ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 30 Januari 2016

Simba, Yanga leo tena

DURU la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara linaanza leo wakati timu 12 zikiwemo za Yanga na Simba kushuka kwenye viwanja tofauti kusaka pointi tatu muhimu. Hata hivyo, Azam FC inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, leo ilitakiwa kucheza na Prisons ya Mbeya, haitashuka dimbani kwa sababu inashiriki mashindano ya timu nne nchini Zambia.
Yanga wenyewe wako kileleni wakiwa na pointi 39 sawa na Azam FC, lakini wanaongoza kwa uwiano wa tofauti ya magoli, leo watakuwa wageni wa Coastal Union katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Katika mchezo wa raundi ya awali, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Yanga watataka kudhihirisha kuwa hawakubahatisha kuifunga Coastal katika mchezo wa kwanza, huku Wagosi hao wa Kaya nao watataka kudhihirisha wao sio wanyonge mbele ya mabingwa hao watetezi.
Vijana hao wa Jangwani wakishinda leo watakuwa wamejikusanyia pointi 42 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo na kuiacha Azam FC ikibaki na pointi zake 39 katika nafasi ya pili.
Kwa upande wa Simba, wenyewe katika mchezo wa kwanza dhidi ya African Sports uliochezwa Mkwakwani, iliibuka na ushindi kiduchi wa bao 1-0, hivyo na leo itataka kuendeleza ubabe dhidi ya vijana hao wa Tanga.
Simba yenye pointi 33, inazihitaji sana pointi tatu kutoka kwa African Sports ili angalau izidi kujisogeza katika nafasi ya tatu nyuma ya Azam katika mbio hizo za ubingwa wa ligi hiyo.
Kwa sasa Simba inafundishwa na Mganda Jackson Mayanja aliyechukua nafasi ya Muingereza Dylan Kerr aliyetimuliwa licha ya timu hiyo kuwa katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo.
Mayanja alisema pamoja na ugumu wa mchezo huo, watajitahidi kuibuka na ushindi ili kuendelea kuzifukuza Yanga na Azam FC zilizoko kileleni. Coastal Union na African Sports ziko katika nafasi ya 14 na 15 baada ya kucheza mechi 15 na kuambulia pointi tisa na 10 badala ya kuwa na pointi 45 kutoka katika mechi hizo 15 za duru la kwanza.
Mechi zingine leo ni JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Majina ya Songea, huku Mtibwa Sugar wakiikaribisha Stand United, wakati Mwadui FC itaikaribisha Toto African wakati Kagera Sugar watacheza na Mbeya City na Mgambo JKT watakuwa wenyeji wa Ndanda FC.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa Mgambo kuikaribisha Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. Kwa upande wa ufungaji mabao, Amis Tambwe ndiye anayeongoza hadi duru la kwanza linapomalizika baada ya kupachika mabao 13 huku Hamisi Kiiza wa Simba akifuatia kwa mabao 10.

Hakuna maoni: