) na Jones Likuda (Kaliua).
Tanga ni Veronika Kinyemi (Lushoto), Mariagrace Kallega (Korogwe),
John Mahali (Handeni), Faiza Salim (Tanga), Desderia Haule (Muheza),
Ebene Mabuga (Pangani), Joseph Sura (Mkinga) na Philis Nyimbi (Kilindi).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), George Simbachawene amesema wanaendelea kukusanya takwimu za
madawati mikoa yote nchini ambazo zitabainisha mkoa wa kwanza hadi wa
mwisho katika kufanikisha kampeni hiyo na hatua zitakazochukuliwa kwa
walioshindwa.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati akikabidhiwa hundi ya Sh milioni
900 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati nchini iliyotolewa na Benki ya
NMB.
Alisema tatizo la uhaba wa madawati lilikuwepo tangu awamu zilizopita
za uongozi wa nchi, hata hivyo tatizo hilo liliongezeka mwaka huu
kutokana na serikali kuanza kutekeleza utoaji wa elimu ya msingi bila
malipo.
Aliongeza kuwa, utekelezaji huo ulihamasisha wazazi na jamii kwa
ujumla kuwaandikisha watoto wengi kuanza darasa la awali na darasa la
kwanza, hivyo idadi kubwa ya uandikishaji imeongeza upungufu wa madawati
uliokuwepo.
Waziri huyo alisema Januari mwaka huu, watoto waliotegemewa kuanza
darasa la kwanza walikuwa milioni moja, lakini walioandikishwa walifikia
milioni 1.3.
“Tunaendelea kukusanya takwimu za madawati na tutajua wa kwanza hadi
wa mwisho na hatua zitakazochukuliwa kwa walioshindwa,” alisema na
kuongeza kuwa pamoja na hayo, sasa wanaelekeza nguvu kwenye kukabiliana
na upungufu wa vyumba vya madarasa, kwani vilivyopo havitoshi.
Alisema katika shule za msingi kuna upungufu wa vyumba vya madarasa
127,799 sawa na asilimia 54 kati ya vyumba 236,092 vinavyohitajika huku
kwa upande wa sekondari kuna upungufu wa vyumba 10,636 (asilimia 23.7).
Aidha, Simbachawene ameishukuru NMB kwa kuitikia mwito wa Serikali ya
Rais, Dk John Magufuli kwa kuchangia Sh milioni 900 za kununulia
madawati. Naye Ofisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Waziri Barnabas
alisema sera yao ni kutoa asilimia moja ya mapato yao kwa ajili ya
shughuli za kijamii.
MBUNGE wa Mwibara, Kangi Lugola, anayekabiliwa na mashtaka ya kuomba
rushwa ya Sh milioni 30, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itoe
onyo kwa kitendo cha upande wa Jamhuri kuahirisha kesi mara kwa mara.
Licha ya Lugola, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa
Mvomero, Ahmad Saddiq (53) na wa Lupa, Victor Mwambalaswa (63).
Lugola alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba, baada ya
Wakili wa Serikali, Dennis Lekayo kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa
waendesha mashitaka katika kesi hiyo hawapo.
Awali, Wakili Lekayo alidai, kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuwasomea
washtakiwa maelezo ya awali lakini aliomba ipangiwe tarehe nyingine kwa
kuwa mawakili hawapo.
Lugola aliomba Mahakama ikemee tabia hiyo kwa kuwa ofisi ya waendesha
mashitaka ina watu wengi hivyo ingeweza kutoa wengine kwa ajili ya
kuwasomea maelezo ya awali. Aliendelea kudai kuwa, kitendo cha
kuahirisha kesi hiyo mara kwa mara, kinawanyima haki yao ya msingi ya
kufanya shughuli za kibunge.
“Kwa kuwa imekuwa kawaida washtakiwa wanapokuwa watoro, Mahakama
inawaita ili wathibitishe, kwa nini hawajafika na wakati mwingine
wanachukuliwa hatua hivyo naomba mahakama itoe onyo kwa upande wa
Jamhuri,” alidai Lugola.
Baada ya maelezo hayo Wakili Lekayo aliiomba Mahakama iwawie radhi na
kuahidi watafanya haraka kesi iendelee. Hakimu Simba alisema hoja ya
mshtakiwa ni ya msingi kwani kama mwendesha mashitaka aliondoka,
alitakiwa alete wengine. Aliwataka wasirudie kufanya hivyo.
Kesi imeahirishwa hadi Julai 12 mwaka huu kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Wabunge hao wanadaiwa wakiwa wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali
za Mitaa, waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni 30 kutoka
kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta kama
kishawishi cha kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashau