ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 10 Machi 2016

APR, Yanga watambiana

HOMA ya pambano la raundi ya kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na APR ya Rwanda, imezidi kupanda, kiasi cha kila moja kutamba kumshikisha adabu mpinzani wake.
Tayari makocha wa klabu hizo, Hans van der Pluijm wa Yanga na Nizar Khanfir wa APR aliyeweka rekodi ya kuwa mwarabu wa kwanza kufundisha soka Rwanda baada ya kuanza kazi rasmi jana, ameelezea utayari wake kushinda mechi ya Jumamosi wiki hii huko Kigali, Rwanda.
Khanfir amekaririwa jana kuwa, ameshawaona Yanga kupitia video mbalimbali na kwamba anataka kuwafunga Jumamosi. “Lengo letu ni kushinda huo mchezo,”amesema na kuongeza; “Nimeona baadhi ya video zao na tutaendelea kuwachambua katika siku chache zijazo kuelekea kwenye mechi”.
Kwa ujumla, Khanfir amesema malengo yake makuu katika miezi sita ya mwanzo ni kuiwezesha timu kutetea ubingwa wa Rwanda na pia kuifikisha mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Mtaalamu huyo wa Tunisia aliongoza mazoezi yake ya kwanza APR jana Uwanja wa Kicukiro akisaidiwa na kocha aliyemkuta kazini, Emmanuel Rubona.
“APR ni timu kubwa Rwanda na ina heshima kubwa Afrika na pia ina wachezaji wengi katika timu ya taifa, ambacho ndicho kilichonivutia mimi kukubali kazi hii,” amesema Khanfir. “Wachezaji ni vijana wadogo na timu ina uwiano mzuri ambao unafaa vizuri katika falsafa yangu. Tunaitaka kuipeleka timu katika kiwango kingine.
Ni wajuzi na tunataka kuongeza ufundi zaidi, lakini zaidi ya hapo nimevutiwa na timu kwa ujumla,” amesema. Wakati Khanfir akisema hayo, Pluijm kwa upande wake amesema anatambua wanakwenda Kigali kwenye mchezo mgumu wa ugenini dhidi ya APR, lakini watapambana wasipoteze.
“APR ni timu nzuri na watakuwa wamejiandaa vizuri, lakini sisi tuko vizuri, tutakwenda kupambana tusipoteze mchezo, ili tumalizie vizuri mchezo wa nyumbani,”amesema. Yanga SC inatarajiwa kuondoka leo nchini kwenda Kigali kwa ajili ya mchezo huo, unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezeshwa na marefa wa Malawi Jumamosi Uwanja wa Amahoro, Kigali Rwanda. Duncan Lengani anatarajiwa kupuliza filimbi, wakati washika vibendera watakuwa Clemence Kanduku na Jonizio Luwizi.
Mchezo wa marudiano wiki moja baadaye Dar es Salaam, utachezeshwa na marefa wa Shelisheli; katikati Bernard Camille na pemebeni watakuwapo Eldrick Adelaide na Gerard Pool.
Mchezo wa kwanza utafanyika mjini Kigali, Rwanda Machi 12 kabla ya timu hizo kurudiana Dar es Salaam Machi 19 na mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa mchezo mwingine wa raundi ya kwanza, kati ya Al Ahly ya Misri na Recreativo de Libolo ya Angola mwezi ujao.

Hakuna maoni: