Imesisitizwa, awamu hii ya ubomoaji, itajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu na watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma, zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo, hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga.
Maamuzi hayo yamefikiwa juzi baada ya mawaziri watatu wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI); Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.
Mawaziri hao walifanya mkutano wa kutathmini uhamishaji wa wakazi wa mabondeni katika jiji la Dar es Salaam. Waliamua kuwa watumishi wa umma waliowamilikisha wakazi maeneo hayo, watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
Taarifa ya maamuzi hayo ilitolewa jana na Ofisi ya Makamu wa Rais. Pia, taarifa hiyo ilisema mawaziri hao wameamua katika siku tatu zijazo, serikali itaanza kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji umefanyika.
Mawaziri hao walibainisha kuwa serikali itaheshimu amri za mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi wa mabondeni, lakini pia itafuatilia kesi hizo ziishe haraka ili taratibu zinazofuata zifanyike.
“Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake wanaoendesha zoezi hili kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa, na kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwemo wanaoweka alama za X zaidi ya mita zilizowekwa kisheria,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali imeanzisha dawati la malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupokea malalamiko au maswali kuhusu zoezi hilo.
Walisema nyumba na majengo yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa kwa sheria zinazotekelezwa katika ubomoaji huo hayatabomolewa, isipokuwa tu pale maisha ya wakazi yapo hatarini.
Vile vile ilisema wanaoishi katika makazi hayo, watapewa miongozo ya hatua za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa, kwani serikali haina dhamira ya kubomoa hoteli kubwa za siku nyingi zilizo karibu na fukwe katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa hoteli hizo, watapewa masharti na miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria.
Pia, serikali inaweka utaratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi zake ili hatua za utekelezaji wa sheria za nchi, zisiwe chanzo cha taharuki katika jamii. “Serikali haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi.
Lakini, pia haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yapo hatarini,” ilisisitiza taarifa hiyo. Itakumbukwa kwamba katika mafuriko ya mwaka 2011, wananchi 49 waishio mabondeni walipoteza maisha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya Hewa, mwaka huu zinatarajiwa kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea miaka ya hivi karibuni. Tathmini ya ubomoaji huo iliyotolewa ripoti kwa mawaziri hao, ilieleza kuwa hadi sasa wananchi katika nyumba 774 wamehama na nyumba hizo kubomolewa.
Taarifa hiyo ilieleza pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa kuhama, uhakiki kuhusu uhalali wa makazi anayoishi hufanywa. Kutokana na uhakiki huo, jumla ya wakazi 20 walikuwa na hati halali za makazi na wakazi 119 walikuwa na leseni za makazi za muda mfupi, hivyo hawakuhamishwa.
Nchi ina kingo za mito na mabonde na maeneo mengi hatarishi, ambamo watu wanaishi kinyume cha sheria, huku wakiharibu mazingira na kuhatarisha maisha yao, lakini kutokana na uhaba wa makazi, hali ni mbaya zaidi katika mabonde ya jiji la Dar es Salaam, hasa bonde la Mto Msimbazi.
Taarifa hiyo ilisema sababu za kufanya usafishaji wa mabonde na mito katika jiji la Dar es Salaam na mazingira yanayozunguka, unalenga kunusuru maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Eneo la Bonde la Mto Msimbazi, lilitangazwa ni eneo hatarishi kuishi binadamu tangu mwaka 1949 na baadaye 1979, hivyo usafishaji huo utapanua uwezo wa mito ya Dar es Salaam kupitisha maji ya mvua kwa kasi kubwa na kupunguza uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa wakati wa mvua nyingi.
Taarifa hiyo ilisema kabla ya nyumba kubomolewa, taasisi zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba anayokaa mkazi ina nyaraka za umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo nyaraka hizo zina uhalali wowote.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo nyumba ambazo zimethibitika kuwepo katika maeneo yasiyostahili, ndizo zinawekwa alama X kuashiria kwamba wakazi wanapaswa kuhama au kubomolewa, baada ya hapo mkazi hupewa muda wa kubomoa na kuhama mwenyewe.
“Kutokana na utaratibu huu, sehemu kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa wenyewe, baada ya hapo alama huwekwa kuonesha mpaka wa bonde,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Pia, taarifa hiyo ilieleza kwamba imebainika sehemu kubwa ya wakazi wa mabondeni ni wapangaji huku wamiliki wanakaa sehemu nyingine salama. Suala la Mchungaji Rwakatare Taarifa ya mawaziri hao pia ilieleza kuhusu suala la Mchungaji Getrude Rwakatare.
Ilisema mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) amefukuzwa kazi Januari 6 mwaka huu na taarifa zake zimekwishafikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutokana na tuhuma za kufanya udanganyifu kwa niaba ya Baraza, kwa lengo la kumlinda Mchungaji huyo wa kiroho.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais imeshafungua upya kesi mahakamani kuanzia Desemba 29 mwaka jana, kuomba “makubaliano” kati ya mwanasheria huyo wa NEMC na Mchungaji Rwakatare, yawekwe pembeni kwa sababu yalipatikana kwa njia ya udanganyifu.
Taarifa hiyo ilisema Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake mahali ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya mikoko, kinyume na sheria tatu muhimu.
Ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza, jitihada za kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za serikali za mitaa, lakini ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali. NEMC ilipoingilia kati na kutaka kubomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani na wakati kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, Mei 11 mwaka jana aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali kwa niaba ya Baraza, kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
Ilielezwa kuwa makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu Mei 13 mwaka jana, kisha Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba mwaka jana, yalipogundulika na mtumishi mwingine wa Baraza.
Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (DART) Taarifa hiyo ilisema mkutano wa mawaziri hao, ulielezwa kwamba Sheria ya Mazingira Kifungu 57 (2) inatoa nafasi ya kutolewa ruhusa kwa miradi au shughuli zenye maslahi ya taifa kufanyika katika maeneo ya mabondeni.
Hivyo, waziri mwenye dhamana ya mazingira anaruhusiwa kutoa miongozo ya namna ya shughuli hizo, zinavyoweza kufanyika bila kuathiri mazingira. “Mradi wa DART ulipata kibali hicho na una mkataba na Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya mazingira, zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mawaziri walitaka kufahamu hayo kutokana na hoja inayozungumzwa kwamba wananchi wanaondolewa katika maeneo ya kuishi mabondeni, lakini mradi wa DART umeachwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni