ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatatu, 27 Juni 2016

Maeneo korofi kufikishiwa simu kwa satelaiti



 SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kutumia mtambo wa satelaiti, kufikisha huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo korofi nchini.
Maeneo hayo ni yaliyo kwenye changamoto za kijiografia yaliyopo maeneo ya mabondeni na milimani, ambako watoa huduma za simu wameshindwa kuyafikia kutokana na kutokuwa na mvuto wa kibiashara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustin Kamuzora alisema hayo mkoani Morogoro akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa minara ya simu ya Vodacom na Tigo katika kata za Kanga na Maskati wilayani Mvomero.
Mvomero ipo katika mradi wa mawasiliano vijijini wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Ziara hiyo iliongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Peter Ulanga na wahandisi wa minara hiyo kutoka kampuni za Tigo na Vodacom.
Profesa Kamuzora alisema ameridhishwa na kazi ya miradi hiyo baada ya kuikagua na kubaini mawasiliano yanapatikana. Alitaka kampuni zilizo kwenye mradi huo, kuhakikisha zinatatua changamoto ndogo zilizopo miradi hiyo iwe endelevu.
“Inabidi sasa kuangalia suala la matumizi ya satelaiti kwa maeneo ambayo jiografia yake ni ngumu, hasa kwa watu wanaokaa mabondeni. Nimeridhishwa na mradi hasa kwa namna walivyoamua kutumia teknolojia ya umeme wa jua katika minara yote,” alisema hayo akiwa kwenye mradi wa Maskati, uliopo kilometa 110 kutoka Morogoro mjini.

Hakuna maoni: