ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 1 Januari 2016

Wasomi wapongeza makatibu wakuu

  Imeandikwa na Waandishi Wetu
WAKATI makatibu wakuu wateule na manaibu wao wanaapishwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam, baadhi ya wasomi wamesema uteuzi wao ambao ameufanya Rais John Magufuli unalenga kuisaidia nchi iweze kuingia kwenye uchumi wa Viwanda.
Profesa Emrod Elisante wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) alisema kwamba uteuzi huo ni mzuri kwani umezingatia utaalamu zaidi. Alisema lazima wizara ziwe na wasimamizi madhubuti ambao wataisaidia nchi kuwa yenye viwanda.
“Nikiwaangalia watu kama Dk Chamriho (Leonard, Katibu mkuu Uchukuzi) Profesa Mkenda (Adolf, Katibu mkuu katibu Mkuu Biashara na Uwekezaji) hawa ni watu makini na ni watendaji wazuri naamini wataisaidia nchi,” alisema.
Alisema iwapo watapewa malengo na rais, wana uwezo wa kuyatekeleza hasa kuifanya Tanzania iwe sekta ya viwanda kama alivyoahidi Rais Magufuli wakati wa kampeni.
Profesa Elisante alisema licha ya nchi kuwa na changamoto mbalimbali kama za kifedha na rasilimaliwatu, lakini alisema uteuzi huo umejaa wataalamu ambao wengi wamepelekwa kwenye fani zao.
“Unajua hata waliopita ni wazuri, ila tatizo waliingia kwenye siasa, Rais Magufuli akiweza kuwadhibiti hawa wasiingie kwenye siasa na wakafanya kazi yao kwa weledi na kujua malengo ya wizara na nchi naamini tutachomoka,” alisema.
Naye Mwanaharakati za haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa alisifu uteuzi wa makatibu wakuu hao kwa maelezo kuwa umewapeleka watu katika fani walizosomea.
“Mfano Profesa Mchome (Sifuni ambaye ni Katibu mkuu wizara ya katiba na sheria) yule ni mwanasheria aliyebobea naamini ataisaidia nchi kwa kutumia taaluma yake,” alisema Olengurumwa.
Alisema kitendo cha Rais Magufuli kujaza wataalamu kama maprofesa na madaktari katika Serikali yake kunaonesha kuwa anathamini wataalam hao na angependa kuona wanatumia taaluma yao kuisaidia nchi.
“Utakuta katika wizara kwa mfano ya Madini, kuanzia Waziri hadi makatibu wakuu ni profesa na daktari, wakikaa pamoja wanaweza kufanya vizuri lakini pia wanaweza kufanya vibaya,” alisema Olengurumwa.
Alisema dhamira ya rais ni nzuri, hata hivyo alikosoa wingi wa makatibu wakuu hao hasa uteuzi wa manaibu makatibu wakuu kuwa haukuwa na maana kwani kila kitengo na idara kina mkurugenzi ambaye kama katibu mkuu hayupo anaweza kufanya kazi zake.
“Alipunguza baraza la mawaziri tukafurahi, lakini amerudi nyuma kwa kuleta makatibu wakuu wengi tofauti na alivyotangaza kuwa makatibu wakuu pia wangepungua, kwa hiyo tuko kule kule,” alisema Olengurumwa.
Naye Katibu Mkuu mteule wa Afya katika wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya amesema ameupokea uteuzi wake kwa mshituko mkubwa kwa kuwa ni jambo ambalo hakuwahi kulifikilia.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake ya Ukurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dk Ulisubisya alisema uteuzi wake umekuja kwa ghafla huku akiwa na mipango aliyokuwa amejiwekea ya kuendeleza hospitali hiyo.
Alisema mawazo yake yote ilikuwa ni kujipanga kuhakikisha anatekeleza majukumu aliyokuwa ameachiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii majuma mawili yaliyopita, Dk Donan Mbando aliyefanya ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo.
Dk Ulisubisya alisema agizo lingine lilikuwa kuhakikisha hospitali hiyo inaanzisha Chuo Kikuu kwa ajili ya kuongezea taaluma kwa madaktari na kuboresha huduma za dharura na kupunguza foleni kwa wagonjwa, mambo ambayo tayari alianza kuyafanyia kazi na kuyawekea mikakati.
Wakati huo huo, leo Rais Magufuli anawaapisha makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu wa wizara mbalimbali aliowateua juzi. Kazi ya kuwaapisha inafanywa leo Ikulu na kwa hatua hiyo, Rais atakuwa amekamilisha kazi ya kupata watendaji wa ngazi za juu katika wizara mbalimbali, ambazo ni moja ya vyombo vinavyotegemewa kuleta maendeleo ya watanzania ikiwa kila mmoja kwa nafasi yake, atatimiza wajibu wake. Imeandikwa na Shadrack Sagati, Dar na Joachim Nyambo, Mbeya.

Hakuna maoni: