ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 10 Juni 2016

Wasichana 500 kurejeshwa nchini

Imeandikwa na Hellen Mlacky
SERIKALI itawarudisha nchini Watanzania 500, waliokwama India baada ya kampuni zilizowachukua kwenda kuwatafutia kazi, kukiuka mikataba yao na kuwalazimisha kufanya kazi tofauti ikiwemo ukahaba.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga aliyasema hayo jana Dar es Saalam wakati akizungumzia matatizo wanayoyapata Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.
“Kati ya Machi hadi Mei 2016, balozi zetu nchini India na Malaysia zimepokea maombi ya kusaidia kuwarejesha nyumbani Watanzania ambao walipelekwa nchini India na Thailand kwa ahadi za kupatiwa ajira ambazo hutolewa na watu wasio waaminifu ambao wanashukiwa kujihusisha na mtandao wa biashara ya kusafirisha binadamu,” alisema Kasiga.
Alisema mtandao huo unawatafuta wasichana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 na hata chini ya umri huo na kuwalaghai kuwa kuna fursa za ajira katika hoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani nchi za nje na kuwawezesha kupata hati za kusafiria na tiketi ya ndege kwa ajili ya kusafiri kwenda kwenye nchi husika.
“Wengi huvutika kirahisi kwa kuona hiyo ni fursa ya kujipatia kipato ila kwa taarifa tulizopata ni kwamba wengi hujua mapema kuhusu kazi wanayoenda kuifanya huko ila ugumu wa maisha unapelekea kurubuniwa na kuingia kwenye matatizo makubwa,” alifafanua msemaji huyo.
Alisema nchini India peke yake, kuna Watanzania takribani 500 wengi wao wakiwa New Delhi (350), Bangalore (45), Mumbai (20) na wengine wanaelekea Goa. Alisema kwa upande wa Mashariki ya Kati, kumekuwa na wimbi kubwa la wasichana kurubuniwa kwa kutafutiwa fursa za kwenda katika nchi za Oman, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu hasa Dubai kufanya kazi za ndani.
“Baadhi ya wahanga wamekuwa wakikimbilia kwenye ofisi zetu za ubalozi kuomba msaada na balozi zimekuwa zikiwahifadhi ubalozini na kisha kuwasiliana na jamaa zao ili wawatumie nauli na kurejea nyumbani,” alisema.
Alisema wizara imekuwa ikipokea maombi kutoka ofisi za ubalozi nchi za Asia na Mashariki ya Kati ili kuwasaidia wasichana hao kurejea nchini, na hivi karibuni kutoka Ubalozi wa Oman kulikuwa na wasichana 18 kati yao 10 wamesaidiwa kurudi na kuunganishwa na familia zao na Ubalozi wa India wasichana 15 wamepeleka maombi yao.
Aliyataja matatizo yanayowakabili Watanzania nchi za Mashariki ya Kati na Asia kuwa ni pamoja na kulazimishwa ukahaba na kunyang’anywa hati za kusafiria ili kuwadhibiti wasitoroke na wengine kujikuta kukubali kufanya ukahaba ili kurejesha gharama za kuwasafirisha pamoja na kupata nauli.
Matatizo mengine ni kufanya kazi bila mikataba, kufanya kazi nyingi ambazo zingetakia kufanywa na zaidi ya watu wawili au watatu, kufanya kazi kwenye familia zaidi ya moja tofauti na makubaliano, kufanya kazi bila muda maalumu wa kupumzika, kunyanyaswa na kubaguliwa na kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kupigwa, kutopewa fursa ya kuwasiliana na mtu yeyote pamoja na kunyanyaswa kijinsia.
Alisema serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kutafuta majina ya wahusika wote wa mtandao huo na kufanya mawasiliano na serikali za nchi hizo ili kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika mkono wa sheria.

Mzee Mwinyi akunwa mabasi ya haraka

Imeandikwa na Anastazia Anyimike
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi jana alitembelea Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka na kusema licha ya kuchelewa kwa mradi huo ana imani utasaidia kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kumaliza safari yake katika kituo cha Kivukoni jana akitokea kituo cha Morocco na kwenda kituo cha Gerezani, Kariakoo na baadaye Kivukoni, Mwinyi aliyekuwa amefuatana na mkewe, Mama Sitti, alisema mradi huo utasaidia kupunguza foleni katika jiji na kwamba umeanza kuwaondolea wananchi adha ya kugombea usafiri wakati waendapo na warudipo katika shughuli zao.
Alisema licha ya mabasi hayo kugawana abiria na daladala na bodaboda, ana imani siku zijazo na utaratibu ukiwekwa vyombo vingine vya usafiri visiingie mjini ili mabasi hayo yawe huru kufanya kazi, tija zaidi itaonekana.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), Ronald Lwakatare alisema muda wowote ndani ya mwezi huu wananchi wataanza kutumia tiketi za kadi baada ya taratibu zote kukamilika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Usafirishaji ya UDA-RT, David Mgwasa alisema wananchi wameanza kuelewa juu ya matumizi ya mabasi na miundombinu yake, huku akisema tatizo linalowakabili kwa sasa ni mlundikano wa abiria wakati mmoja jambo ambalo linafanya usafiri huo kuelemewa nyakati fulani.

Magazeti ya Leo ijumaa ya tarehe 10/06/2016














Alhamisi, 9 Juni 2016

‘Hali ya Spika Ndugai ni njema’


Imeandikwa na Mwandishi Wetu

OFISI ya Bunge imesema kuwa hali ya Spika wa Bunge, Job Ndugai (pichani) ni njema kabisa na yupo nchini India kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake kutokana na maelekezo ya daktari wake kumtaka hivyo mapema mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Ofisi ya Bunge mjini Dodoma jana, kumekuwa na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hali ya Spika Ndugai na kuzua hofu kwa viongozi na wananchi.
“Ofisi ya Bunge inapenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha Watanzania wote kuwa taarifa hizo ni za uzushi mkubwa na hazina ukweli wowote,” ilieleza taarifa hiyo. Ilieleza kuwa Spika amepokea salamu nyingi za kumtakia kheri wakati akiendelea na uchunguzi wake, kutoka kwa viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge na amewatakia Mfungo mwema wa Ramadhani kwa wale waliofunga kutimiza ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Mheshimiwa Spika pia amewatakia kazi njema wabunge wote ya kushughulikia Bajeti ya Serikali inayosomwa leo (jana),” ilieleza taarifa hiyo na kuongeza: “Tunawaomba Watanzania wote wenye nia njema na Spika wetu waendelee kupuuza taarifa zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii na waendelee kumwombea ili afya yake iimarike haraka

Mikoa mitano iliyokithiri kwa umasikini yatajwa


Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Dodoma


PAMOJA na maendeleo yaliyotokana na kukua kwa pato la wastani la Mtanzania na kupungua kwa umasikini wa mahitaji ya msingi, serikali imeainisha mikoa mitano iliyokithiri kwa umasikini wa kipato.
Akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi ya 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema mkoa unaoongoza ni Kigoma ambao wakazi wake asilimia 48.9, wanakabiliwa na umasikini uliokithiri wa kipato.
Mikoa mingine yenye umasikini wa kipato kiwango chake katika mabano ni Geita (asilimia 43), Kagera (asilimia 39), Singida (asilimia 38.2) na Mwanza (asilimia 35.3). Katika wilaya zilizokithiri kwa umasikini wa kipato, ni Kakonko mkoani Kigoma na Biharamulo mkoani Kagera, ambapo Dk Mpango alisema katika wilaya hizo, takribani asilimia 60 ya watu wake, wako chini ya mstari wa umasikini wa mahitaji ya msingi.
Tathmini ya hali ya umasikini kimaendeleo iliyoainisha umasikini huo, imetumia takwimu za Sensa ya Watu ya mwaka 2012 na Utafiti wa Hali ya Kipato na Matumizi katika Kaya wa 2012, ulionesha pia ahueni ya umasikini katika mikoa mitano.
Dk Mpango alitaja mikoa hiyo yenye ahueni na idadi ya watu wanaokabiliwa na umasikini wa kipato katika mabano kuwa ni Dar es Salaam (asilimia 5.2), Kilimanjaro (asilimia 14.3), Arusha (asilimia 14.7), Pwani (asilimia 14.7) na Manyara (asilimia 18.3). Pamoja na tathmini ya kimkoa na kiwilaya lakini katika nchi nzima, alisema kati ya mwaka 2010 na 2015, Pato la Mtanzania liliongezeka kutoka Sh 770,464.3 kwa mwaka mpaka Sh milioni 1.9 mwaka 2015 sawa na mara 2.5.
Aidha kupungua kwa umasikini nako kulikuwa kasi katika kiwango cha asilimia 6.2 ndani ya miaka mitano tu kati ya mwaka 2007 na 2012, ikilinganishwa na kupungua kwa umasikini kwa asilimia 4.6 tu katika miaka 15 kulikotokea mwaka 1992 mpaka 2007.
Kuhusu ajira, Dk Mpango alisema Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 ulionesha kuwa nguvukazi ya Taifa ilikuwa watu 25,750,116 sawa na asilimia 57 ya watu wote wa Tanzania Bara.
Kati ya nguvu kazi hiyo, wanawake wametajwa kuwa 13,390,678 sawa na asilimia 52 na wanaume ni 12, 359, 438 sawa na asilimia 48. Pamoja na nguvukazi kuwa watu milioni 25.8, utafiti huo kwa mujibu wa Dk Mpango, ulionesha kuwa watu wenye uwezo wa kufanya kazi walikuwa watu milioni 22.3 tu na sababu za watu kushindwa kufanya kazi zilikuwa ni ulemavu na ugonjwa wa muda mrefu.
Aidha, kati ya nguvu kazi ya taifa; watu milioni 25.8, utafiti huo umeonesha kuwa asilimia 77.8 ndio walikuwa katika ajira, wengi wakiwa wa vijijini sawa na asilimia 82.2 ikilinganishwa na mijini ambapo Dar es Salaam waliokuwa wakifanya kazi ni asilimia 59.8 tu.
Mafanikio ya kupungua kwa umasikini, yameonekana pia katika kuongezeka kwa umri wa kuishi wa Mtanzania kutoka miaka 51 ilivyokuwa mwaka 2001 mpaka miaka 61 kwa takwimu za mwaka 2012.
Vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja, pia vimepungua kufikia 43 kwa kila watoto hai 1,000 mwaka 2015 kutoka vifo vya watoto 51 kwa kila watoto hai 1,000 mwaka 2010.
Kuhusu watoto wa chini ya miaka mitano, pia vifo vyao vimepungua kutoka vifo vya watoto 81 kwa kila watoto hai 1,000 mwaka 2010 mpaka vifo vya watoto 67 kwa kila watoto hai 1,000 mwaka 2015.
Mafanikio hayo ya kupungua kwa vifo na kuongezeka kwa umri wa kuishi wa Mtanzania, katika upande mwingine yameleta changamoto kutokana na kuongezeka kwa wasichana waliopata ujauzito utotoni.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, idadi ya wasichana wanaopata mimba katika umri wa miaka 15 hadi 19 imeongezeka na kufikia asilimia 27 mwaka 2015, kutoka asilimia 23 mwaka 2010.
Dk Mpango alisema hali hiyo si dalili nzuri kwani kunaashiria kuongezeka kwa utegemezi na kudumaza jitihada za kuondoa umasikini katika jamii na kuwataka wabunge kushirikiana na Serikali kuhimiza watoto wa kike, kuongeza bidii katika masomo ili kwa pamoja kupatikane manufaa kutokana na mapambano ya umasikini.

Serikali kutekeleza miradi mikubwa 4 ya kielelezo



MPANGO wa Maendeleo wa Mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, umekuja na miradi mikubwa minne ya kielelezo, itakayotekelezwa kwa kutumia sehemu kubwa ya Sh trilioni 11.8 zilizotengwa kwa maendeleo, ambazo ni sawa na asilimia 40 ya Bajeti yote ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Kwa kuonesha dhamira ya serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo, asilimia 74 ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo itakuwa makusanyo ya ndani ya serikali na asilimia 26 tu ndio mapato ya nje. Akisoma Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2016/2017 bungeni jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (pichani) alitaja miradi hiyo ambayo baadhi Rais Magufuli alishaizungumzia katika baadhi ya hotuba zake.
“Kwa maana ya kipekee, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17, umeainisha miradi mikubwa ya kielelezo, ambayo itapewa msisitizo katika utekelezaji wake,” alisema Dk Mpango. Mradi wa kwanza wa maendeleo katika kundi hilo la miradi minne mikubwa ya kielelezo ni ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) ambao Rais Magufuli aliahidi kutenga Sh trilioni moja ya kuanza ujenzi wakati wakitafuta fedha za kuendeleza ujenzi wake.
Reli hiyo itaanzia Dar es Salaam kwenda Kigoma na Tabora mpaka Mwanza na itakuwa na matawi ya kutoka Isaka hadi Kigali/Keza na Msongati hadi Kaliua- Mpanda. Aprili mwaka huu, wakati Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alipokwenda Ikulu, Rais Magufuli alimweleza kuwa Tanzania imedhamiria kuanza ujenzi wa reli hiyo haraka iwezekanavyo na tayari imetenga fedha hizo katika bajeti yake hii ya kwanza kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
“Tuna imani kuwa mradi huu utasaidia kuleta mapinduzi makubwa ya uchumi katika nchi yetu na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kati zikiwemo Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ndio maana hatutaki kupoteza muda kwa mazungumzo marefu, tunataka kazi ianze na watu waanze kunufaika,” alikaririwa Rais Magufuli katika mazungumzo hayo. Naye Dk Youqing alielezea utayari wa China kushirikiana na Tanzania katika mradi huo ambao zabuni za ujenzi zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Rais Magufuli pia alipozindua ujenzi wa barabara ya juu ya Tazara, alirejea kauli hiyo, lakini akasisitiza kuwa reli hiyo ikifika Ruvu, mizigo yote ya Bandari ya Dar es Salaam itasafirishwa kwa reli mpaka eneo hilo na malori yataanzia Ruvu badala ya kuongeza foleni na kuharibu barabara za Dar es Salaam.
Manufaa mengine reli hiyo itakapokamilika, itapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 30, na kuifanya bandari hiyo kuwa na unafuu mwingine kwa wateja kimataifa, mbali na unafuu unaotokana na eneo la kimkakati.
Mradi wa pili wa kielelezo katika bajeti ya maendeleo ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa mujibu wa Dk Mpango ni ununuzi wa ndege tatu mpya za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Dk Mpango alitaja aina ya ndege hizo kuwa ni Bombardier Q400 mbili, zenye uwezo wa kubeba abiria 67 mpaka 88 kila moja na nyingine aina ya Bombardier CS 300 yenye uwezo wa kubeba abiria 100 mpaka 150.
Dk Mpango alitaja mradi wa tatu wa kipaumbele kuwa ni ununuzi wa meli moja mpya ya usafirishaji wa mizigo na abiria katika Ziwa Victoria, ununuzi utakaofanyika sambamba na ukarabati wa meli tatu za Mv Victoria, Mv Butiama na Mv Liemba ili kuimarisha usafirishaji.
Nia hiyo ya serikali ambayo sasa imewekwa katika utekelezaji wa miradi ya kielelezo iliyotengewa fedha iliwahi kuzungumziwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Machi mwaka huu aliposema serikali imeanza kukusanya fedha kwa ajili ya kununua meli mpya.
Alisema ahadi ya ununuzi wa meli hiyo iliyotolewa na Rais Magufuli katika kampeni za 2015 iko palepale kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo kwenye Ziwa Victoria. Mradi wa nne wa msisitizo katika mpango wa maendeleo wa mwaka huu ambao utekelezaji wake utaanza ni mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma na mradi wa chuma Liganga katika wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Eneo la Mchuchuma linakadiriwa kuwa na hazina ya tani milioni 540 za makaa ya mawe ambayo ni malighafi muhimu ya uzalishaji umeme nafuu kuliko wa mafuta unaohitajika kwa wingi kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda.
Aidha, eneo la Liganga linakadiriwa kuwa na hazina ya chuma cha pua tani milioni 45 ambayo ndiyo malighafi mama ya viwanda vikubwa na vya kati duniani. Mbali na hazina hiyo, maeneo hayo pia yapo kimkakati zaidi kwa kuwa yako karibu na hivyo kufanya uyeyushaji wa chuma hicho cha pua kuwa nafuu kuliko mahali pengine duniani, kutokana na ukaribu wa hazina ya makaa ya mawe na chuma hicho.

Habari zilizopo katika Magazet ya Leo alhamisi ya tarehe 9/6/2016