ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 6 Februari 2016

HAO NDIO MAWAZIRI VIVULI

KAMBI rasmi ya upinzani bungeni, imetangaza baraza lake la mawaziri kivuli ambalo Chama cha ACT Wazalendo, chenye mbunge mmoja, Kabwe Zitto, ndicho hakikuingizwa kwenye baraza hilo. Kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe alitangaza jana bungeni baraza hilo.
Chadema chenye wabunge wengi katika kambi hiyo, kina mawaziri vivuli wengi ikilinganishwa na vyama vingine na wakati huo huo, kina wizara nyingi ambazo kinaongoza peke yake kwa maana ya kuwa na mawaziri na naibu mawaziri vivuli.
Mawaziri, naibu mawaziri vivuli wa Chadema ni katika Wizara ya Ofisi ya Rais, Tamisemi, ambayo Waziri Kivuli ni Mbunge wa Moshi Mjini, Japhary Michael (Chadema) na Naibu wake ni Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi (Chadema).
Wizara ya Fedha na Mipango inaongozwa na wabunge wa Chadema ambao ni Halima Mdee wa Kawe na Mbunge wa Momba, David Silinde. Kwa upande wa Wizara ya Nishati na Madini pia inaongozwa na wabunge wote wa Chadema. Waziri kivuli ni Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Naibu wake ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaongozwa na Mbungewa Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Sakuru (Chadema).
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inaongozwa na wabunge wa Chadema; ambao ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye ni waziri kivuli akisaidiana na wa Viti Maalumu, Devotha Minja.
Kwa upande wa wizara ya Utumishi, Utawala Bora inaongozwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema) pekee bila naibu.
Mawaziri Chadema kuhusu wizara ambazo mawaziri vivuli ni wa Chadema na manaibu ni wa vyama vingine, ni Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu inaongozwa na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema). Bulaya anasaidiana na manaibu ambao wote ni wa CUF.
Nao ni Mbunge wa Chake Chake, Yusuf Kaiza Makame na Abdallah Maftah wa Mtwara Mjini .
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa inaongozwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na Naibu wake Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Mngwali (CUF).
Mambo ya Ndani ya Nchi amepangiwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (Chadema) akisaidiwa na Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaongozwa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Viti Maalumu, Salma Mwassa (CUF).
Waziri kivuli mwingine ni Suzane Lyimo wa Viti Maalumu anayeongoza Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi akisaidiana na Mbunge wa Mgogoni, Dk Ali Suleiman Yusuf (CUF) ambaye ni naibu.
Wizara ya Katiba na Sheria inaongozwa na Mbunge Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema ) akisaidiana na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolela (CUF).
Mawaziri wa CUF, Wizara zinazoongozwa na CUF kwa maana ya waziri kivuli kutoka chama hicho, ni Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ambayo Mbunge wa Malindi, Ali Saleh Ali(CUF) anasaidiana na Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema).
CUF imepata pia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo Waziri kivuli ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) na naibu ni Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Immaculate Semesi (Chadema).
Kwa upande wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi laKujenga Taifa, inaongozwa na Mbunge wa Ole, Juma Hamad Omary (CUF) na naibu wake ni Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema). Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) anaongoza wizara ya Maji na Umwagiliaji akisaidiwa na Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema).
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR) amepangiwa wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akisaidiwa na Naibu ambaye ni Mbunge wa Karatu, Qambalo Qulwi (Chadema). Kiongozi wa Upinzani bungeni, Mbowe aliomba wote wanaohusika watoe ushirikiano kwa baraza hilo kadri inavyowezekana.

Hakuna maoni: