ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumanne, 28 Juni 2016

#WAZO LANGU# pongezi mliochaguliwa kidato cha tano lakini............


Imeandikwa na Ikunda Erick

UPO usemi usemao, Elimu ni Ufunguo wa Maisha. Usemi huu unatumika kama msisitizo wa umuhimu wa elimu kwa wale wanaopenda mafanikio katika maisha. Juzi mjini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene alitangaza matokeo ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo mbalimbali vya ufundi nchini.
Katika matokeo hayo, jumla ya wanafunzi 90,248 wamechaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2016, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.1 ikilinganishwa na wanafunzi 55,003 waliochaguliwa mwaka jana.
Mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka jana ni kwamba jumla ya watahiniwa 393,734 walihitimu kidato hicho, hii ina maana kwamba waliopata nafasi ya kuendelea kidato cha tano kupitia mfumo wa serikali ni hao wateule 90,248.
Hii ina maana kubwa kwa wale walio makini kufuatilia masuala ya elimu. Kwanza kwa wanafunzi waliopata nafasi watambue kuwa wamechaguliwa wao kutokana na bahati, kwani waliofaulu ni zaidi ya hao, ila uwepo wa nafasi ni chache.
Hivyo ni vyema, wanafunzi hao wakatumia nafasi hiyo kikamilifu kwa kuongeza juhudi kwenye masomo na kutilia mkazo elimu kwa sababu wakiichezea, watajuta na hivyo kuwa mwanzo wa kuharibu maisha yao ya baadaye.
Kama nilivyotangulia kusema, Elimu ni Ufunguo wa Maisha, ni wazi kwamba wale waliopata nafasi ya kuendelea kusoma ama kidato cha tano au chuo cha ufundi, kinachohitajika ni kutia nia, kusoma kwa bidii na kujiepusha na makundi mabaya ambayo yanaweza kuwapoteza na kuishia kuingia kwenye makundi yasiyofaa.
Ikumbukwe kwamba wapo kundi kubwa waliokosa nafasi ya kuendelea na masomo hayo sio kwamba wamefeli, la hasha bali ni kutokana na uhaba wa nafasi na kwamba huenda wakaishia hapo kutokana na sababu tofauti zikiwemo za wazazi kushindwa kumudu gharama za kuwasomesha shule binafsi za sekondari.
Sasa basi, rai yangu kwa waliopata nafasi, msiichezee na jambo la msingi kwa wazazi na walezi ni kuwa karibu na wanafunzi hao na kuwaeleza ukweli wa maisha yalivyo kwamba wajibu wao ni kusoma na sio kucheza na maisha.
Kwa wale watakaotia nia na kujituma ni wazi kwamba watafika mbali kielimu na wanaweza kuwa ufunguo huo waliopata wa kidato cha tano, ndio unaoweza kuwa ufunguo wa kuendelea hadi ngazi ya chuo kikuu na kuja kuwa na wasomi wenye ujuzi wa kujiajiri au kubahatika kuajiriwa, hivyo wasome kwa bidii badala ya kubweteka kwa kuamini hayo ndiyo mafanikio ya juu kielimu kwao.
Pia jambo muhimu kwa jamii yetu ni kwamba tushirikiane sote katika kuhakikisha kila tarafa katika maeneo yetu inakuwa na shule ya kidato cha tano na sita, ili kutoa nafasi ya wanafunzi wengi zaidi kuchaguliwa kuendelea na masomo hayo.
Kama kila mkoa, mji, wilaya na kata kwa ushirikiano wa viongozi wake wataweka msisitizo kwenye ujenzi wa madarasa kwa ngazi hizo, na jamii ikishirikishwa, ni wazi kwamba idadi ya wanafunzi watakaochaguliwa kuendelea na masomo hayo itaongezeka.
Mwito ni kwa jamii mzima kuona umuhimu wa kuchangia sekta ya elimu, ambayo hivi sasa agizo la Rais John Magufuli ni kwamba kila mkoa uhakikishe shule zilizopo kwenye maeneo yao zinakuwa na madawati ya kutosha, sambamba na vyumba vya madarasa.
Agizo hilo, linapaswa kutimia ifikapo Julai mwaka huu na lengo la Rais ni kuona sekta hiyo inakua na kwa kuanza tumeona juhudi zilizofanywa kwa serikali kufuta ada katika shule za msingi na sekondari, jambo ambalo limeongeza idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza.
Sasa basi, ongezeko hilo liwe na tija kwa kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake, kama mzazi kuhakikisha unafuatilia maendeleo ya watoto na kama mwanafunzi kusoma kwa bidii na walimu nao watimize wajibu wao kwa kutoa elimu stahiki. Kwa kufanya hivyo ni wazi kwamba tutajenga taifa lenye wasomi na kuondokana na uwepo wa watu wasio na elimu, ambao ni chanzo kimojawapo cha umasikini.

Hakuna maoni: