ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 9 Januari 2016

Magufuli ampa 5 Samatta

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amemtumia salamu za pongezi mshambuliaji wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Samatta kwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.
Magufuli alituma salam hizo jana kupitia Wizara ya Habari, Michezo, Utamaduni na Sanaa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari, Dk Magufuli alimtumia salamu za pongezi Waziri wa Wizara hiyo, Nape Nnauye afikishe salamu zake za pongezi kwa Samatta.
“Rais Magufuli amemtaka Waziri Nnauye amfikishie salamu zake za pongezi kwa mchezaji huyo, ambaye pia anaichezea TP Mazembe,” imesema taarifa hiyo ikiongeza kuwa tuzo hiyo imejenga heshima kwa Samatta na Tanzania.
Katika taarifa hiyo, Magufuli amewasihi wachezaji wa soka wote na wadau wa mchezo huo kuongeza juhudi kuuendeleza mchezo ili upige hatua zaidi kimaendeleo. Samatta alitwaa tuzo ya mchezaji bora juzi usiku iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) katika sherehe zilizofanyika Abuja, Nigeria.
Mchezaji huyo alikuwa akipambana na wachezaji wengine wawili ambao ni Robert Kidiaba Muteba (wa TP Mazembe na Congo) na Baghdad Bounedjah (Algeria & Etoile du Sahel).
Samatta alipata pointi 127, mbele ya mchezaji mwenzake wa TP Mazembe, kipa Kidiaba wa DRC aliyepata pointi 88, wakati mshambuliaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia na timu ya taifa ya Algeria, Bounedjah alipata pointi 63.
Mchezaji huyo wa Tanzania ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Afrika Mashariki kushinda tuzo kubwa ya Afrika. Mafanikio hayo yamekuja baada ya kuiwezesha Mazembe kutwaa taji la tano la Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake manane.
Mshambuliaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa mara ya kwanza na kumshinda Yaya Toure wa Man City na Ivory Coast aliyekuwa akisaka tuzo hiyo kwa mara ya tano.
Aubameyang wa Borussia Dortmund ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 26, amewaangusha Toure aliyekuwa anashikilia tuzo hiyo na Andre Ayew wa Ghana. Amekusanya pointi 143, saba zaidi ya Toure wakati Ayew ameshika nafasi ya tatu kwa kupata pointi 112.
Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametoa pia pongezi zake kwa mchezaji huyo. Naye, Kocha wa Yanga, Hans Pluijm amempongeza Samatta kwa tuzo hiyo akisema kuwa, itawatia moyo wachezaji wengine wa ndani wa Tanzania kubadilika katika mtizamo wa kucheza soka la kulipwa.
“Tuzo hiyo itawafanya wachezaji wengine wa Tanzania kucheza katika kiwango cha juu sio tu katika kujipandisha wao wenyewe, bali kuisaidia timu ya taifa hasa katika mashindano ya kimataifa,” alisema.

Hakuna maoni: