Wakati
Kamati ya Haki, Maadili na Madara ya Bunge imepokea mashtaka dhidi ya
Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, mbunge mwingine wa upinzani
ameamua kumshtaki kiongozi huyo kwenye Kamati ya Kanuni ya Bunge.
Mbunge
wa kwanza kumshtaki Dk Tulia, alikuwa Mbunge wa Simanjiro (Chadema),
James ole Millya aliyewasilisha kusudio lake kwa Spika wa Bunge hilo,
Job Ndugai mashtaka sita na tayari yamewasilishwa kwenye kamati husika.
Mbunge
wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alitangaza jana uamuzi wake wa
kumshtaki Dk Tulia, ambaye ndiye anayeliongoza Bunge kwa sasa.
Dk Tulia atakuwa na kesi mbili, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka na kwenye Kamati ya Kanuni.
Dk
Tulia anakuwa Naibu Spika wa kwanza tangu kuanza Bunge linalojumuisha
wabunge wa upinzani, kushtakiwa kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu
za Bunge.
Kubenea
alisema ameamua kumshtaki Dk Tulia katika kamati hiyo akidai kuwa
alivunja kanuni na taratibu wakati akiwasilisha malalamiko ya Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kwenye Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa mbunge huyo alisema uongo
bungeni.
Akizungumza
na wanahabari, mbunge huyo alisema hakuridhishwa na hatua ya Dk Tulia
aliyoifanya Mei 13 na kwamba tayari alishawasilisha barua yake yenye
hoja tano za mapungufu ya kikanuni kwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashililah tangu Ijumaa iliyopita.
Kubenea
alieleza kuwa Dk Tulia alitumia kanuni ya 71 kupokea malalamiko ya Dk
Mwinyi kinyume na utaratibu kwa kuwa kanuni hiyo huruhusu watu wasio
wabunge kupeleka malalamiko yao kwa Spika, iwapo masuala yaliyojadiliwa
bungeni yamewaathiri.
Alisema
wakati akichangia hoja ya wizara hiyo Mei 10, alimtaka Dk Mwinyi aeleze
juu ya kuwapo kwa mkataba baina ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na
Kampuni ya Heinan Guoji Industry & Investment Limited na kama upo
haoni kama kuna mgongano wa masilahi kutokana na kushiriki kumjengea
nyumba yake.
Hata
hivyo, alidai hakuna mbunge aliyesimama kudai hoja hiyo ilikuwa ya
uongo kama kanuni ya 63(3) inavyotaka, badala yake siku tatu baadaye
alitakiwa kufuta bungeni jambo ambalo anaona Dk Tulia hakumtendea haki.
“Naibu
Spika wakati akitoa mwongozo wa Spika alinukuu sehemu tu ya maelezo
yangu jambo lilipotosha misingi na mantiki ya mchango wangu bungeni
hivyo kuashiria alikuwa na nia mbaya dhidi yangu,” alisema Kubenea na kuongeza: “Hata
nilipoomba kufanya hivyo siku aliposoma mwongozo na kunipa nafasi ya
kufuta maneno yangu au kuyathibitisha, alikataa na endapo angezingatia
mchango wangu wote angetenda haki.”
Katika
barua hiyo, Kubenea amelalamika kuwa wakati Dk Tulia anapokea
malalamiko kutoka kwa Dk Mwinyi hakumpelekea nakala ili kurahisisha
utetezi wake.
Pia,
alieleza kuwa Naibu Spika aliamua kimakosa kuwasilisha tuhuma dhidi
yake kwenye kamati hiyo bila kuzingatia maelezo aliyowasilisha kwake na
vielelezo huku akijua Waziri huyo wa ulinzi alikiuka kanuni ya 63 (3) na
64(2).
Kubenea
alisema anaiomba Kamati ya Kanuni yenye nguvu kuliko Spika kusimamisha
mchakato unaoendelea kufanywa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge juu ya suala lake hadi pale itakapofanya uamuzi iwapo ilifuata
kanuni ama la.
Katika
barua hiyo, Kubenea anamuomba Dk Kashililah amjulishe Spika ili aweze
kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5(5) ili
kuona kama kulikuwa na uhalali wa shauri lake na anaamini Katibu huyo wa
Bunge atamtendea haki.
Kubenea
alishahojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Alhamisi
iliyopita na kueleza kuwa alikubali kufanya hivyo kwa kuwa kamati hiyo
ina nguvu kubwa ya kikanuni ikiwamo kukamatwa.
Kubenea
alisema hana wasiwasi na aliyoyasema ila anataka haki itendeke kwa
kufuata kanuni na hadi sasa ana vielelezo vya kutosha kuhusu suala lake.
Dk Kashililah alieleza jana kuwa hawezi kuzungumzia kwa kina jambo hilo kwa kuwa taratibu zote za kufuata zinafahamika.
“Inawezekana
ameandika, lakini mpaka ifike tuipokee. Mimi nilikuwepo Ijumaa hadi saa
tano usiku sikuiona. Huenda ipo njiani ikifika tutaipokea na
tutaifanyia kazi,” alisema Kashililah.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni