Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga aliyasema hayo jana Dar es Saalam wakati akizungumzia matatizo wanayoyapata Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.
“Kati ya Machi hadi Mei 2016, balozi zetu nchini India na Malaysia zimepokea maombi ya kusaidia kuwarejesha nyumbani Watanzania ambao walipelekwa nchini India na Thailand kwa ahadi za kupatiwa ajira ambazo hutolewa na watu wasio waaminifu ambao wanashukiwa kujihusisha na mtandao wa biashara ya kusafirisha binadamu,” alisema Kasiga.
Alisema mtandao huo unawatafuta wasichana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 na hata chini ya umri huo na kuwalaghai kuwa kuna fursa za ajira katika hoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani nchi za nje na kuwawezesha kupata hati za kusafiria na tiketi ya ndege kwa ajili ya kusafiri kwenda kwenye nchi husika.
“Wengi huvutika kirahisi kwa kuona hiyo ni fursa ya kujipatia kipato ila kwa taarifa tulizopata ni kwamba wengi hujua mapema kuhusu kazi wanayoenda kuifanya huko ila ugumu wa maisha unapelekea kurubuniwa na kuingia kwenye matatizo makubwa,” alifafanua msemaji huyo.
Alisema nchini India peke yake, kuna Watanzania takribani 500 wengi wao wakiwa New Delhi (350), Bangalore (45), Mumbai (20) na wengine wanaelekea Goa. Alisema kwa upande wa Mashariki ya Kati, kumekuwa na wimbi kubwa la wasichana kurubuniwa kwa kutafutiwa fursa za kwenda katika nchi za Oman, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu hasa Dubai kufanya kazi za ndani.
“Baadhi ya wahanga wamekuwa wakikimbilia kwenye ofisi zetu za ubalozi kuomba msaada na balozi zimekuwa zikiwahifadhi ubalozini na kisha kuwasiliana na jamaa zao ili wawatumie nauli na kurejea nyumbani,” alisema.
Alisema wizara imekuwa ikipokea maombi kutoka ofisi za ubalozi nchi za Asia na Mashariki ya Kati ili kuwasaidia wasichana hao kurejea nchini, na hivi karibuni kutoka Ubalozi wa Oman kulikuwa na wasichana 18 kati yao 10 wamesaidiwa kurudi na kuunganishwa na familia zao na Ubalozi wa India wasichana 15 wamepeleka maombi yao.
Aliyataja matatizo yanayowakabili Watanzania nchi za Mashariki ya Kati na Asia kuwa ni pamoja na kulazimishwa ukahaba na kunyang’anywa hati za kusafiria ili kuwadhibiti wasitoroke na wengine kujikuta kukubali kufanya ukahaba ili kurejesha gharama za kuwasafirisha pamoja na kupata nauli.
Matatizo mengine ni kufanya kazi bila mikataba, kufanya kazi nyingi ambazo zingetakia kufanywa na zaidi ya watu wawili au watatu, kufanya kazi kwenye familia zaidi ya moja tofauti na makubaliano, kufanya kazi bila muda maalumu wa kupumzika, kunyanyaswa na kubaguliwa na kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kupigwa, kutopewa fursa ya kuwasiliana na mtu yeyote pamoja na kunyanyaswa kijinsia.
Alisema serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kutafuta majina ya wahusika wote wa mtandao huo na kufanya mawasiliano na serikali za nchi hizo ili kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika mkono wa sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni