ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatatu, 27 Juni 2016

Makinda: Wanawake viongozi kuweni chachu kwa wengine


Imeandikwa na Mwandishi Wetu

WANAWAKE waliopata nafasi za uongozi katika Bodi za Wakurugenzi kwenye mashirika na kampuni mbalimbali nchini, wamehimizwa kuonesha umahiri katika kazi ili kuwavutia wanawake wengine kufuata nyayo zao.
Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda, alisema wanawake katika ngazi za juu wana nafasi nzuri kuonesha njia kwa wenzao kufikia mafanikio.
Alikuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya Madola uliolenga kujadili na kushawishi wanawake kuingia kwenye uongozi.
“Ingawa katika nafasi za siasa na bunge hali si mbaya, takwimu zinaonesha wanawake wenye nafasi za uongozi kwenye Bodi za Wakurugenzi nchini ni ndogo,” alisema.
Alisema, jambo la msingi kwa waliopata fursa ni kufanya kazi vizuri na kuwa chachu kwa wengine kujitokeza na kuingia katika nafasi hizo.
Aliitaka Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania itumike kuwaelimisha na kuwashawishi wanawake wengine wasio viongozi kufikia nafasi hizo.
“Kwa sasa wanawake wengi wana elimu ya kutosha, lakini bado wana tatizo la kujiamini,” alisema na kuongeza kuwa, mikutano kama hiyo inawapa moyo wa kujiamini na kutaka kushika nafasi hizo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania, Said Kambi alisema, mkutano huo ulikuwa wa mafanikio makubwa na ulichokoza majadiliano na midahalo ya wanawake hapa nchini.
Alisema, wameanzisha kikosi kazi ambapo majumuisho yote yatapelekwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ili yafanyiwe kazi na kuongeza kuwa taasisi hiyo itashirikiana kwa karibu na kikosi kazi hicho.
Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Uratibu Uwezeshaji wa Wanawake katika fursa za uongozi Tanzania, Margareth Chacha, alisema wamejiandaa kuweka mikakati ya kuwaondolea woga wanawake na kuwasaidia katika nyanja mbalimbali.
Naye mmoja wa wajumbe, Dk Marina Njelekela alisema bado kazi kubwa inatakiwa kufanywa ili kuongeza mchango wa mwanamke katika maendeleo ya uchumi.
Mkutano huo uliandaliwa na Jumuiya ya Madola kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Watoto, Mamlaka ya Hisa na Uwezeshaji Mitaji na Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania.

Hakuna maoni: