ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 1 Januari 2016

Maxime amlalamikia mwamuzi


BAADA ya Mtibwa Sugar kupata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Azam, Kocha Mecky Maxime amemlaumu mwamuzi wa mchezo huo akidai aliwabeba wapinzani wao.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi juzi, bao pekee la Azam lilifungwa na John Bocco.
Akizungumza baada ya mchezo huo Maxime alisema mwamuzi Ngole Mwangole ambaye alikuwa akichezesha mchezo huo alikuwa akitafuta namna ya kuipa ushindi Azam.
“Ukiangalia kwa mfano faulo iliyotolewa kwa Azam na Mwangole haikuwa ya haki, wanadai Bocco alitendewa madhambi na Salim Mbonde katika eneo la hatari, lakini ukiangalia halikuwa kosa,” alisema.
Alisema kikosi chake kilicheza vizuri mechi hiyo isipokuwa mchezo uliharibiwa na mwamuzi huyo na kuvuruga baada ya kupata kipigo hicho. Maxime alisema mara nyingi waamuzi wamekuwa wakiharibu mpira hata kama timu imeanza vizuri.
“Timu zote zilicheza vizuri inavyotakiwa lakini refa tu aliharibu mpira, alikuwa anatafuta kitu na ndio alichokifanya kwa sababu mchezaji wangu ndio alianza kushikwa,” alisema.
Alieleza kuwa waamuzi imekuwa tatizo la muda mrefu na wanachangia kuua soka nchini kutokana na kufanya makosa yanayojirudia bila kuchukuliwa hatua yoyote.
Alisema halalamiki kwa kuwa amefungwa kwani ni sehemu ya mchezo isipokuwa afungwe kihalali.

Hakuna maoni: