ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumapili, 13 Machi 2016

Breaking News: Rais Magufuli Afanya Uteuzi wa Wakuu wa Mikoa 26....Kati Yao 13 ni Wapya, 7 Wamebakizwa na 5 Wamehamishwa

Kikoti blog

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa wakuu wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara, ambapo kati yao 13 ni wapya, 7 wamebakizwa katika vituo vyao vya kazi, 5 wamehamishwa vituo vya kazi na 1 amepangiwa Mkoa Mpya wa Songwe.
Uteuzi huo umetangazwa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe leo tarehe 13 Machi, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam.
 
Wakuu wa Mikoa walioteuliwa ni kama ifuatavyo;
  1. Mh. Paul Makonda - Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.
  2. Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Elias Kyunga - Mkuu wa Mkoa wa Geita.
  3. Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu - Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
  4. Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga - Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
  5. Brigedia Jeneral Mstaafu Emmanuel Maganga - Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
  6. Mh. Godfrey Zambi - Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
  7. Dkt. Steven Kebwe - Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
  8. Kamishna Mstaafu wa Polisi Zerote Steven - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
  9. Mh. Anna Malecela Kilango - Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
  10. Mhandisi Methew Mtigumwe - Mkuu wa Mkoa wa Singida.
  11. Mh. Antony Mataka - Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
  12. Mh. Aggrey Mwanri - Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
  13. Mh. Martine Shigela - Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
  14. Mh. Jordan Mungire Rugimbana - Mkuu wa Mkoa Dodoma.
  15. Mh. Said Meck Sadick - Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.
  16. Mh. Magesa Mulongo - Mkuu wa Mkoa Mara.
  17. Mh. Amos Gabriel Makalla - Mkuu wa Mkoa Mbeya.
  18. Mh. John Vianey Mongella - Mkuu wa Mkoa Mwanza.
  19. Mh. Daudi Felix Ntibenda - Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
  20. Mh. Amina Juma Masenza - Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
  21. Mh. Joel Nkaya Bendera - Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
  22. Mh. Halima Omary Dendegu - Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
  23. Dkt. Rehema Nchimbi - Mkuu wa Mkoa wa Njombe.
  24. Mhandisi Evarist Ndikilo - Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
  25. Mh. Said Thabit Mwambungu - Mkuu wa Mkoa Ruvuma.
  26. Luteni Mstaafu Chiku Galawa - Mkuu wa Mkoa wa Songwe (Mkoa mpya).
Wakuu wote wa Mikoa walioteuliwa, wataapishwa Jumanne tarehe 15 Machi, 2016 saa 3:30 Asubuhi Ikulu, Jijini Dar es salaam.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
13 Machi, 2016

Jumamosi, 12 Machi 2016

Vita ya ukatibu mkuu Chadema

freeman-mbowe-chadema
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, yupo katika wakati mgumu kutokana na wajumbe wa Baraza Kuu na wabunge wenye ushawishi kumtaka amteue Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Hii inakuwa mara ya kwanza kutokea katika historia ya kuasisiwa kwa chama hicho kikuu cha upinzani kwa wajumbe wa Baraza Kuu kumshawishi Mwenyekiti kumteua mtu anayefaa kushika wadhifa huo.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu, linalotarajiwa kuketi leo wanaotajwa kujipanga kumshawishi Mwenyekiti kumteua Sumaye kuwa Katibu Mkuu ni Profesa Mwesiga Baregu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na Mbunge wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa.
Wengine ni pamoja na Makamu Mwenyekiti Bara, Profesa Abdallah Safari, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa, Anthony Komu na  Benson Kigaila na Katibu Mkuu Baraza la Wanawake (Bawacha), Grace Tendega.
Katika orodha hiyo pia wamo wabunge wenye ushawishi mkubwa ambao ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.
Katika orodha hiyo yumo Mbunge wa zamani wa Ilemela, Ezekia Wenje na baadhi ya waliokuwa wagombea ubunge wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama.
Hadi jana Profesa Safari hakuwa amehudhuria vikao vya Mwanza kutokana na kile kilichoelezwa kukabiliwa na matatizo mbalimbali.
Juzi Lissu aliweka wazi sifa za kiongozi aliyekuwa akimtaka, jambo ambalo lilitafsiriwa na wachambuzi wa mambo kwamba alikuwa akimuelezea Sumaye.
Naye mmoja wa wajumbe ambaye hakupenda jina lake litajwe anayemuunga mkono Sumaye ashike nafasi ya Katibu Mkuu, alisema ukiondoa sifa alizotaja Lissu za kumtaka Katibu Mkuu anayeweza kuzungumza na Watanzania, vyama vya Ukawa, ndani na nje ya nchi wakamsikiliza, nyingine ni mtu aliyeingia Chadema kwa kutofuata cheo.
“Hakuna mwingine zaidi ya Sumaye, ambaye alijiunga na chama hiki wakati ambao nafasi nyingi zilikuwa zimeshanyakuliwa na wanachama wengine,” alisema mjumbe huyo.
Sababu kubwa ya wajumbe kumtaka Sumaye inaelezwa kutokana na kubaini kuwepo kwa mpango wa Mwenyekiti, Mbowe kumtaka Salum Mwalimu, anayekaimu nafasi hiyo.

Majipu tisa yaliyoiva Dawasco yatumbuka

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge amewasimamisha kazi kupisha uchunguzi vigogo tisa wa Kampuni ya Maji Safi na Taka (Dawasco) na kutaka aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Jackson Midala kusakwa na kuchunguzwa na ikibainika alihusika kwenye ubadhirifu wa maji, afikishwe mahakamani.
Kadhalika,Waziri Lwenge ameitaka Bodi ya Dawasco, kuchunguza tuhuma za wizi wa maji zinazofanywa na baadhi ya watendaji wa kampuni hiyo kwa kuwaunganishia maji bure kampuni na viwanda kadhaa jijini Dar es Salaam na kulipwa ujira kila mwisho wa mwezi na viwanda hivyo.
Waziri Lwenge alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Dawasco kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe, kuona utendaji wao na kuzungumza na watumishi hao.
Pia ameitaka bodi hiyo kuchunguza Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na kampuni nyingine pamoja na viwanda jijini Dar es Salaam kama wana akaunti za maji ya Dawasco na kwamba madai ya kuwa wao wana visima vyao vya maji, lazima ukweli upatikane.
Alisema kama kampuni inasema ina visima vyake binafsi vya maji, ni lazima wawe na kibali walichopata kutoka Wizara ya Maji, kinachowaruhusu wao kuchimba na kinaonesha kiwango cha maji, na kwamba kuna madai mengi ya kampuni na viwanda kuwa na visima vyao, ila wizara haifahamu.
“Kama unadai una kisima cha maji cha kwako kibali kinatolewa na wizara yangu, sasa yapo madai mengi viwanda vinasema vinatumia maji yao, ila zipo taarifa kwamba wanajificha kwenye hilo na ukweli ni kwamba wanaiba maji ya Dawasco, sasa lazima mchunguze hayo,” alisema Lwenge.
Waliosimamishwa kazi ni Meneja Rasilimali Watu, Mvano Mandawa, Meneja Ufuatiliaji na Tathmini, Reinary Kapera, Teresia Mlengu, Emmanuel Guluba, Peter Chacha, Fred Mapunda, Reginald Kessy, Jumanne Ngelela na Bernard Nkenda.
“Sehemu kubwa ya upotevu wa maji ni wizi unaofanywa na wezi ambao ni baadhi ya viwanda na kampuni kubwa kwa kushirikiana na watendaji wa Dawasco, tuna taarifa na kila mwisho wa mwezi wako kwenye ‘payroll’ wanaenda kuchukua malipo, hawa ni majipu lazima yatumbuliwe,” alisema Waziri Lwenge.
Mara baada ya kusomewa taarifa fupi ya utendaji kazi wa Kampuni hiyo kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja, Waziri Lwenge alitoa maagizo hayo na kusema pamoja na Kampuni kuwa na malengo mazuri, lakini ni lazima ifanyiwe mabadiliko ili kupata watendaji waadilifu.
Alisema upotevu wa maji hivi sasa ni asilimia 47 na kwamba maji hayo yanapotea katika mazingira tatanishi na kuikosesha kampuni hiyo mapato. Strabag Alitoa mfano mzuri wa Kampuni ya Ujenzi wa Barabara ya Strabag, ambayo ilipewa zabuni ya kujenga barabara za mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), kwamba tangu kampuni hiyo ianze kufanya kazi hadi sasa, haijalipa Dawasco bili ya maji iliyotumia.
“Strabag walifanya wizi wa maji, wamejenga barabara lakini hakuna malipo yoyote waliyofanyika Dawasco, wanadaiwa zaidi ya Sh bilioni 2.9 pamoja na faini na natoa siku 14, wawe wamelipa vinginevyo wakamatwe wafikishwe mahakamani.
Waziri Lwenge alisema Serikali haiwezi kufanya kazi na wabadhirifu ambao wako ndani ya taasisi, kampuni au mashirika yake na kusisitiza kuwa ni lazima watendaji wasio waaminifu waondolewe ili kuleta ufanisi nchini.
“Tunafanya mageuzi ili tufanye kazi kwa ufanisi na lazima tuwe na watendaji waadilifu na wenye maadili, si wanaoangalia maslahi binafsi,” alisema Lwenge. Waziri Lwenge alitoa wiki mbili kwa bodi hiyo kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo na zile za wateja wakubwa wa Dawasco kutokuwa na akaunti za maji, ili kuthibitisha ukweli wa madai hayo.
Maagizo mengine ni kuitaka Dawasco ifikapo Juni, mwaka huu kuhakikisha wamefanikiwa kupunguza upotevu wa maji kwa asilimia 30 na ifikapo 2020 upotevu huo uwe chini ya asilimia 20.
Awali Ofisa Mtendaji wa Dawasco, Luhemeja alisema changamoto kubwa ya Dawasco ni upotevu wa maji na kubainisha katika maeneo 10 wanayohudumia maji Dar es Salaam na Pwani, Magomeni ni eneo korofi kwa wizi wa maji.
Alisema eneo hilo hivi sasa limebainishwa na wameweka mtandao ambao kuanzia mwisho wa mwezi huu, utabaini wezi wote lakini pia hatua nyingine walizochukua ni kuweka vituo vya kuuza maji kwenye eneo korofi, vinavyosimamiwa na jamii ya eneo husika.
Alisema kwa miezi kadhaa sasa, tangu kuanza kwa huduma hiyo wameweka vituo 47 vya kuuza ambavyo vimefungiwa mita na wauzaji hutakiwa kulipa Dawasco bili ya maji baada ya kuwauzia wateja wadogo wadogo.
Ofisa Mtendaji huyo mpya wa Dawasco, alisema kwa kipindi cha muda mfupi tangu aingie kwenye kampuni hiyo, wamefanikiwa kuongeza mapato ya maji kutoka Sh bilioni 2.9 mwaka jana hadi kufika Sh bilioni 7.1 Januari mwaka huu.
Aliongeza kwamba lengo lao ifikapo Juni mwaka huu, ni kukusanya Sh bilioni 12 kwa mwezi na hiyo ni kutokana na kuweka mifumo imara na dhabiti ya kufuatilia mita za maji na masharti waliyopewa mameneja wa maeneo husika ya kampuni hiyo.
Dawasco hivi sasa ina wateja waliounganishiwa mita zaidi ya 151,000 na lengo lao ni kuongeza idadi ya wateja baada ya kuongeza uzalishaji na usambazaji wa maji hasa baada ya kuimarika kwa mitambo miwili ya maji ya Ruvu Chini na Juu.

Alhamisi, 10 Machi 2016

Simba leo tena

TIMU ya soka ya Simba na Mbeya City leo zinashuka dimbani kwenye viwanja viwili tofauti kusaka pointi tatu muhimu katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu bara. Simba itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam wakati Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Stand United kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.
Wekundu hao wa Msimbazi huenda wakapanda kileleni tena iwapo watafanikiwa kuwafunga Ndanda Fc katika mchezo huo kwa kuwa watafikisha pointi 51 na kuishusha Yanga yenye pointi 50.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Simba ilikaa kileleni kwa siku mbili kabla ya Yanga juzi kupanda na kumpiku kufuatia ushindi wake wa mabao 5-0 dhidi ya African Sports ya Tanga. Simba, Yanga na Azam FC zinatofautiana kwa pointi chache kiasi kwamba mmoja akishinda, mwingine anashuka.
Simba ina uwezekano wa kushinda mchezo wa Ndanda, kwani katika mchezo wake wa raundi ya kwanza ilishinda bao 1-0 ugenini mjini Mtwara. Hali itakuwa mbaya kwa Ndanda kama itakubali kichapo kwa mara nyingine kwani licha ya kuwa katika nafasi ya nane, ina pointi 24 ambazo hazitoshi kuihakikishia kubaki salama kwenye msimamo wa ligi kwa kuwa timu zilizoko chini yake zinaweza kupanda kutokana na kutofautiana pointi chache.
Kwa upande wa Mbeya City, huenda ikafanya vizuri leo baada ya kuonesha kiwango bora chenye mabadiliko katika mchezo dhidi ya Simba wiki iliyopita. Licha ya kufungwa mchezo huo, walicheza vizuri isipokuwa inayumbushwa na ubutu wa safu yake ya ushambuliaji.
Pengine kwa vile inacheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wanaweza kutumia faida hiyo katika kufanya vizuri na kufuta machungu ya kufungwa na timu hiyo ya Shinyanga bao 1-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza.

APR, Yanga watambiana

HOMA ya pambano la raundi ya kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na APR ya Rwanda, imezidi kupanda, kiasi cha kila moja kutamba kumshikisha adabu mpinzani wake.
Tayari makocha wa klabu hizo, Hans van der Pluijm wa Yanga na Nizar Khanfir wa APR aliyeweka rekodi ya kuwa mwarabu wa kwanza kufundisha soka Rwanda baada ya kuanza kazi rasmi jana, ameelezea utayari wake kushinda mechi ya Jumamosi wiki hii huko Kigali, Rwanda.
Khanfir amekaririwa jana kuwa, ameshawaona Yanga kupitia video mbalimbali na kwamba anataka kuwafunga Jumamosi. “Lengo letu ni kushinda huo mchezo,”amesema na kuongeza; “Nimeona baadhi ya video zao na tutaendelea kuwachambua katika siku chache zijazo kuelekea kwenye mechi”.
Kwa ujumla, Khanfir amesema malengo yake makuu katika miezi sita ya mwanzo ni kuiwezesha timu kutetea ubingwa wa Rwanda na pia kuifikisha mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Mtaalamu huyo wa Tunisia aliongoza mazoezi yake ya kwanza APR jana Uwanja wa Kicukiro akisaidiwa na kocha aliyemkuta kazini, Emmanuel Rubona.
“APR ni timu kubwa Rwanda na ina heshima kubwa Afrika na pia ina wachezaji wengi katika timu ya taifa, ambacho ndicho kilichonivutia mimi kukubali kazi hii,” amesema Khanfir. “Wachezaji ni vijana wadogo na timu ina uwiano mzuri ambao unafaa vizuri katika falsafa yangu. Tunaitaka kuipeleka timu katika kiwango kingine.
Ni wajuzi na tunataka kuongeza ufundi zaidi, lakini zaidi ya hapo nimevutiwa na timu kwa ujumla,” amesema. Wakati Khanfir akisema hayo, Pluijm kwa upande wake amesema anatambua wanakwenda Kigali kwenye mchezo mgumu wa ugenini dhidi ya APR, lakini watapambana wasipoteze.
“APR ni timu nzuri na watakuwa wamejiandaa vizuri, lakini sisi tuko vizuri, tutakwenda kupambana tusipoteze mchezo, ili tumalizie vizuri mchezo wa nyumbani,”amesema. Yanga SC inatarajiwa kuondoka leo nchini kwenda Kigali kwa ajili ya mchezo huo, unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezeshwa na marefa wa Malawi Jumamosi Uwanja wa Amahoro, Kigali Rwanda. Duncan Lengani anatarajiwa kupuliza filimbi, wakati washika vibendera watakuwa Clemence Kanduku na Jonizio Luwizi.
Mchezo wa marudiano wiki moja baadaye Dar es Salaam, utachezeshwa na marefa wa Shelisheli; katikati Bernard Camille na pemebeni watakuwapo Eldrick Adelaide na Gerard Pool.
Mchezo wa kwanza utafanyika mjini Kigali, Rwanda Machi 12 kabla ya timu hizo kurudiana Dar es Salaam Machi 19 na mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa mchezo mwingine wa raundi ya kwanza, kati ya Al Ahly ya Misri na Recreativo de Libolo ya Angola mwezi ujao.

St Joseph watakiwa kurudi darasani

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ameingilia kati mgogoro wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Joseph Dar es Salaam, waliogomea kufanya mitihani na kuwataka warejee madarasani wakati matatizo yao yakishughulikiwa.
Wanafunzi hao walikuwa katika siku ya tatu ya mgomo wao jana ambapo pamoja na mambo mengine walikuwa wakilalamikia mapungufu yaliyopo chuoni hapo, ikiwa ni pamoja na maabara za kufanyia mafunzo kwa vitendo, matatizo ya kiutawala, mitaala ya kufundishia pamoja na ada.
Profesa Ndalichako aliwasili chuoni hapo jana asubuhi na kukagua mazingira ya kufundishia ya chuo hicho kwa kutembelea maabara zote chuoni hapo na kisha kwenda kuzungumza na utawala, Serikali ya wanafunzi na mwisho alihutubia wanafunzi wote.
Ndalichako baada ya kuzungumza na pande zote mbili aliagiza wanafunzi hao warejee madarasani kuendelea na mitihani yao na kuutaka uongozi wa chuo uyafanyie marekebisho mapungufu ya kiutawala yaliyojitokeza.
Aidha ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), chini ya Katibu Mtendaji wake, Profesa Yunus Mgaya kufuatilia na kuchunguza kwa makini madai ya wanafunzi hao juu ya kuwepo kwa wahadhiri wasio na sifa zinazotakiwa.

Magufuli aitamani Vietnam

RAIS John Magufuli amesema anatamani mafanikio ya nchi ya Vietnam kiuchumi na kubainisha kuwa ziara ya Rais wa nchi hiyo, Truong Tang Sang nchini, ni fursa na changamoto kwa watanzania kujifunza mambo mengi, yatakayosaidia kukuza pia uchumi wa Tanzania.
Aidha amehamasisha Watanzania kuchangamkia fursa na rasilimali zilizopo nchini katika kujiinua na kuimarisha nchi yao kiuchumi. Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi tajiri kwa rasilimali na fursa nyingi, ingawa bado iko nyuma kimaendeleo. Kwa upande wake, Rais Sang amesema nchi yake na Tanzania zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya biashara, kilimo, viwanda na uvuvi lengo likiwa ni kuhakikisha nchi zote zinanufaika kwenye ushirikiano huo.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari na marais hao Ikulu Dar es Salaam jana, Dk John Magufuli alisema ni wakati sasa wa Tanzania kujifunza kutoka kwa nchi hiyo ya Vietnam ambayo pamoja na kukabiliwa na vita ya muda mrefu, imefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati. “Ukweli ni kwamba ziara ya Rais Sang nchini kwetu ni muhimu sana na imekuja kwa wakati muafaka.
Mwaka 1976 Rais wa Vietnam alikuja nchini na alichukua mbegu ya korosho na kuipeleka nchini kwake, na leo hii Vietnam ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kuzalisha korosho duniani,” alisema. Alitaja mafanikio mengine ya nchi hiyo ni pamoja na kuwa na uchumi wa kati, licha ya kukabiliwa na mapigano ya muda mrefu. Ilipata uhuru wake mwaka 1945 na ilidumu kwenye mapigano hadi Julai 2, mwaka 1976.
Alisema mwaka 1977 mapato ya kila raia wake yalikuwa ni dola 100, lakini sasa imefanikiwa kupandisha mapato hayo na sasa kila raia wa nchi hiyo mapato yake ni dola 2000 kwa mwaka na imepunguza kiwango cha umasikini kwa asilimia 50. “Sisi tangu mwaka 1960 bado tuko kwenye nchi masikini, kwa hiyo hii ni changamoto kwa nchi yetu. Tunatakiwa kujifunza kuondokana na hali hii.
Wao uzalishaji kwa mchele wanalima mara tatu kwa mwaka, sisi tunalima mara moja tu na inawezekana uzalishaji wetu ni mdogo sana,” alisema. Alisema nchi hiyo pamoja na kuchukua mbegu ya korosho nchini, ndio nchi inayoongoza kwa kuzalisha korosho duniani, wakati Tanzania ndio iliyotoa mbegu hiyo, zao hilo badala ya kuzalishwa kwa wingi ndio uzalishaji wake unafifia.
“Samaki sina uhakika kama walichukua huku, lakini leo hii Vietnam ni wazalishaji wa samaki wakubwa sana. Lakini kwa nchi yetu ambayo ina maziwa 21 na mito kila mahali na bahari lakini uzalishaji wa samaki uko chini…” “Tuna ng’ombe zaidi ya bilioni 22 hadi bilioni 23 nafikiri tunaweza kuwa wa pili barani Afrika baada ya Ethiopia, lakini ngozi zetu za viatu hapa tunaagiza nje.
Kwa hiyo kwa hili watanzania tunatakiwa tusiogope kujifunza kwa wale waliotutangulia ili na sisi nchi yetu iweze kufika mahali pazuri,” alisisitiza Dk Magufuli. Alisema ujio wa Rais Sang pamoja na ujumbe wake wa zaidi ya mawaziri takribani 20 na wafanyabiashara ni wakati pekee wa Watanzania na wa Vietnam, kuimarisha ushirikiano uliokuwepo kwa zaidi ya miaka 50 sasa kuhakikisha uhusiano unaleta maendeleo kwa pande zote.
“Ziara hii ni muafaka kwetu sisi watanzania kujenga uhusiano mzuri na nchi ya Vietnam ili kuweza kujifunza na sisi tuweze kufikia lengo letu la kuwa nchi ya kipato cha kati,” alisema. Pamoja na hayo, Rais Magufuli alisema katika mazungumzo yake na Rais wa Vietnam alipata mwaliko wa kutembelea nchi hiyo mwakani. “Kwa kweli mwaliko huu nimeupokea na ninajisikia kuthaminiwa na kuheshimiwa sana,” alisema.
Kwa upande wake, Rais Sang alisema anajisikia fahari kuona uhusiano kati ya Tanzania na nchi yake unaimarika. Alisisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaleta maendeleo ya dhati baina ya nchi hizo mbili. Alipongeza serikali kupambana dhidi ya umasikini kwa kusisitiza kuwa inafanya vizuri kiuchumi kwani ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.
“Kama rafiki wa karibu tunavutiwa na maendeleo yenu hasa katika kupambana na umasikini lakini pia ukuaji wa kasi wa uchumi wenu. Katika mazungumzo yetu na Rais Magufuli tumezungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kilimo, biashara na viwanda,” alisema rais huyo. Aidha, alisema uhusiano wa nchi hizo mbili ni wa muda mrefu, kwani pamoja na umbali wa kijiografia Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vietnam.
Alisema ziara hiyo ni moja ya njia za kudumisha na kuboresha zaidi uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili. Rais huyo alisema kwenye mazungumzo yake na Magufuli, wamekubaliana kushirikiana katika maeneo yatakayonufaisha nchi zote. Maeneo hayo ni kilimo, biashara, viwanda na mawasiliano. Pia walisaini mikataba ya kutowatoza kodi mara mbili wawekezaji na wafanyabiashara wanaowekeza katika nchi hizo.
Aidha Rais huyo alisema katika kikao chake na Rais Magufuli pamoja na mawaziri wa nchi zote mbili wamekubaliana kuanzisha tume ya pamoja itakayosimamia masuala ya uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili. Aidha marais hao walizungumzia masuala ya kimataifa ambapo wote kwa pamoja walikubaliana suala la kuhakikisha amani na utulivu linapewa kipaumbele na mataifa yote duniani.
“Tulikubaliana kuwa nchi zote zina wajibu wa kuhakikisha suala la amani linapewa kipaumbele, ikiwemo na mataifa ya kimataifa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha na kutuliza vurugu zinazoibuka katika nchi mbalimbali,” alisema. Alisisitiza kuwa amemwalika Rais Magufuli kutembelea Vietnam wakati wowote. Tayari Marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, walishafanya ziara katika nchi hiyo wakati wa utawala wao.
Rais Sang aliyeongozana na ujumbe wa watu 51 ataendelea kuwepo nchini kwa ajili ya kumalizia ziara yake katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kutembelea Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).