ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 30 Juni 2016

NEC yaanza mkakati wa kuhamia Dodoma



Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetekeleza kwa haraka agizo la Rais John Magufuli la kujenga Ofisi Kuu ya Tume baada ya jana kuoneshwa kiwanja katika eneo la Iyumbu katika Manispaa ya Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva, amesema katika uchaguzi zijazo wataanza shughuli za usimamizi wakiwa Dodoma.
“Katika Uchaguzi Mkuu ujao, wapambe wa wagombea watakaa nje ya viwanja hivi wakiwasubiri watu wao wachukue fomu, huu ni mwanzo wa safari yetu ya kuhamia rasmi mjini Dodoma,” alisema Jaji Lubuva akionesha kiwanja hicho ambacho kimenunuliwa kutoka Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA).
Akizungumza baada ya kukagua eneo la ekari 10 litakalotumika kujenga ofisi hizo, Lubuva alisema huo ni mwanzo wa safari ya kuhamia Dodoma na katika chaguzi zinazokuja wataanzia shughuli za usimamizi wa uchaguzi hapo.
“Uchaguzi zijazo tutaanza shughuli za usimamizi wa uchaguzi kutoka Dodoma...Mimi na makamishna wa Tume tumefika hapa kukiona kiwanja ni kizuri tumekinunua kwa shilingi milioni 470 kwa upande wa tume tumeridhika,” alisema Lubuva.
Alisema lengo hilo lilikuwa la muda mrefu kuwa na jengo la kutosheleza mahitaji kwani sasa ofisi ya tume hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam ina ofisi tatu maeneo matatu tofauti lakini sasa wanatakiwa kufanya kazi eneo moja.
“Wale wa mwanzo kuhamia Dodoma tutakuwa ni sisi na huko mbele chaguzi zijazo tutakuwa katika majengo yetu,” aliongeza Mwenyekiti huyo wa NEC siku chache baada ya Rais Magufuli kuwataka kutafuta eneo la kujenga ofisi yao baada ya kuwapa Sh bilioni 12 ambazo ni bakaa la Uchaguzi Mkuu uliopita.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhani alisema katika Uchaguzi Mkuu uliopita walibakiza fedha kiasi cha Sh bilioni 12 ambazo walimrudishia Rais Magufuli kwa ajili ya matumizi mengine na rais aliwarudishia huku akiwataka wajenge jengo lao.
Kailima alisema eneo hilo lina miundombinu yote na wameanza mazungumzo la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ili ifikapo Oktoba ujenzi uanze na baada ya mwaka mmoja tume iwe na jengo lake.

Hakuna maoni: