WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimechukua maamuzi magumu katika historia ya chama hicho tangu kizaliwe kwa kuwafukuza viongozi wa juu wengi kwa wakati mmoja baada ya kubainika kukiuka misingi ya Katiba ya chama hicho, gazeti hili limebaini sababu zaidi za kufukuzwa kwa viongozi hao.
CCM jana ilitangaza uamuzi mzito wa kuwafukuza uanachama, kuwavua uongozi na kuwapa onyo kali vigogo 22 ambao wamechangia kukihujumu na kukifanya chama hicho kinuke mbele ya jamii.
Kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), CCM imeamua kuchukua hatua hiyo ya kuadhibu viongozi wake baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Kamati Kuu (CC) iliyokutana jana asubuhi ambayo nayo ilipokea ripoti kutoka kwenye Kamati Ndogo ya Maadili naNidhamu ya chama iliyoketi mjini hapa juzi.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamprey Polepope ndiye aliyeutangazia umma uamuzi huo na kusema adhabu hizo zimeanza jana. Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo, chanzo cha kuaminika kutoka Dodoma (jina kapuni) kililidokeza gazeti hili kuwa hatua hiyo imetokana na usaliti mkubwa uliofanywa na viongozi hao wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.