Alhamisi, 4 Agosti 2016
Jumatano, 3 Agosti 2016
Msigwa apewa kibali kufanya mkutano wa hadhara.......
Hatimaye Jeshi la Polisi
limetoa kibali cha kufanya mkutano wa hadhara kwa Mbunge wa Iringa
Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, lakini limeweka mlolongo wa masharti
ambayo atalazimika kuyatii kuepuka rabsha.
Wakati Jeshi la Polisi
likitoa masharti hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema
vyama vya upinzani vitaendelea kuendesha mikutano ya hadhara licha ya
kufungua kesi Mahakama Kuu ya kupinga zuio la shughuli hizo, huku
akisema amri ya kuzuia wanasiasa kufanya mikutano nje ya maeneo yao
imetolewa bila ya kusoma sheria.
Mkoani Iringa, Jeshi la Polisi lilitoa masharti hayo baada ya Msigwa, ambaye anaongoza Jimbo la Iringa
Mjini kwa kipindi cha pili mfululizo, kutaarifu kuwa atafanya mkutano wa
hadhara kuanzia Septemba Mosi, siku ambayo Chadema imepanga kuanza
operesheni ya nchi nzima inayoiita “ya kupinga udiktekta Tanzania”.
Katika barua aliyomwandikia Mchungaji Msigwa juzi, Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Iringa (OCD), Y. Z Mjengi amerejea barua ya mbunge huyo yenye
kumbukumbu namba MB/IR/M/05 ya Agosti Mosi mwaka huu, inayohusu mikutano
ya hadhara kuanzia Agosti 3 hadi 22, ikianza saa 8:00 mchana hadi 12:00
jioni.
Kupitia barua hiyo, ambayo Msigwa alithibitisha kuipokea, Jeshi
la Polisi limesema limeridhia kwa sababu lengo la mkutano wake ni
kuhamasisha maendeleo na kupokea kero za wananchi, kazi ambayo inatakiwa
kufanywa na mbunge wa eneo husika.
“Natarajia mkutano wako (Msigwa)
utakuwa wa amani na utulivu bila kumkashifu mtu wa chama kingine,”
anasema Mjengi katika barua hiyo.
“Mikutano yote hiyo kibali kimetolewa kwako kama mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini. Sitarajii
mtu mwingine kutoka nje ya Mkoa wa Iringa kuja kukusemea kuhusu
maendeleo ya jimbo lako au kuja kupokea kero za wananchi wako na
kuzijibia wakati hiyo ni kazi ya mwenye himaya ambaye ni wewe.
“Kashfa,
kejeli, matusi na maneno ya uchochezi kwa viongozi wa Serikali
vitahesabiwa ni uvunjifu wa amani na hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yako na zitapelekea kuzuiliwa kufanya mikutano yako
inayoendelea.”
Barua hiyo inaishia kwa maneno yaliyoandikwa kwa herufi
kubwa. “Kumbuka: Amani ya Tanzania italindwa na kila Mtanzania kwa hiyo
ni jukumu lako wewe Mhe. Mbunge kutekeleza jukumu la ulinzi wa amani.
Kwa pamoja tutaweza,” inasema barua hiyo.
Alipoulizwa kuhusu masharti
hayo, Mchungaji Msigwa alisema hayo ni ya kwanza lakini hakutaka
kuzungumza zaidi kwa maelezo kuwa alikuwa kwenye kikao.
Msimamo wa Lissu
Hata hiyo, Lissu alisema muda mfupi baada ya kesi yake kuahirishwa
jijini Dar es Salaam kuwa suala hilo halikubaliki kwa kuwa sheria
inawaruhusu kufanya mikutano popote.
“Mbona huniulizi kama Magufuli
yuko sahihi anaposema kila mmoja akafanye mikutano kwenye kajimbo kake?”
Lissu aliwauliza waandishi nje ya Mahakama ya Kisutu akionekana kutaka
kuzungumzia suala hilo baada ya kuulizwa swali tofauti.
“Sheria ya
Tanzan ia inasema chama kilichopata usajili wa kudumu kina haki ya
kufanya mikutano ya hadhara mahali popote,” alisema.
Alisema chama
chenye usajili kina haki kufanya mikutano na kwamba Rais Magufuli
alitangaza zuio hilo bila ya kusoma sheria.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya nchi hii na sheria zake zote, hana
mamlaka yoyote ya kusema lolote au kufanya lolote kuhusiana na mikutano
ya hadhara,” alisema.
“Mtu anayetambuliwa na sheria kuhusiana na
mikutano ni OCD peke yake.”
Lissu alisema kuweka mipaka hiyo kwa
wanasiasa kufanya shughuli zao kwenye maeneo waliyoshinda tu, itawanyima
haki viongozi ambao vyama vyao havikupata ushindi, akitoa mfano wa
Augustine Mrema, ambaye ni mwenyekiti wa TLP na John Cheyo (mwenyekiti
UDP), kufanya shughuli za siasa.
Lissu pia alizungumzia
uamuzi wao wa kutangaza mikutano ya hadhara nchi nzima wakati wakiwa
wamefungua kesi kutaka tafsiri ya Sheria ya Vyama vya Siasa.
“Kesi
mahakamani, maisha hayasimami. Hatuachi kuwa chama cha siasa, hatuachi
kuwa na haki zetu kama vyama vya siasa. Haki zetu zinabaki palepale,”
alisema Lissu alipoulizwa sababu za Chadema kutangaza mikutano ya
hadhara kabla ya uamuzi wa kesi yao haujatoka.
“Na kwa mujibu wa sheria,
na sheria yenyewe ni ya Vyama vya Siasa, ni kwamba vyama vya siasa vina
haki ya kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kwa mujibu wa sheria.
“Kwa hiyo tutafanya maandamano na mikutano nchi nzima, si kwa sababu
tumefungua kesi tu, bali kwa sababu
tuna haki kwa mujibnui wa sheria za Tanzania kufanya maandamano na
mikutano, kama alivyo na haki mwenyekiti mpya wa CCM bwana Magufuli,
kama alivyo na haki bwana ole Sendeka (msemaji wa CCM), kama alivyo na
haki kiongozi wa chama chochote kilichosajiliwa.”
Alisema hawawezi
kuacha kutumia haki yao ambayo ipo kisheria kwa sababu tu Mahakama
haijatoa uamuzi.
Kesi ya uchochezi
Jana, katika kesi nayomkabili Lissu, upande wa mashtaka umeieleza Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshtakiwa huyo alikiri mbele ya polisi kutenda
kosa la kutoa maneno ya uchochezi.
Wakili wa Serikali, Bernard Kongola alisema hayo wakati akimsomea Lissu maelezo ya awali ya kesi ya
kutoa maneno ya uchochezi.
Hata hivyo, Lissu aliyakana maelezo hayo na
badala yake katika maelezo hayo alikubali utambulisho wake tu, yaani
jina lake na wadhifa wake kuwa ni mbunge.
Baada ya kusomewa maelezo hayo
na kukana mashtaka hayo, Hakimu Dk Yohana Yongolo anayesikiliza kesi
hiyo aliiahirisha hadi Agosti 24 wakati upande wa mashtaka utakapoanza
kutoa ushahidi.
Akimsomea maelezo ya awali, Wakili wa Serikali
aliieleza mahakama kuwa Lissu alitenda kosa la kumuita Rais Magufuli
kuwa ni dikteta Juni 28, 2016 katika eneo la mahakama hiyo, alikokuwa
amekwenda kwenye kesi nyingine ya jinai.
Wakili Kongola alinukuu maneno hayo kuwa alisema: “Mamlaka ya Serikali mbovu ya kidikteta uchwara
yanapaswa kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote. Huyu dikteta
uchwara lazima apingwe kila sehemu kama uongozi utafanywa na utawala wa
kijinga, nchi itaingia kwenye giza nene.”
Wakili Kongola alisema kuwa
Juni 29, 2016, mshtakiwa huyo alikamatakwa akiwa nyumbani kwake Tegeta
Kibaoni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam na kwamba alipohojiwa alikiri
kutamka maneno hayo.
Jana nje ya mahakama, Lissu aliwashukuru wafuasi
waliofurika kushuhudia kesi hiyo akisema ni ishara nzuri na kwamba
watamaliza kesi zote zinazowakabili kwa kufurika kwa wingi mahakamani na
hivyo kuwa kero.
Mbunge Nassari na Madiwani 28 wa CHADEMA wafutiwa kesi
SERIKALI kupitia Ofisi ya Mwendesha Mashitaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imetakiwa kufanya utafiti wa kina katika mashauri inayoyafungua mahakamani.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Arusha
jana na Wakili wa Kujitegemea, Charles Abraham, aliyekuwa
akiwawakilisha watuhumiwa 29 katika kesi iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi
ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) na madiwani 28
wa chama hicho wakituhumiwa kuvunja uzio wa thamani ya Sh milioni saba.
Akizungumza
nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya Hakimu
Mkazi, Desder Kamugisha kuifuta kesi hiyo, Wakili Abraham alisema uamuzi
huo ulitolewa baada ya Serikali kukosa ushahidi.
“Ni
rai yangu kwa Serikali kwamba iwe inafanya utafiti katika mashauri
inayoletewa kabla haijapeleka kesi mahakamani. Hii itasaidia kuondoa
gharama zisizo za lazima na usumbufu kwa watu na jamii wakiwamo
viongozi,” alisema Wakili Abraham.
Awali,
mahakamani hapo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Blandina Msawa,
uliwasilisha ombi la kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo, hivyo
ulimuomba hakimu huyo kuiondoa hoja ambayo ilikubaliwa na upande wa
utetezi.
Akitoa
uamuzi wa kuifuta kesi hiyo, Hakimu Kamugisha alisema kwa vile upande
wa mashitaka umeamua kuiondoa kesi hiyo, mahakama haitakuwa na
kipingamizi.
Mbunge Nassari akizungumzia kufutwa kwa kesi hiyo, alisema ilifunguliwa kisiasa badala ya kuangalia maslahi ya mali za Serikali.
Naye
Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Yona Nnko ambaye mwaka jana alihamia
Chadema, alimpongeza Nassari na madiwani kwa kufanikiwa kupigania haki
ya wananchi wa Arumeru Mashariki.
Nassari na madiwani hao walifunguliwa kesi hiyo na Jamhuri wakidaiwa kuharibu mali ya Itandumi Makere katika eneo la Usa River.
Jumanne, 2 Agosti 2016
Jumatatu, 1 Agosti 2016
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)