ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatano, 28 Machi 2018

Machinga kupewa vitambulisho

Na Veronica Kazimoto,-Dar es Salaam,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  jana imezindua rasmi utoaji wa vitambulisho vya Wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi ikiwa ni pamoja na Wamachinga.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Charles Kichere alisema kuwa, utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo unatokana na marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 yaliyofanywa na Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi.

“Baada ya marekebisho ya Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018, zoezi hili la kuwatambua wafanyabiashara wadogo lilianza kutekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Idara ya Uhamiaji”, alisema Kichere.

Kichere alieleza kwamba, TRA  kwa kushirikiana na wadau hao, ilianza kutekeleza jukumu hilo kwa kuutambua Umoja wa Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambapo leo hii baadhi yao wamepatiwa vitambulisho maalum vya wafanyabiashara wadogo kama ishara ya uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho hivyo.

Aliongeza kuwa,  zoezi la kutambua vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo na kuwapatia Kitambulisho cha Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi linaendelea kufanyika nchi nzima na kubainisha kuwa, ili wafanyabiashara wadogo waweze kupata vitambulisho hivyo maalum,  wanatakiwa kujiunga katika vikundi vinavyotambuliwa kisheria na Serikali, kuwa na Kitambulisho cha Taifa, kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi ya kikundi alichojiunga nacho pamoja na kuchangia shilingi 10,000.

“Zoezi la kuwatambua wafanyabiashara wadogo linaendelea kufanyika nchi nzima na vitambulisho maalum vinavyotolewa kwa  wafanyabiashara hao vitadumu na kutumika kwa kipindi cha miaka mitatu (3). Maelezo ya mfanyabishara mdogo yaliyopo kwenye kitambulisho hicho maalum ni pamoja na jina na picha ya mfanyabiashara, jina la eneo analofanyia biashara, Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi na Sahihi ya mfanyabiashara husika”, Alifafanua Kichere.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam Mhe. Sophia Mjema aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kuwatambua wafanyabiashara wadogo ili waweze kupiga hatua kiuchumi kutoka daraja la chini hadi la kati na hatimaye kuweza kuchangia maendeleo ya nchi kupitia ulipaji wa kodi mbalimbali.

“Lakini kwanza naomba nimshukuru Mhe. Rais wetu John Pombe Magufuli kwa hii ndoto yake ya kuwasaidia wanyonge waliokuwa wanafanya biashara ndogo ndogo kutambulika na Serikali na kisha waondoke katika hali ya daraja la chini na kufikia daraja la kati.  Nafurahi kuwaeleza kwamba, ndoto ya Mhe. Rais wetu imetimia”, alisema Mjema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam Steven Lusinde alisema kuwa, wamefurahishwa na azma ya Serikali ya kuwatambua wafanyabiashara walio kwenye sekta isiyo rasmi kwa kuwa wamekuwa na hamu ya kuchangia maendeleo ya Taifa kwa muda mrefu.

“Sisi wamachinga tumekuwa na hamu kubwa sana ya kuchangia Taifa letu kwa sababu tunaamini chochote tunachokiona katika nchi hii bila sisi kuchangia hakiwezi kwenda”, alieleza Lusinde.

Moja ya majukumu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ni kukusanya mapato ya Serikali sambamba na kutoa elimu kwa walipakodi na watanzania kwa ujumla ili kuongeza uhiari wa ulipaji kodi na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yanahitajika katika kuleta maendeleo ya nchi pamoja na wananchi wake

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi ya March 28




Jumapili, 25 Machi 2018

Ujumbe wa Pasaka toka kwa Maaskofu wa KKKT

Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka, alipowatokea wanafunzi wake wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, aliwasalimu na kujifunua kwao kwa salaamu ya kuwatakia amani. 


Wapendwa watu wa Mungu, katika umoja wetu, sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tunawasalimuni nyote kwa kuwatakia amani. Bwana wetu Yesu Kristo Amefufuka kweli kweli - Haleluya!. Yeye ni amani yetu, na pia ni amani kwa watu wote wenye mapenzi mema. Kwa kufufuka kwake, upendo umeishinda chuki; unyenyekevu umeushinda ubabe; nuru imelishinda giza; haki imeshinda udhalimu; msamaha umeshinda visasi; ujasiri umeshinda hofu; na kwa hiyo uzima umeshinda kifo.

Mwaka 2017, Kanisa letu limeadhimisha miaka 500 ya Matengenezo ya Kanisa. Tukiwa wana Matengenezo tumekumbushwa tena kuwa mwanadamu anaokolewa kwa Neema ya Mungu tu: Wokovu Hauuzwi; Mwanadamu Hauzwi wala kununuliwa; na Uumbaji hauuzwi. Kanisa zima na dunia kwa ujumla tunaitwa kusimama pamoja na kuueleza ukweli huu unaoziweka huru dhamiri zetu (Yohana 8:31-32).

Matengenezo (Reforms) ni dhana ya kibiblia. Tangu zama za Agano la Kale, Mungu kwa nyakati mbalimbali aliteua wajumbe wake kuwasilisha ujumbe wake kwa jamii na kwa watawala wa dunia. Kwa Umungu wake, aliwainua wanawake na wanaume kwa makusudi ya kutoa unabii yaani, ujumbe wa Mungu kwa jamii au watawala. Wakati mwingine aliinua manabii kuwasemea wasiokuwa na sauti. Unabii na Matengenezo ni njia ya Mungu katika kusimika utawala wa haki na unaostawisha uhuru na amani.

Kwa namna ya pekee, manabii kama Daniel, walionya juu ya uongozi unaojenga uhalali wake katika wingi wa watu wanaokubaliana na uongozi huo hata kama ni katika makosa. Haikuwa rahisi kibinadamu kuukosoa mfumo kama huo lakini Mungu alitumia manabii kuzungumza na mfumo wa namna hiyo. Unabii wa Daniel 3:7 unasema, “Kwa hiyo watu WOTE, mara waliposikia sauti za baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari, na sauti za ala nyingine za muziki, walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebkadneza aliisimamisha”. Hapa tunaona kosa la kiongozi kutengeneza sanamu, linasababisha kosa la watu wanaokubali kuiabudu hiyo sanamu. Tumetafakari na kusadiki kuwa, kosa la kiongozi au mfumo, haliwaondolei hatia wanaomfuata kiongozi au kuufuata mfumo, hata kama watu hao walikula kiapo cha kutii maongozi ya kiongozi huyo na mfumo wake. Mbele ya Mungu hakuna ile kanuni ya kuwajibika kwa pamoja. Kila mtu kwa dhamiri yake anawajibika mbele za Mungu. Kwa upande mwingine, pamoja na uwajibikaji wa mtu binafsi, Nabii Ezekieli anatukumbusha na kutuonya kuwa tusipoonya na kusimama katika zamu yetu, hatia na damu ya wasio na hatia, itadaiwa mikononi mwetu (Ezekiel 33: 8-9).

Adhimisho la kufufuka kwa Yesu Kristo (Pasaka) na maadhimisho ya miaka 500 ya Matengenezo ya Kanisa, yanatusukuma kutafakari utume wa Kanisa katika jamii kwa nyakati zetu. Tunaalikwa kupeleka ujumbe wa amani kwa watu wote na kusimama kwa ujasiri katika kuwasemea wasio na sauti katika jamii ili kuenzi roho ya Pasaka na Matengenezo katika nyakati zetu. Kama Kanisa na kwa nafsi zetu mmoja mmoja, tunaitwa kwa upande mmoja, kufundisha, kushauri na kutia moyo. Kwa upande mwingine, tunaitwa kuonya, kukaripia, kukemea na kuelekeza kwa uvumilivu wote na upendo (2 Timotheo 4: 1-5).

Wajibu huu kwetu sisi maaskofu ni wito na utume usiokwepeka; na kwa watu wote wa imani, wajibu huu hauna mbadala. Tunaagizwa kuchochea ujenzi wa madaraja ya maridhiano katika upendo na amani, na kuwa kinyume na mifumo yote inayoendeleza chuki na marafakano. Kwa kufanya hivyo, imetupasa kusema wazi wazi ujumbe wa amani, upendo, heshima, utu, ustahimilivu na maelewano. Mfumo wowote unaojengwa katika utii wa sheria bila upendo; heshima bila uhuru; na amani bila haki, unajengwa katika msingi usio imara. Kupuuza wito huu kuna madhara kwa jamii yetu. Ni sawa na kujenga nyumba juu ya mchanga (Mathayo 7: 26). Tunasihi kwa machozi mengi, tuwe wajenzi wenye akili wajengao nyumba zao juu ya mwamba (Mathayo 7:24). Mwamba tunaotakiwa kujenga taifa letu lenye dini mbalimbali, vyama mbalimbali, na makabila mbalimbali, umetajwa katika sala kuu ya taifa letu, yaani, "DUMISHA UHURU NA UMOJA". Bila Uhuru hakuna umoja uwezao kuleta maendeleo; na bila umoja wa kitaifa, uhuru wetu hauleti amani endelevu. Kwa sababu ya nguvu ya dhamiri safi iliyo dira ya taifa letu, tunalazimika kumtii Mungu kuliko mwanadamu (Matendo 5:29).

B. TAIFA LETU NA AMANI YETU
Tunapoadhimisha sikukuu ya kukumbuka kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, tunatambua kuwa utume wa Kanisa letu katika taifa letu, unafanyika katikati ya changamoto kadhaa. Kwa kuwa Kanisa ni sehemu ya jamii, linaguswa na changamoto hizo. Katika kukaa pamoja na kuliombea taifa letu, sisi maaskofu wa KKKT, tumetafakari na kubaini changamoto hizo. Kwa njia ya salaam za Pasaka, tunaleta kwenu changamoto tatu ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake.

1. Jamii na Uchumi
Kiini cha Utume wetu katika jamii kinatuingiza kwa nia njema katika maisha ya uchumi na mshikamano wa kijamii. Neno la Mungu linatufundisha kuwa "Mwanadamu hawezi kuishi kwa mkate peke yake" (Luka 4:4). Pia neno la Mungu linatuhakikishia kuwa Bwana wetu Yesu Kristo alikuja ili tuwe na uzima tele (Yohana 10:10). Tunawiwa katika umoja wetu wa ubaba, kuipongeza serikali yetu kwa jitihada inazofanya kuboresha maisha ya wananchi. Tumeshuhudia jitihada na nia njema kuhusu uvunaji na umilikaji wa raslimali za nchi kwa manufaa ya taifa zima. Aidha, tunapongeza jitihada za ukusanyaji wa kodi ili kuiwezesha serikali kugharamia huduma za jamii. Hata hivyo, bila kukatisha tamaa jitihada hizo, tunawiwa kushauri yafuatayo:

I. Sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo, si washindani wa serikali katika kuchangia maendeleo ya taifa. Mazingira yasiyo rafiki kuhusu wadau hawa, ni kikwazo kisicholeta mshikamano kati ya serikali na sekta binafsi na mashirika ya dini katika kuleta maendeleo. Jitihada za makusudi na za mara kwa mara zifanyike kuondoa dhana ya ushindani kati ya serikali na wadau hawa ili kuimarisha mahusiano mema kati ya serikali na sekta binafsi.

II. Ili mfumo wa ukusanyaji wa kodi uwe endelevu; jitihada za kukusanya kodi ziendane na elimu kwa mlipa kodi. Msisitizo wa uzalendo wa kulipa kodi uende sambamba na ustawi wa walipa kodi katika shughuli zao za biashara. Mivutano isiyo na tija kati ya walipa kodi (wafanya biashara) na mamlaka ya ukusanyaji wa kodi, inastawisha uadui unaopunguza makusanyo ya kodi na kujenga ushawishi wa rushwa. Mfumo wa kodi unaowafilisi wafanya biashara, haulengi kujenga uchumi wa viwanda.

III. Kutokana na ongezeko kubwa la vijana wasio na ajira; jitihada za wazi na za makusudi zifanyike ili msukumo wa uchumi wa viwanda ufikie matumaini yanayoshikika miongoni mwa vijana wasio na ajira. Sekta binafsi, wawekezaji na wadau wengine, wahakikishiwe usalama wa mitaji yao kisheria. Hili likifanyika ni kichocheo kizuri cha ujenzi wa viwanda.

IV. Uchumi wa viwanda (vidogo na vikubwa) uendane na uwekezaji katika sekta ya kilimo maeneo ya vijijini. Kilimo na ufugaji ndizo sekta zenye wigo mpana wa viwanda vinavyogusa maisha ya watanzania walio wengi. Utozaji holela wa kodi na ushuru wa mazao unakatisha tamaa wadau wa kilimo. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja, na wakulima/wafugaji na wawekezaji kwa upande wa pili, si kivutio cha uwekezaji katika sekta ya kilimo.

2. Maisha ya Siasa
Kwa umoja wetu katika utume, tunatambua siasa safi na uongozi bora kuwa ni misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika taifa letu. Ujio wa vyama vingi mnamo 1992, haukuondoa umuhimu wa misingi hii bali ulipanua matumizi ya demokrasia iliyojengwa katika uhuru wa mawazo. Taifa ni mkusanyiko wa taasisi na watu mbalimbali, wenye lengo moja lakini kwa njia mbalimbali. Kutokana na wingi huu, taifa letu daima ni juu ya vyama, taasisi na makundi.

Taifa huongozwa na katiba iliyo kiini cha sheria zote. Taifa haliongozwi na ilani za vyama. Serikali haiongozwi na ilani za vyama. Serikali huongozwa na katiba, sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi na tunu za taifa). Serikali husimamiwa na bunge huru lililo sauti ya wananchi. Wananchi ndilo chimbuko la madaraka ya bunge. Bunge halisimamiwi na ilani, chama chochote wala mtu awaye yote. Kwa umoja wetu na kwa nyakati zetu, hivi sasa tunashuhudia matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi iliyolilea taifa letu. Baadhi ya matukio hayo ni:

I. Hofu iliyojengwa katika matukio halisi yakiwamo utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.

II. Kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari. Kwa mwenendo huu, kuna hofu kuwa hata uhuru wa kuabudu uko mashakani.

III. Kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi. Hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

IV. Kukosekana kwa mazingira ya haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi zote zimeghubikwa na ubabe, vurugu, hila, na vitisho.

V. Utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi. Hatua hii imeimarisha ubaguzi wa kiitikadi katika taifa letu na kukuza migawanyiko.

VI. Kushamiri kwa chuki mioyoni mwa watu ambalo ni chimbuko la visasi, kukata tamaa, na ushiriki mdogo wa wananchi katika chaguzi na maisha ya siasa.

VII. Udhalilishaji wa kauli njema isemayo "Maendeleo hayana chama". Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu anajiuzuru chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama kingine? Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu wanaokufa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali.

Mambo haya ni tishio linalohatarisha umoja na amani ya nchi yetu.

3. Masuala Mtambuka
Kanisa ni alama ya uwepo wa utume wa kuleta na kutunza matumaini katika jamii. Ukimya wa Kanisa katika masuala yanayoigusa jamii ni ukwepaji wa wajibu wake. Lakini pia sauti ya Kanisa isiyomilikiwa na mtu isipokuwa Mungu tu, ni chachu ya amani na matumaini. Kwa dhamiri safi inayotokana na utambuzi wa "Wakati wa Mungu"(Kairos) katika taifa letu, tunawiwa kutambua masuala mtambuka yanayogusa maisha ya watu kipekee na kwa njia nyingi na kuyatolea ushauri ufuatao:

I. Kuhitimisha mabadiliko ya mara kwa mara katika mfumo wa elimu nchini ili kuondoa mwanya wa kila mtendaji mkuu wa wizara kuja na sera yake. Elimu ni kitovu cha ustawi wa taifa, kisiwe kinachokonolewa chokonolewa kila wakati. Sekta zote nchini hujenga mafanikio yake katika mafanikio ya mfumo thabiti wa elimu.

II. Uwezeshaji wa vijana kupata mikopo ya elimu ya juu uwe shirikishi na usiokuwa na "ubaguzi" kati ya wanafunzi wa vyuo binafsi na wale wa serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini na wenye nafasi; waliosoma shule binafsi na wale wa shule za serikali, n.k. Kwa kuwa huu ni mkopo, jitihada ziwekwe zaidi katika urejeshaji wa mkopo huo kwa kuzingatia kuwa huu ni mkopo kwa mtoto siyo kwa mzazi.

III. Vyombo vya usimamizi wa sheria na utoaji haki vionekane vinatenda haki sawa kwa watu wote na makundi yote bila kuacha ishara za fadhila au kukomoana.

IV. Wajibu wa serikali kikatiba katika kulinda uhai wa raia wake, uonekane unatekelezwa bila kuacha mwanya wa kuituhumu serikali. Ukiachwa mwanya katika ulinzi wa uhai wa raia, waweza kutumiwa na mamluki kujichukulia sheria mkononi kwa niaba ya serikali. Damu isiyo na hatia

ina madhara kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo. Mpaka sasa tumeshuhudia umwagaji wa damu unaotusuta sisi sote na mamlaka zote. Mungu anatusuta watanzania kama alivyomsuta Kaini: "Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi" (Mwanzo 4:10).

V. Uhai wa mtu una thamani isiyopimika. Ni wajibu usiokwepeka kuulinda na kuutunza uhai kwa vitendo halisi. Endapo uhai umepotea katika mazingira yoyote, uchunguzi huru na wa haki ufanyike na taarifa zitolewe kwa wakati muafaka ili kujenga jamii yenye imani kwa serikali na vyombo vyake. Matukio ya mauaji ya askari wetu, mauaji ya raia, majaribio ya kuwaua wanasiasa, utekaji, na uteswaji visipochunguzwa na kutolewa taarifa, ni shina la hofu na uchungu katika jamii. Jamii iliyojaa hofu na uchungu, haiwezi kuwa na maendeleo wala kuwa na roho ya uzalendo.

VI. Ili kulipatia taifa letu ufumbuzi wa mambo yote tuliyotaja na kushauri kwa wakati huu na ujao; tunaisihi serikali ya awamu ya tano, kurejea mchakato wa upatikanaji wa KATIBA MPYA ya wananchi, iliyopendekezwa na wananchi kupitia Tume ya Warioba. Watanzania wengi wanaona na kuamini kuwa KATIBA MPYA ina majibu ya kukidhi mahitaji ya taifa letu kwa sasa na baadaye. KATIBA MPYA ni zao la utashi wa Watanzania kupitia tume ya Warioba iliyokuwa na uwakilishi mpana wa taifa letu.

VII. Aidha, tunawashauri raia wema, kwa njia za kidemokrasia kupitia majukwaa ya kikatiba yaliyo katika maeneo yao, kudai upatikanaji wa KATIBA MPYA. Itapendeza ikiwa KATIBA MPYA itapatikana kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Mambo mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano yatadumu iwapo kuna KATIBA MPYA inayolinda mazuri. Kiongozi mzalendo si mbadala wa KATIBA MPYA. Tanzania yenye amani na maendeleo ni tunda la itikadi zote, dini zote, makabila yote na makundi yote chini ya KATIBA MPYA.

C. HITIMISHO
Kufufuka kwa Yesu Kristo ni kiini cha Matengenezo ya Kanisa. Kwamba, katikati ya jamii iliyokata tamaa na kutawaliwa na hofu, Kristo alifufuka na kuleta matumaini mapya. Kwamba, katikati ya wasiwasi wa Kanisa kupoteza nguvu ya utume wake, Roho Mtakatifu aliongoza Matengenezo ya Kanisa. Kwa hiyo Matengenezo ni endelevu katika jamii ya watu na taasisi zao. Muasisi wa Matengenezo Dr. Martin Luther yungali analiwajibisha Kanisa kuzingatia utume wake unaoleta matumaini mapya kila siku. Waliobatizwa wote ni wamisionari tunaotumwa na Bwana wetu Yesu Kristo (Yohana 20:21). Imetupasa kuwa nuru na chumvi ya jamii na kuwa mawakala wa uhuru, umoja na amani.

Taifa letu lilipata uhuru mwaka 1961 bila kumwaga damu. Roho ile ile ya majadiliano na maridhiano iliyokuwamo ndani ya waasisi wa taifa letu, inatakiwa kila wakati. Uhuru ulioletwa kwa majadiliano, utunzwe na kulindwa bila ulazima wa kumwaga damu ya watanzania. Uhuru na Umoja ndizo ngao zetu zilizolitunza taifa kwa zaidi ya miaka 50.

Sisi tulio maaskofu kwa neema ya Mungu, tunaleta wito kwenu wenye imani katika dini mbalimbali, kuliombea taifa letu. Kuwaombea wote wenye madaraka ili wajaliwe hekima, busara na upendo kwa taifa na watu wake. Kupitia jumuia ndogo ndogo na sharika zote, waombee viongozi wetu ili Mungu awajalie na kuwatunuku kiu ya kutenda haki, kusikiliza kuliko kusema, kuelekeza kuliko kuamrisha, kuunganisha kuliko kutawanya, kupenda watu kuliko kutamani kupendwa na watu, kutamani kutumika kuliko kutumikiwa (Marko 10:45), kuheshimu kuliko kuheshimiwa.

Ujumbe wa Pasaka unatuhimiza kuthamini uhai. Bwana wetu Yesu Kristo alikubali kufa ili kuhifadhi uhai wetu. Kwa kufa kwake na kufufuka, amekomesha kifo na mawakala wake. Tunaitwa kuthamini uhai na kutoruhusu tena watu kuteswa na kuuawa. Kwa hekima yote na unyenyekevu, tunasihi tena, kwamba ikubalike kuwa hitaji la watanzania walio wengi kwa sasa ni KATIBA MPYA. Katiba Mpya ipatikane ili kukuza na kuimarisha mfumo wa utawala utakaolinda uhai wa watu, raslimali za nchi, tunu za taifa, uhuru wa mihimili ya dola, na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.

Tunawatakia Pasaka njema ya mwaka 2018, na Mungu awabarikini nyote. 

Advertisement

Mwigulu Nchemba Ataka VIBOKO Vitumike Shuleni Ili Kuwajengea Maadili Wanafunzi

WAZIRI wa Mambo ya ndani, Dk  Mwigulu Nchemba amewataka walimu kuendelea kutoa elimu bora kwa wanafunzi kwa kuwafundisha maadili mema na inapobidi matumizi ya fimbo yatumike.

Akizungumza katika harambee ya ujenzi wa mabweni ya Shule ya Sekondari  Lulumba Wilaya ya Iramba mkoani Singida, jana, Dk Nchemba alisema walimu wanatumia fimbo kunyoosha nidhamu za wanafunzi ili kutengeneza hatma ya nchi.

“Kuna wakati walimu wananyoosha nidhamu za wanafunzi lakini ninyi hamuoni hii na kulalamika tu, kinachofanyika ni kwa manufaa yetu…niwaombe kwenye kutumia mifano tumieni mifano na kwenye kutumia fimbo fanyeni hivyo ili kutengeneza taswira ya nchi yetu,” alisema Dk Mwigulu.

Alisisitiza kuwa ni lazima kuendelea kulinda hadhi za walimu kwa kuwapatia miundombinu bora ya ofisi na vyumba vya madarasa.

Alisema majengo ya taasisi yanapaswa kuwa bora zaidi na sio kutumia ramani za awali pekee kwani zinapaswa kuboreshwa kulingana na maendeleo yaliyopo.

“Naunga mkono ujenzi huu wa mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa vyumba vya madarasa na ofisi za walimu hivyo nachangia mifuko 200 ya saruji nawaahidi pia kutoa Sh milioni sita,” alieleza.

Mkuu wa Wilaya Iramba, Emmanuel Luhaula alisema shule higo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma kutokana na umahiri wa walimu kwani watoto hao wanajua kujieleza kama vile wanasoma chuo kikuu.

Alisema wananchi wa Iramba wanatakiwa kujivunia  kuwa na shule zao pamoja na walimu hao ili kuboresha elimu wilayani humo.
 
“Unafanya jitihada ili kuhakikisha kila sekondari kunajengwa mabweni ili kuondoa kero za wanafunzi.Sisi wa Iramba tushindwe wenyewe kukutumia. Nimekuwa Mbunge lakini anayoyafanya mbunge huyu Mimi sikuyafanya,” alisema Luhaula.

Naye, Mkuu wa shule hiyo, Jeremiah Kitiku alisema licha ya kufanya vizuri kitaaluma, wanakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa baadhi ya majengo, upungufu vitabu vya masomo ya kiada 274.
 
“Mahitaji ya vitabu vya kiada no 2,802 vilivyopo 2,328 upungufu ni 274. Pia tunachangamoto ya kutokuwa na uzio kwa usalama wa wanafunzi, walimu na mali za shule,” alisema Kitiku
 
Hata hivyo, alisema malengo ya shule hiyo ni ukarabati wa vyumba tisa vya madarasa na  ofisi za nane za walimu ambazo zitagharimu Sh Milioni 169.4.
 
Katika harambee hiyo, saruji iliyokusanywa ni mifuko 209, ahadi  ya fedha ni 8,486,000, ahadi ya mifuko ya saruji 572, Gypsum 50 na  nondo tani moja jumla ya ahadi na fedha taslimu ni 19,494,300

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili ya March 25



      PAMOJA TUNASONGA