ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 10 Juni 2016

Mzee Mwinyi akunwa mabasi ya haraka

Imeandikwa na Anastazia Anyimike
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi jana alitembelea Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka na kusema licha ya kuchelewa kwa mradi huo ana imani utasaidia kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kumaliza safari yake katika kituo cha Kivukoni jana akitokea kituo cha Morocco na kwenda kituo cha Gerezani, Kariakoo na baadaye Kivukoni, Mwinyi aliyekuwa amefuatana na mkewe, Mama Sitti, alisema mradi huo utasaidia kupunguza foleni katika jiji na kwamba umeanza kuwaondolea wananchi adha ya kugombea usafiri wakati waendapo na warudipo katika shughuli zao.
Alisema licha ya mabasi hayo kugawana abiria na daladala na bodaboda, ana imani siku zijazo na utaratibu ukiwekwa vyombo vingine vya usafiri visiingie mjini ili mabasi hayo yawe huru kufanya kazi, tija zaidi itaonekana.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), Ronald Lwakatare alisema muda wowote ndani ya mwezi huu wananchi wataanza kutumia tiketi za kadi baada ya taratibu zote kukamilika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Usafirishaji ya UDA-RT, David Mgwasa alisema wananchi wameanza kuelewa juu ya matumizi ya mabasi na miundombinu yake, huku akisema tatizo linalowakabili kwa sasa ni mlundikano wa abiria wakati mmoja jambo ambalo linafanya usafiri huo kuelemewa nyakati fulani.

Hakuna maoni: