ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumanne, 21 Juni 2016

Marais, maspika wastaafu watwishwa zigo la Bunge



MARAIS wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na maspika wastaafu, wametakiwa kusaidia kutoa ushauri ya namna bora ya uendeshaji wa shughuli za vikao vya Bunge kwa sasa, hususan katika kipindi hiki cha vyama vingi ili wananchi wawakilishwe vyema zaidi kuhusu mahitaji yao bungeni.
Pia Watanzania wametakiwa kufanya maombi maalumu, yenye lengo la kuombea Bunge ili lirudi katika misingi ya awali ya Utanzania kwa kujenga umoja, mshikamano na uvumilivu na kuweka mbele dhamira ya dhati ya kuwawakilisha wananchi katika mahitaji yao na si kutanguliza dhamira za kivyama wakati wa vikao vyake.
Hayo yalisemwa na Paroko wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Paulo wa Msalaba la mjini Dodoma, Padri Sebastian Mwaja wakati wa mahubiri ya ibada za Jumapili zilizofanyika kanisani hapo juzi.
Padri Mwaja alisema Bunge la sasa, linaloendelea na vikao vyake hapa linawanyong’onyesha wengi kwa kushindwa kujikita katika taratibu na desturi nzuri za Kitanzania za kujenga umoja, mshikamano na kuvumiliana katika mambo mbalimbali na badala yake limeshuhudia mvutano, mgawanyiko na kutovumiliana.
“Tunapofanya ufuatiliaji wa hoja za wabunge katika vikao vyake, hatupati kuona ile dhamira ya wazi ya kuwakilisha hoja na mahitaji ya Watanzania wa ngazi za chini ili mahitaji yao yapatiwe ufumbuzi na badala yake tunashuhudia hoja zenye mlengo wa kujipendelea mambo yao zaidi na kuwaacha wananchi na hofu ya kujiuliza endapo kweli dhamira ya kuwatumikia wananchi endapo ni kipaumbile cha kwanza,” alieleza Padri Mwaja.
Alieleza jinsi Bunge linavyojikita katika uvyama na kudhoofisha msingi wa umoja, mshikamano na usawa pamoja na kuvumiliana kama ilivyo tangu awali ambako Watanzania walisifiwa kimataifa kwa sifa hiyo lakini sasa, haipo hivyo, na kushauri juhudi za makusudi lazima zifanyike ili kurudi katika mstari huo mzuri.
Alifafanua kwa undani kwamba kujadili hoja bungeni kwa kuweka mbele dhamira za kivyama, kwa kushuhudia hoja za msingi za kuwatetea wananchi, zikiwekwa pembeni na kuweka mbele dhana ya uvyama, akisema hilo halitasaidia kuwatatulia wananchi kero zao nyingi kama Bunge halitarudi katika misingi ya kizalendo.
Alieleza kusikitishwa na mparaganyiko wa umoja bungeni na kutokuwa na mshikamano katika kuendesha shughuli za Bunge na kutoa mwito kwa marais wastaafu na maspika wastaafu kwa umoja wao kusaidia kulishauri Bunge njia nzuri zaidi ya kurejea katika misingi ya Kitanzania ili tumaini lililojengeka kwenye nyoyo za watu lisififie.
Padri Mwaja alisema wastaafu haswa marais na maspika ni hazina kubwa kwa Taifa, ambao wanaweza kutumika kama kisima cha hekima kwa taifa ili kutoa ushauri bora wa namna ya kurejea katika misingi ya kizalendo ya kitanzania na si kama mambo yanavyoendeshwa bungeni hivi sasa.

Hakuna maoni: