ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 30 Januari 2016

Mahakama ya mafisadi yaiva

SERIKALI imewahakikishia Watanzania kuwa mchakato wa kuanzishwa kwa Mahakama Maalumu ya mafisadi na wezi, umefikia hatua nzuri. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema hayo juzi bungeni mjini hapa, wakati akichangia Hotuba ya Rais ya Ufunguzi wa Bunge.
Akizungumzia mchakato wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo maalumu, Mwakyembe alisema unakwenda vizuri na utakapokamilika Watanzania watafahamishwa. “Kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, akitoa tamko lazima litekelezwe.
Kama tunakumbuka Rais, kwa nyakati tofauti kipindi cha kampeni, aliahidi kuanzisha Mahakama Maalumu ya Mafisadi na Wezi,” alisema Mwakyembe. Akiizungumzia hotuba ya Rais, Mwakyembe alisema ikiachwa hotuba ya Mwalimu Nyerere, ya Magufuli pia ni bora na iligusa mioyo ya Watanzania wenye nia njema na Taifa.
“Wakati rais anatoa hotuba yake iliyokuwa na aya 160, alipigiwa makofi na vigelegele mara 137, ni zaidi ya asilimia 86, ya Dk Martin Luther ambaye ni Mmarekani mweusi,” alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo, imewaweka pabaya wapinzani waliokuwa wanapinga kila kitu.
Dk Mwakyembe alisema tatizo ni kwamba kwa hotuba hiyo, yeyote akijaribu kuipinga, wananchi watamuona wa hovyo. Aliendelea kusema; “Wamejaribu (upinzani) kutoka kwenye mjadala, kwa hoja tu ya TBC (Shirika la Utangazaji Tanzania), ili wasiwepo kwenye mjadala, kwani wakiwepo lazima wataisifia tu.”
January na Tanzania Mpya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba alisema safari ya kutengeneza Tanzania Mpya, haitakuwa nyepesi na ni lazima wajaribiwe, watiwe shaka na kukatishwa tamaa kuhusu mwelekeo wao.
Akijibu hoja za wabunge zilizotolewa wakati wa kujadili hotuba hiyo ya Rais Magufuli ya ufunguzi wa Bunge, aliyoitoa Novemba mwaka jana, January alisema;“ni kama kutengeneza keki ya mayai, lazima upasue mayai”.
Aliendelea kusema, “watu wasipate mashaka wala wasiwasi kwamba nchi inaelekea katika mwelekeo usiofaa. Tulifika mahala tukahitaji Rais wa namna hii, tumempata na tumuunge mkono.”
Kauli ya Waziri inalenga kujibu kauli za baadhi ya watu, ikiwemo wabunge wa vyama vya upinzani, ambao hivi karibuni walikosoa kazi ya ‘kutumbua majipu’ inayofanywa na Rais Magufuli pamoja na waziri, wakidai kwamba haizingatii taratibu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene alisema kazi ya Rais Magufuli ya kuisuka Serikali haijakamilika, kwani anaendelea kwa wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi hadi kwa wakuu wa idara, watakaochujwa kuhakikisha wanaendana ya kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Alisema Tanzania mpya ya Magufuli inayokuja ni ya watu wanaofanya kazi. Tunataka tuwahakikishie kwamba Rais anaendelea kuisuka serikali na mtambue kwamba serikali bado haijakamilika, bado tunahitaji wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya lakini tunakwenda vizuri zaidi tunataka kusuka wakurugenzi.
“Tunakwenda mbali kusuka mpaka wakuu wa idara, tunataka tuwachuje vizuri kabisa na siyo kuokotana okotana. Tunataka Tanzania mpya tukianzia juu tukisema hapa kazi tu basi ni hapa kazi,” alisema.
Hotuba ya Rais Bungeni Akizungumzia Mapambano Dhidi ya Rushwa na Ufisadi, alipofungua rasmi Bunge mjini Dodoma, Novemba 20, mwaka jana, 2015, Rais Magufuli alisema, “Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia. Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo.
Mimi pia ninachukia rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.”
Magufuli alisema “Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka nirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine.
Hivyo ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na muniunge mkono wakati natumbua majipu haya.” Alieleza kuwa anafahamu ugumu wa vita aliyoamua kuipigana na anafahamu ugumu na changamoto zake kwa sababu wanaojihusisha na rushwa, sio watu wadogo wadogo.
Alisema Vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara makubwa kwa nchi na ustawi wa nchi yetu, hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za uongozi na utumishi, ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya watu.
“Katika kushughulikia tatizo hili, nimeahidi kuunda Mahakama ya Rushwa na Ufisadi. Ni matumaini yangu vyombo husika katika jambo hili havitanikwamisha,” alisema Magufuli.

Hakuna maoni: