Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza kutoa vitambulisho vya Taifa
vyenye saini ya mwenye kitambulisho kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
Kauli
hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa
Mamlaka hiyo Bi. Rose Mdami wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo
jijini Dar es salaam.
Akifafanua
Mdami alisema kuwa lengo la Mamlaka hiyo ni kuhakikisha kuwa Watanzania
wote wanapata vitambulisho vya Taifa ambapo katika hatua ya kwanza
mamlaka hiyo inachakata taarifa za wananchi walizotoa wakati wa
kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa
mwaka jana.
Utoaji
wa vitambulisho hivi vyenye saini ya mwombaji utasaidia kuwatambua
wahusika pale wanapohitaji huduma mbalimbali za kijamii.
“Upatikanaji
wa vitambulisho vya Taifa utasaidia Serikali kuondokana na tatizo la
Watumishi hewa kwa kuwa mfumo wetu utaunganishwa na mifumo mingine
inayosimamia utumishi wa umma” alisisitiza Mdami.
Utoaji
huo wa vitambulisho utaanza kwa kutoa namba za utambulisho kwa wananchi
ili zisaidie katika upatikanaji wa huduma mbalimbali wakati mchakato wa
kuzalisha vitambulisho hivyo ukiendelea.
Mdami
alifafanua kuwa baada ya kuchakata taarifa kutoka Tume ya Taifa ya
Uchaguzi zitarudishwa kwenye mitaa na vijiji husika kwa ajili ya uhakiki
wa taarifa hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni