ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 23 Machi 2017

Waziri Nape apokea Ripoti ya kamati ya uchunguzi wa tukio la RC Makonda Kuvamia Kituo cha Clouds Media

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam amedaiwa kuwatishia kuwafunga jela miezi 6 au kuwapa tuhuma za dawa za kulevya bila kupitia mahakamani wafanyakazi wa kituo cha utangazaji cha Clouds kwa kukataa kurusha habari aliyoitaka.

Hayo yamebainika katika ripoti ya uchunguzi wa tukio la mkuu huyo wa mkoa kuvamia katika kituo cha utangazaji cha Clouds akiwa na askari wenye silaha, ripoti ambayo pia imependekeza mamlaka husika kumchukulia hatua za kinidhamu.

Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mbele ya wanahabari katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Kamati ya uchunguzi Deodatusi Balile amesema kamati hiyo haikuweza kumpata Paul Makonda kwa ajili ya mahojiano.

Akitaja mambo yaliyobainika katika sakata hilo, Balile amesema kamati hiyo iliyohoji watu mbalimbali wakiwemo wafanyakazi 14 wa kituo cha Clouds, imejiridhisha pasipo shaka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alivamia katika kituo hicho saa 4:30 usiku wa Machi 17 akiwa anaendesha gari yenye namba za usajili T553 BFH.

Amesema uchunguzi wa kamati umebaini kuwa sababu ya uvamizi huo ni habari iliyodaiwa kumuhusu mwanamke aliyedai kuzaa na Mchungaji Josephati Gwajima ambapo alitaka habari hiyo iruke kwenye kipindi..

Pia kamati hiyo imethibitisha kuwa Makonda na askari waliingia hadi katika vyumba ambavyo hawakupaswa kuingia, na waliingia hadi kwenye studio ambayo inarusha matangazo na kutoa vitisho kwa watangazaji, waandaji na wafanyakazi wengine, kiasi cha baadhi yao kuagua vilio.

“Vitisho hivyo ni askari wenye silaha za moto, kuingia ndani ya studio kibabe wakiwa na silaha za moto, Makonda aliwatisha usiku huo kwamba angewafunga jela miezi sita, pia angewakagua watangazaji wa kipindi kama wanahusika na dawa za kulevya, au kuwabana wadhamini wa kipindi na pengine kuwaingiza kwenye orodha ya wahusika wa dawa za kulevya endapo wangeendelea na msimamo wao” Amesema Balile

Pia amesema kamati imebaini kuingiliwa kwa uhuru wa habari kinyume cha sheria kwa kulazimisha kutangazwa kwa habari isiyokidhi vigezo.

Kuhusu wafanyakazi kupigwa, Balile amesema kamati hiyo haikuona uthibitisho wowote kuwa kuna watu walipigwa, isipokuwa wapo waliolia kutokana na vitisho vya kupelekwa jela miezi 6.

Kamati hiyo imetoa mapendekezo manne ikiwa ni pamoja kumtaka Makonda aombe radhi kwa tasnia ya habari, kumtaka Waziri kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka yake ya uteuzi ili hatua zichukuliwe, vyombo vya dola vianzishe uchunguzi wa ndani dhidi ya askari walioingia.

Amesema kamati hiyo ilijiridhisha kuwa Makonda hakuwa tayari kuhojiwa wala kutumia fursa ya kujieleza jambo ambalo hata hivyo halikuathiri uchunguzi wa kamati hiyo.

"Tulianza kwa kumpigia simu, lakini hakupokea, tukaamua kumpelekea ujumbe hakuujibu, tukatumia wasaidizi, wakatutaka tufike ofisini kwake, tulifanya hivyo, tulifika lakini ilielezwa kuwa ana mgeni, ulipofika muda akatuita, tukaelekezwa kupita ngazi za mbele lakini yeye akapita mlango wa nyuma akaondoka. Tukaambiwa tumsubiri, tukasubiri lakini baadaye tukaambiwa amepata shughuli nyingine kwa hiyo hataweza kurejea ofisini". Amesema Balile

Mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Waziri Nape amesema ataifikisha katika mamlaka husika kwa ajili ya hatua kuchukuliwa huku akiwataka wanahabari kuendelea kuwa na imani na serikali katika kulinda uhuru wa habari.

"Juu yangu kuna Waziri Mkuu, kuna Makamu wa Rais na kuna Rais, nitawakabidhi ripoti hii, nawaomba wanahabari, tuendelee kuwa watulivu, Rais wetu Magufuli ana nia njema na tasnia ya habari na ndiyo maana akaipitisha haraka sheria inayoipa hadhi tasnia hii... Wakati mwingine madhaifu yakitokea kwa mtendaji mmoja mmoja, yasiwe tope kwa serikali nzima....Mimi nitaipeleka taarifa kwa wenzangu, wataiangalia na litakuwa ni funzo kwa watu wengine" Amehitimisha Waziri Nape

Magazeti ya Leo Alhamisi ya tarehe 23/03/2017

Magazeti na vichwa vya magazeti ya Leo vinaletwa kwenu Kwa hisani ya Vodacom