Aidha, imesema itahakikisha viongozi waliochaguliwa kushiriki utambuzi na ugawaji wa fedha hizo kwa kaya masikini, wakiwemo wa vijiji waliohusika kuwaingiza kwenye orodha watu wasio na sifa kwa makusudi, nao wanachukuliwa hatua zinazostahili. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema hayo bungeni mjini hapa jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Sabreena Sungura (Chadema) aliyetaka kufahamu hatua zilizochukuliwa kwa waliofanya makosa hayo.
“Kwa kuwa mpango huo umeleta malalamiko mengi na kumekuwa na watumishi waliohusika kusababisha makosa hayo ya kuorodhesha wasio masikini, je, Serikali inawachukulia hatua gani?” alihoji.
Akijibu, Simbachawene alisema, baada ya kutambua udanganyifu katika kaya 25,446 kwamba hazikuwa na vigezo, Serikali imechukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuagiza kuondolewa kwa watu hao kwenye orodha.
Alisema, kuhusu viongozi wa vijiji na wengine waliochaguliwa kushiriki mpango huo wa kugawa fedha kwa kaya masikini, itaangaliwa kuona endapo walifanya makusudi kuwaingiza watu wasio na sifa au ilitokea bahati mbaya kwa sababu ya kutokuwa na takwimu sahihi, ili hatua zichukuliwe.
Alisema kuwa makosa mengine yanaweza yakatokea lakini si kwa makusudi ya aliyoyatenda, hivyo wanaangalia suala hilo pia kabla ya kuchukua hatua zaidi. Katika swali lake la msingi, Sungura kupitia Mollel alitaka kujua Serikali imejipangaje kutatua kero ya mgawanyo wa fedha hizo, ambapo alieleza kuwa wananchi wengi wasio na uwezo wamekuwa hawazipati.
Simbachawene alisema, hasa katika Mkoa wa Kigoma, udanganyifu umefanyika kwa kiasi kikubwa na wahusika wote watachukuliwa hatua zinazostahili za kisheria, kuhakikisha suala hilo haliendelei kutokea.
Alieleza kuwa utambuzi wa kaya za walengwa wa mpango huo ulianza Novemba, 2013 na hadi sasa umekwishaandikisha kaya milioni moja na laki moja katika halmashauri 159 za Tanzania Bara, pamoja na wilaya zote za Unguja na Pemba.
Kwa mujibu wa Simbachawene, kaya hizo zinapata ruzuku kwa utaratibu wa uhawilishaji fedha baada ya kutimiza masharti ya kupeleka watoto shule na kliniki. Alisema, wakati mpango wa kunusuru kaya masikini unaanza ulipanga kufikia asilimia 70 ya vijiji, mitaa na shehia za halmashauri ambavyo vimefikiwa zilijaziwa dodoso ili kukusanya taarifa zaidi za kaya na hatimaye ziliandikishwa kwenye daftari la walengwa na kuanza kupokea ruzuku.
Alisema, maeneo yote 161 ya utekelezaji ambayo ni halmashauri 159 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba, zimeshaondoa kaya zisizostahili kuwa kwenye orodha ya walengwa. “Jumla ya kaya 25,446 zimekwishaondolewa kwenye mpango huo kwa sababu mbalimbali zikiwemo vifo, kukosa vigezo vya kuwa kaya masikini na kuondolewa kwa wajumbe wa kamati za mpango na viongozi wa vijiji, mitaa na shehia katika orodha ya kaya masikini,”alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni