Hatua hiyo ilitokana na mwongozo uliotolewa kwa nyakati tofauti na wabunge; Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT Wazalendo) na wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).
Wabunge hao walisema Waziri amewasilisha hoja kinyume na kanuni za kudumu za Bunge, zinazosema katika mkutano wa bunge wa kila Oktoba na Novemba, Serikali inatakiwa kuwasilisha mpango wa maendeleo wa taifa wa kila mwaka.
“Kutokana na maelezo uliotoa (Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge) na kwa kutumia kanuni ya hamsini na nane, tano ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la 2016, naomba ruhusu kuondoa hoja niliyoiwasilisha leo (jana) asubuhi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha miaka mitano 2016/17 mpaka 2020/21,” alisema Dk Mpango.
Hoja hiyo iliondolewa baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Chenge kutoa mwongozo na kisha kuahirisha Bunge hadi kesho kutwa. Awali katika maelezo yao bungeni na nje ya Bunge, wakati wakizungumza na waandishi wa habari, Zitto na Lissu walisema uwasilishwaji wa hoja ya Waziri Mpango, umekiuka Katiba. Hata hivyo akitoa mwongozo, Chenge alisema suala hilo halikukiuka katiba.
“Nimelitafakari sana jambo hili, na baada ya kutafakari hakuna ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.” Alisema kilicholetwa na serikali ni mchakato wa kushirikisha wawakilishi wa Tanzania ili watoe maoni, ushauri na mapendekezo yao kuhusu na mpango unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2020/16/17.
Alisema kitu ambacho wabunge lazima wakubali, ni kwamba kulingana na Kanuni ya 94 (1), Bunge linapofanya kazi hiyo huwa haliketi kama Bunge, bali linaketi kama kamati ya mipango. “Hiyo ni dosari ambayo tumeiona,” alisema na kukiri kwamba hapa ilikuwa ni mpango wa muda mfupi.
Hata hivyo alisema Ibara ya 63 haisemi ni lini huo mpango uletwe. Alikiri kuwa mpango mfupi unatokana na wa mwaka mitano, ambao hitimisho lake ni pale waziri atakaposoma mpango wa serikali kwa mwaka unaofuata wa fedha na jioni yake, Waziri anaposoma bajeti ya serikali.
Akihimiza kuwa Kanuni ya 94 (1) lazima izingatiwe, Chenge alisema, “Bunge halikuweza kukutana Oktoba na Novemba kama kanuni hiyo inavyotaka kwa sababu kulikuwa na shughuli kubwa ya uchaguzi.
Alisema Serikali na Bunge hawakuwa na njia nyingine, jambo ambalo ilikuwa lazima mchakato ufanyike sasa ili Machi 11, serikali iwasilishe mbele ya wabunge kama ilivyofanyika mwaka jana katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam.
“Waziri mwenye dhamana anawasilisha mipango na ukomo wa bajeti. Wakishawasilisha, katibu wa bunge ndiye anapeleka kwa spika ili aelekeze ipelekwe kwenye kamati ya bajeti hadi watakapokuja kutoa taarifa,” alisema.
Kwa mujibu wa kanuni, siku ya kusoma bajeti ya serikali, waziri anawasilisha hoja yake ya mpango; utekelezaji wa hali ya mwaka jana na mwaka unaofuata. Hivyo kunakuwa na hoja mbili ambazo hujadiliwa kwa pamoja; hoja ya mpango na ya bajeti ya serikali.
“Haya ndiyo yanapaswa yafanyike,” alisema na kusihi wabunge kuelewa kanuni. Baada ya maelezo hayo, Chenge alimuita Waziri mtoa hoja; Waziri wa Fedha, aombe idhini ya Bunge ya kuondoa hoja. Kabla ya kutoa hoja hiyo, wabunge walihojiwa, na wote waliridhia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni