ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 20 Agosti 2016

Watakaochakachua Mitihani Kidato cha Nne Kukiona

 
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema haafiki uchakachuaji kwenye mitihani na kusema wakuu wa shule watakaobainika kufanya udanganyifu huo hawatapona.

Profesa Ndalichako alisema hayo kwenye kikao kati ya Ofisi ya Rais, Tamisemi, Maofisa Elimu wa Mikoa, Wakuu wa shule kongwe na wakuu wa shule zilizoungua moto.

Alisema ikiwa imebaki miezi mitatu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kufanya mitihani aliwataka wakuu wa shule kujipanga kupata ufaulu mzuri.

“Bado siafiki suala la uchakachuaji kwenye mitihani wanafunzi waachwe wafanye mitihani wenyewe na si kupitia kamati za ufundi, sasa Wizara inaangalia ubora wa elimu na wakuu wa shule watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua,” alisema.

Alisema pia matokeo ya mitihani ya shule za sekondari ya mwaka jana yalimhuzunisha sana lakini anaamini wakuu wa shule watajipanga kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri zaidi.

“Nilipokuwa Baraza la Mitihani nilisema nisiulizwe kutokana na matokeo kuwa mabaya lakini sasa niko Wizara ya Elimu siwezi kukwepa hilo tena,” alisema.

Waziri Ndalichako alisema watabadilisha mfumo wa namna maofisa elimu watakavyofanya kazi zao ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule za serikali na kuwataka wakuu wa shule na maofisa elimu kila mmoja ajipange.

Aidha alisema mkuu wa shule ni mdhibiti wa taaluma katika eneo lake na hatakiwi kumuogopa mtu anayemuongoza. Waziri huyo pia alisema katika mtihani wa kidato cha sita uliopita shule 100 za kwanza shule za serikali zilikuwa tatu na kuwa nafasi ya 53 ndio ilishikwa na Ilboru ya Arusha.

“Mpaka namba 100 shule za serikali ni tatu tu, sio kitu cha kawaida hapa ndio mahali pa kuzungumza kama serikali tunashindwa kuonesha mfano tuachie sekta binafsi,” alisema
 

Mfanyabiashara Moshi Ajimwagia Petroli na Kujipiga Kiberiti

lnawezekana likawa tukio baya lililoacha gumzo na simanzi baada ya mfanyabiashara wa mjini Moshi, Romani Shirima (74), kujiua kwa kujilipua kwa petroli nje ya nyumba yake.

Habari kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo zinasema mfanyabiashara huyo alijifunika kwa blanketi, kisha kujimwagia petroli na kutumia kibiriti kuwasha moto ambao ulimlipua na kusababisha kifo chake. 

Ingawa hakuna taarifa rasmi ya nini kiini cha mfanyabiashara huyo kuchukua uamuzi huo mgumu ulioacha maswali mengi, lakini baadhi walidai ni msongo wa mawazo uliotokana na madeni. 
Hili ni tukio la pili kwa mfanyabiashara mkazi wa mkoa wa Kilimanjaro, kwani miaka kadhaa iliyopita, mfanyabiashara anayemiliki hoteli eneo la Marangu alijilipua kwa petroli akiwa katika gari lake. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema  jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi, saa 11.25 asubuhi maeneo ya Mjohotoni. 
Alisema, mfanyabiashara huyo ni mmiliki wa shule ya sekondari ya Merinyo iliyopo mjini Moshi, na kusema kuwa aliamka asubuhi nyumbani kwake na kujimwagia mafuta hayo na kisha kujilipua na kiberiti. 
Kamanda Mutafungwa alisema chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika ingawa kuna maneno yanayoongelewa na watu, lakini hawawezi kuyachukua moja kwa moja na kwamba jeshi hilo linachunguza ili kubaini chanzo chake.
Taarifa za tukio hilo la aina yake zimekuwa gumzo katika maeneo mbalimbali ya mji wa Moshi na vitongoji vyake, hasa njia aliyoitumia kukatisha uhai wake.