ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatatu, 20 Juni 2016

Majibu 10 ya Bajeti yasubiriwa bungeni leo



MAMBO makubwa 10 yaliyojitokeza kwenye mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 pamoja na Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2015, yatajibiwa na kutolewa ufafanuzi leo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango bungeni.
Moja ya mambo hayo ni hoja ya kufuta au kutofuta kodi kwenye kiinua mgongo cha wabunge. Kabla ya Dk Mpango kutoa ufafanuzi na marekebisho ya Bajeti Kuu ya Serikali, kama yatakuwepo na hatimaye kupitishwa au kutopitishwa kwa kupigiwa kura, mawaziri mbalimbali wanatarajiwa pia kujibu baadhi ya hoja zilizoelekezwa kwenye wizara zao.
Kutokana na mjadala wa bajeti uliochukua takribani wiki nzima, wabunge walipendekeza kodi na tozo kadhaa kufutwa ili kuwapunguzia wananchi mzigo, hatua itakayosababisha serikali kuongeza kodi kwenye baadhi ya vitu kama itakubaliana na hoja za wabunge. Moja ya eneo linaloweza kukumbwa na ongezeko la kodi kama serikali kama wanavyopendekeza wabunge ni petroli.
Alipowasilisha Bajeti ya Serikali Juni 8, Waziri Mpango alisema serikali haikuongeza kodi yoyote kwenye petroli na dizeli ili kutowaongezea wananchi mzigo na hofu ya kusababisha mfumuko wa bei.
Kiinua mgongo cha wabunge Wawakilishi hao wa wananchi wamekuwa wakipinga hatua ya serikali kupendekeza kuwakata kodi ya asilimia tano kwenye kiinua mgongo chao wanacholipwa kila baada ya miaka mitano, wakidai kitawaumiza kwa kuwa wao hawalipwi pensheni na kwamba fedha hizo, mbali na kujikimu, zinawasaidia pia katika kuchangia shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwenye majimbo yao.
Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba mwaka jana Bunge la 10 lilipovunjwa, kila mbunge alilipwa kiinua mgongo cha Sh milioni 230 na kama wabunge watalipwa kiasi kama hicho mwaka 2020, kila mbunge atabakiwa na Sh milioni 218.5 baada ya kukatwa kodi hiyo wanayoilalamikia.
Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM), alidai kwamba hatua ya kuwakata wabunge kodi kwenye kiinua mgongo inapaswa kuangaliwa upya kwani wabunge wa Tanzania ndio wanaolipwa mshahara mdogo kulinganisha na wenzao wa Afrika Mashariki.
Alidai kwamba mbunge wa Kenya analipwa Dola za Marekani 11,000, Rwanda Dola 9,000, Uganda Dola 8,000, Sudan Kusini Dola 7,000, Burundi Dola 6,000, wakati wabunge wa Tanzania hulipwa Dola 5,000. Wabunge wanaona pia kama hatua hiyo ni ya kibaguzi wakisema kama serikali imefikia uamuzi huo katika kusaka mapato zaidi, basi ni vyema kodi ya kiinua mgongo iende hadi kwa marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu, maspika na naibu spika na wakuu wa mikoa na wilaya.
Mtazamo huu wa wabunge ni tofauti na walio nao wananchi wengi nje ya Bunge wakiwemo wasomi ambao wanaamini kwamba wabunge ambao wamekuwa wakiomba sana maendeleo kwenye majimbo yao, wangekuwa wa kwanza kuonesha utayari wa kuchangia mapato ya serikali kwa kukubali kukatwa kodi hiyo. Hata hivyo, wapo wabunge kadhaa wa CCM na karibu wote wa upinzani wamehiari kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao.
VAT kwenye utalii Suala la pili lililozungumziwa na wabunge wengi ni kuitaka serikali kuachana na hatua ya kuanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18 kwenye huduma za utalii. Wakati akiwasilisha hotuba yake ya Bajeti, Dk Mpango alisema kwamba kodi hiyo ipo pia katika nchi za Kenya, Afrika Kusini na Rwanda. Lakini wabunge katika mjadala walimpa angalizo Waziri kwamba Kenya imeondoa kodi hiyo na bila shaka sababu ni kujikuta wakipoteza watalii wengi.
Walisema kama serikali haitaondoa kodi hiyo basi itegemee mpango wa kuongeza watalii zaidi kutofanikiwa kwani wengi watakimbilia maeneo yatakayoonekana kutokuwa ghali. CAG aongezewe fedha Suala la tatu lililozua mjadala mkubwa ni hatua ya serikali kuipunguzia fedha ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kulinganisha na kiwango kilichoombwa wakisema hatua hiyo itaifanya ofisi hiyo muhimu katika kupambana na ufisadi kushindwa kutimiza majukumu yake.
Ofisi hiyo iliomba Sh bilioni 68.8 katika mwaka huu wa fedha ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi lakini katika bajeti inayopendekezwa imepewa Sh bilioni 32.3 pekee. Wabunge walisema ofisi hiyo ni chombo muhimu katika kupeleka ushahidi kwenye Mahakama ya Mafisadi inayotarajiwa kuundwa mwezi ujao hivyo ni lazima serikali ihakikishe utendaji wake haukwamishwi na uhaba wa fedha.
Wabunge pia waliitaka serikali kuongeza fedha kwenye miradi ya maji kwani maji ndio kero kubwa inayowasumbua wananchi wengi na hata wakati wa kampeni, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alikiri kwamba ndio kilikuwa kilio kikubwa cha wananchi alichokutana nacho. Walitaka serikali iongeze Sh 50 kwenye petroli kwa ajili ya miradi ya maji vijijini sawa na ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye mkakati wa kupeleka umeme vijijini ambao kwa kiwango kikubwa umeleta mafanikio.
TRA na kodi ya majengo Lingine lililozua mjadala mkubwa kwenye mapendekezo ya serikali katika bajeti yake ni kuhamisha jukumu la ukusanyaji wa kodi za majengo kutoka katika halmashauri na kupelekwa katika Mamlaka ya Mapato (TRA). Wabunge waliopinga mpango huo walitaja sababu zaidi wakidai taarifa walizonazo ni kwamba hata mpango wa majaribio wa TRA kukusanya kodi za majengo katika mkoa wa Dar es Salaam haukuzaa matunda makubwa.
Waliokubaliana na pendekezo hilo la serikali nao walitoa angalizo kwamba kama hatua hiyo itachukuliwa ni lazina kuwe na utaratibu utakaohakikisha kwamba fedha hizo hazichelewi kupewa halmashauri husika kwa kuwa zimekuwa zikitegemewa sana kwa shughuli mbalimbali. Takwimu za mikoa masikini Lingine lililowagawa wabunge ni kuhusu takwimu za mikoa mitano masikini zaidi nchini na mitano yenye ahueni ambapo baadhi ya wabunge walizitilia mashaka.
Mbunge mmoja alishangaa kuona mkoa wa Mwanza ukiwa miongoni mwa mikoa mitano masikini wakati taarifa ya Benki Kuu inaonesha kwamba mkoa huo ni wa pili katika kuipatia Hazina mapato mengi nyuma ya Dar es Salaam.
Akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2015, Dk Mpango alitaja mikoa masikini zaidi kuwa ni Kigoma, Geita, Kagera, Singida na Mwanza huku yenye ahueni ikiwa ni Dar es Salaam, Kilimajaro, Arusha, Pwani na Manyara.
Kodi miamala ya simu, mitumba Jambo la saba ambalo wawakilishi hao wa wananchi walitaka serikali iliangalie kwa mapana yake pia ni kodi kwenye miamala ya simu na benki. Hofu ya wabunge ilikuwa kwamba kama kodi hiyo itawekwa bila udhibiti wowote, kampuni, hususan za simu zitahamishia ‘maumivu’ ya kodi hiyo kwa wananchi.
Lingine ambalo wabunge walililalamikia ni Bajeti inayopendekezwa na serikali kupandisha ushuru wa nguo na viatu vya mitumba kutoka Dola za Marekani 0.2 mpaka Dola za Marekani 0.4 kwa kilo. Hatua hiyo ambayo ni sehemu ya makubaliano ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, inalenga kudhibiti mitumba ikiwa ni sehemu ya kujiandaa kwa kuzuia kabisa uingiaji wake.

Hakuna maoni: