Alhamisi, 12 Januari 2017
Jumatano, 11 Januari 2017
Rais Obama Amwaga Chozi Wakati Akiwaaga Wamarekani
Rais
wa Marekani, Barack Obama amewaaga Wamarekani na ulimwengu mzima kwa
ujumla ikiwa ni mara ya mwisho akiwa kama rais, katika hotuba iliyojaa
hisia kubwa aliyoitoa mjini Chicago na kuwataka Wamarekani kuunganisha
nguvu katika kuleta mabadiliko.
Rais huyo ametokwa na machozi wakati akimshukuru mke wake Michelle Obama kwa namna alivyotoa mchango mkubwa katika utawala wake.
Akihitimisha
utawala wake katika Ikulu ya Marekani, Obama amerejea katika mji ambao
sasa ni nyumbani kwake wa Chicago ambako kampeni yake ya "ndio tunaweza"
ilianzia hapo na leo akisema "ndio tumeweza".
Akiorodhesha
mafanikio ya utawala wake kuanzia mkataba wa nyukilia na Iran hadi
huduma ya bima ya afya, sehemu kubwa ya hotuba yake iliegemea katika
kuwatia moyo wafuasi wake waloshtushwa na ushindi wa Donald Trump pamoja
na kutathmini mafanikio aliyoyapata katika uongozi wake na mtazamo wake
kuhusu wapi Marekani inaelekea .
Obama
amewataka Wamarekani kuamka, kupigania demokrasia lakini akaonya kuwa
ubaguzi wa rangi na kukosekana kwa usawa bado ni kitisho kwa
demokrasia.
"Sisi sote bila ya kujali vyama, ni lazima turudi katika ujenzi wa taasisi ya demokrasia", amesema Obama.
"Hivyo
sisi kama wananchi, lazima tuwe macho dhidi ya uchokozi wa nje, ni
lazima tuilinde misingi yetu inayodhoofika inayotutambulisha sisi ni
akina nani. Ndio maana katika kipindi cha miaka nane iliyopita nimefanya
kazi ya kuweka mapambano dhidi ya ugaidi katika misingi ya kisheria.
"Ndio
maana tumemaliza mateso, kufanya kazi kulifunga gereza la Guantanamo,
na mageuzi ya sheria zetu zinazosimamia ufuatiliaji wa kulinda faragha
na uhuru wa raia. Na ndio maana mimi nimekataa ubaguzi dhidi ya Waislamu
Wamarekani", amenukuliwa rais huyo.
Miongoni
mwa mafanikio mengine anayojisifia Obama ni pamoja na kuimarishwa kwa
uchumi, kuhalilisha ndoa za jinisia moja, kufunguliwa kwa mahusiano ya
kidiplomasia na Cuba na maenedeleo mengine.
Mke
wake Michele Obama na makamu wa rais Joe Biden na mke wake Jill ambao
rais amewaelezea kama "familia" wamehudhuria hafla hiyo.
Obama
akifuta machozi machoni mwake amemshukuru mke wake Michelle akimuita ni
rafiki yake mkubwa, mtoto wake Malia aliyekuwa akibubujikwa na machozi
pamoja na Sasha ambaye hakuwepo.
Akielezea mchango wa mke wake, Obama anasema, "Michelle
Lavaughn Robinson, msichana kutoka upande wa kusini, kwa miaka zaidi ya
20 iliyopita, umekuwa sio tu mke wangu na mama wa watoto wangu lakini
rafiki yangu mkubwa.
"Ulichukua
jukumu ambalo hukuuliza na ukalifanya kuwa lako kwa neema , ujasiri,
mipango na ucheshi mzuri. Uliifanya Ikulu kuwa sehemu ya kila mtu."
Anasema Marekani imekua bora na yenye nguvu duniani tangu alipokula kiapo kuiongoza nchi hiyo miaka nane iliyopita.
Donald
Trump atakayeapishwa Januari 20 anatarajiwa kuondoa baadhi ya
yaliyofikiwa na karibu kiasi ya watu elfu 18 waliohudhuria hafla hiyo
mjini Chicago walimshangilia rais huyo wakisema "miaka minne zaidi" na
Obama akasema hawezi kufanya hivyo.
Obama
katika hotuba yake ya mwisho ameepuka kumkosoa Trump moja kwa moja na
kulaani mgawanyiko ambao umezikumba siasa za taifa hilo.
Imeandikwa na Mtandao wa DW
Breaking News:Mbunge wa Kilombero Morogoro (CHADEMA ) ahukumiwa miezi 6 jela Bila Faini
Mbunge
wa Jimbo la Kilombero, Peter Lijualikali na Dereva wake, John Kibasa
wamehukumiwa kwenda jela miezi sita bila faini kwa kosa la kufanya
vurugu kipindi cha uchaguzi mwaka 2015.
Hukumu
hiyo imetolewa leo katika Mahakama ya Wilaya ya Kilombero na sasa
amepelekwa gerezani huku taratibu za kukata rufaa zikiendelea.
Hukumu
hiyo ilisomwa chemba lakini wabunge wawili wa Chadema Joseph Haule
(Mikumi) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) waliingia na kusikiliza hukumu.
Jumanne, 10 Januari 2017
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)