ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumanne, 30 Agosti 2016

Lowassa, Mbowe Watakiwa Kuripoti Polisi Leo

Viongozi waandamizi wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana walikamatwa na Jeshi la Polisi wakati wakiwa katika kikao cha ndani katika Hoteli ya Giraffe mkoani Dar es Salam

Lowassa, ambaye alikaa kituoni hapo kwa takribani saa tatu anaweza kuwa kiongozi wa kwanza aliyewahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu kuhojiwa na polisi.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwataja viongozi wengine waliokamatwa kuwa ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa.

Mara baada ya kukamatwa, walipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako baadhi ya wajumbe na wabunge waliwafuata na kuwasubiri nje ya kituo hicho kujua hatima yao. 
Viongozi hao walionekana wakiingia Polisi saa 10.30 jioni na kutoka saa 1.25 usiku, jambo ambalo liliwafanya wakae kituoni hapo kwa saa tatu. 
Lissu alisema polisi walivamia kikao hicho kilichokuwa na wajumbe 170, wakiwamo baadhi ya wabunge wa chama hicho na kuwakamata viongozi hao kwa maelezo kuwa wamekaidi amri ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya ndani na nje ya vyama vya siasa. 
Imeelezwa kuwa viongozi hao wa Chadema walikuwa na mkutano uliotanguliwa na kikao cha viongozi wakuu na kufuatiwa na cha viongozi hao kikijumuisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri. 
Wakiwa katika kikao hicho, ilielezwa kuwa watu wanne waliingia wakiwa wamevalia kiraia na kuwaeleza kuwa viongozi wao wanahitajika kituo kikuu cha polisi kutokana na kufanya mkutano kinyume cha sheria. 
Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza ambaye  alikuwa kwenye mkutano huo alisema pamoja na mambo mengine ya chama, walikuwa wakijadili suala la operesheni Ukuta la Septemba Mosi kama liendelee au lisiendelee kutokana na hali ilivyo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwao, alisema viongozi hao walikamatwa kwa kukukaidi amri ya polisi ya kuzuia mikusanyiko ya kisiasa na kuchochea wananchi kuandamana kinyume cha sheria Septemba Mosi. 

Alisema baada ya kuachiwa kwa dhamana, viongozi hao wametakiwa kuripoti kituoni hapo leo. 
Wiki iliyopita, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamishana wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Marijani lilipiga marufuku mikutano ya ndani likisema inatumika kuhamasisha watu kuvunja sheria za nchi na kupambana na askari. 

Hatua hiyo ilikuja huku jeshi hilo likiwa limepiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano kufuatia uamuzi wa Rais John Magufuli kuzuia shughuli  za kisiasa hadi 2020. 

Wanafunzi hewa 4,445 wabainika Kahama

 Image result for kahama
Imeandikwa na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo, amesema Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, ina wanafunzi hewa 4445 ambao wanasoma katika shule za sekondari za serikali kinyume na utaratibu.
Jaffo aliyasema hayo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri za Msalala na Mji, juzi, katika ziara ya kushitukiza, ambapo aliwaasa kufanya kazi kwa weledi kwa kufuata sheria na taratibu za kuwahudumia wananchi.
Alisema kuwepo kwa idadi hiyo kubwa ya wanafunzi hewa katika shule za sekondari kunatokana na maofisa elimu kutokujua takwimu za wanafunzi na kuongeza kuwa, muda mwingi wamekuwa wakikaa ofisini bila ya kutembelea maeneo ya kazi.
Naibu Waziri huyo alisema, takwimu za utengenezaji wa madawati, zimekuwa kinyume na ilivyotarajiwa, hali ambayo imesababisha kuchelewa kumalizika kama iliovyokuwa imepangwa na Rais John Magufuli.
Pamoja na mambo mengine, Naibu Waziri huyo aliwaonya watumishi hao kutotumia fedha vibaya zitakazotolewa na wizara hiyo, kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya barabara katika halmashauri ya mji wa Kahama.
Mbunge wa Jimbo la Kahama, Jumanne Kishimba alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa Halmashauri ya Mji wa Kahama, ina changamoto nyingi zikiwamo za miundombinu ya barabara, kuzidiwa kwa wagonjwa wanaotoka katika wilaya 16 katika hospitali ya halmashauri ya mji pamoja na upungufu wa watumishi.
Alisema Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, imezidiwa na wagonjwa ambao wanatoka katika sehemu mbalimbali zilizopo jirani, hali ambayo watumishi wake wanapata wakati mgumu katika kutoa huduma na wakati mwingine kushindwa kutoa huduma kwa wakati.

Ajira zinakuja mh Angella Kairuki asema :. Nawashauri vijana wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja


SERIKALI imeanza kuwashughulikia watumishi walionufaika na fedha za watumishi hewa ambapo hadi sasa watumishi 839 wapo katika hatua mbalimbali wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.
Sambamba na hilo, serikali inatarajia kutoa ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kukamilisha uondoaji wa wafanyakazi hewa. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na mikakati ya wizara yake katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1). Kairuki alisema,
“Kwa sasa tayari wapo watumishi wameshahojiwa na kuchukuliwa maelezo yao polisi na upelelezi utakapokamilika watachukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani… Tunakamilisha ushahidi na tutawatangazia tutakapokamilisha,” alisema.
Alisema waligundua kwamba kuna maofisa utumishi na wahasibu ambao siyo waaminifu, badala yake walikuwa wakielekeza fedha kwa ndugu zao na miradi yao na wengine walishastaafu lakini bado majina yao yalikuwa yakiendelea kupokea mishahara wakati walitakiwa kuondolewa kwenye mfumo.
Alisema kwa kipindi cha Machi mosi hadi Agosti 20 mwaka huu, watumishi hewa waliogundulika ni zaidi ya 16,127 na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Kwa kipindi cha Agosti pekee watumishi hao hewa wangelipwa mishahara wangeisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 16.
“Uhakiki huu ni endelevu na tumegundua changamoto kubwa katika usimamizi wa mishahara ni uadilifu kwa watu waliokasimiwa madaraka. Maofisa Utumishi, Maofisa Utawala na Wahasibu wamepewa madaraka lakini wengi wao siyo waaminifu, hivyo kwa sasa tumeweka uwajibikaji kwa waajiri,” alisema.
Aidha alisema wanaufanyia mfumo wao maboresho zaidi ili uweze kuchakata taarifa nyingi zaidi ambapo pia sekta ya mishahara imeshushwa katika ngazi za chini zaidi hasa katika sekta za elimu na afya ambazo zimekutwa na watumishi hewa wengi zaidi ili waweze kuwa na taarifa za mtumishi mmoja mmoja.
Alisema upo muongozo ambao fedha za serikali zinaporejeshwa zinapitia hazina na kusisitiza kwamba wataendelea kuhakikisha wanasimamia fedha zote ambazo zilichukuliwa serikalini kinyume na utaratibu na isivyo halali zinarudishwa kwa mfumo sahihi.
Pia alisema wameongeza kasi ili kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya kazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo wanaanda mkataba wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma na ikiwezekana utaanza kutumika mwaka ujao wa fedha.
Alisema serikali imefanya maboresho makubwa katika mishahara na motisha kwa ajili ya maslahi ya watumishi wa umma, sambamba na kuhimiza taasisi mbalimbali kuweka vitendea kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akizungumzia ajira hizo mpya Kairuki aliwatoa hofu watanzania waliokuwa wanatarajia ajira serikalini na kusisitiza kwamba walichokuwa wanasubiri ni takwimu halisi kwa taasisi ili kujua ni watumishi wangapi wameondolewa.
“Baada ya kukamilisha mchakato huo, hatua nyingine zitaendelea… Hii ni neema kwa waliomaliza vyuo, cha msingi wavute subira maana tutatoa ajira 71,496 kwa mwaka huu wa fedha na hatukuzifuta ajira. Nawashauri vijana wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja,” alisema. Katika hatua nyingine, Kairuki alisema, wamepokea malalamiko zaidi ya 200 kutokana na ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa Utumishi wa Umma ambayo inamnyima mtumishi kutotumia madaraka yake vibaya.
“Katika malalamiko hayo 142 yanahusu sheria ya maadili. Sekretarieti ya Maadili imefanya uchunguzi wa awali na malalamiko 12 yataanza kufikishwa Baraza la Maadili na hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa ikiwemo kushushwa vyeo au kuachishwa kazi,” alisema.
Pia aliwaagiza maofisa utumishi kuwahudumia watumishi na kuwapa haki zao ikiwemo kuwapandisha madaraja kwa wakati pale wanapostahili. Aidha Kairuki alikemea tabia ya baadhi ya watu kughushi taarifa za utumishi wa umma na kusisitiza kwamba jambo hilo ni kosa kubwa kwa yeyote anayefanya hivyo.
“Mtu yeyote ambaye anatoa nyaraka za serikali na siyo mlengwa au anayetoa nyaraka ambayo imewekewa zuio kwa mujibu wa sheria ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Tunawasisitiza watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia sheria hizo na mwongozo wa utoaji nyaraka na kumbukumbu za taarifa za serikali,” alisema.
 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjPIRiuCu-pbeMneQbRw6xO4fK054P32No4NJciADd8tYSD2QmTI1047hLx3Q-zGgWxYOazVOcCJf0LSIthRjWY2PiXDf_vM3buIwd25Wf6YO-J5pZWiqY_cGKNE63-haqgWI7gjmobmAND/s640/IMG-20160815-WA0011.jpg

Magazeti ya Leo jumanne ya tarehe 30/08/2016