ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 15 Aprili 2016

TAKUKURU yakabidhiwa Kampuni ya Lugumi


Image result for valentino mlowola
picha :Mkurugenzi Mkuu Takukuru-Valentino Mlowola
Sakata la kampuni ya Lugumi iliyoingia mkataba wa Sh37 bilioni na Jeshi la Polisi wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole nchi nzima, sasa limetua Takukuru baada ya taasisi ya kupambana na rushwa kuchukua faili lake la usajili.

Kampuni hiyo ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati ya 108 ilizotakiwa kufunga, licha ya kulipwa  asilimia 99 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo.

Wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikitaka nguvu itumike ili Jeshi la Polisi liwasilishe mkataba huo, utata umeibuka katika umiliki wa kampuni hiyo kutokana na kuwepo tuhuma kuwa baadhi ya vigogo wa Polisi na wanasiasa ni wanahisa wa Lugumi Enterprises.

Jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Frank Kanyusi alisema kuwa Takukuru inashughulikia suala hilo, huku akibainisha kuwa kwa sasa Brela hawana takwimu za kina za kampuni hiyo.

“Kampuni hii ilisajiliwa kihalali na kupewa cheti cha usajili. Ila ninachoweza kukueleza kwa sasa ni kwamba jalada la usajili la Lugumi lipo Takukuru kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Kinyusi jana.

Kanyusi, ambaye hakutaka kuzungumzia kiundani kuhusu usajili wa kampuni hiyo, alisema: “Waandishi wa habari wamekuwa wakiniuliza maswali mengi kuhusu suala hili ila kwa sasa hali ndiyo hiyo. Jambo hili lipo Takukuru.”

Alisema kwa sasa kampuni zilizosajiliwa na Brela zipo 120,000 na zinakaribia kufika 130,000 na kwamba kampuni lazima zitoe taarifa zake kila mwaka, kinyume na hapo zinaweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutwa.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Brela zilieleza  kuwa taarifa za usajili wa kampuni hiyo zilitoweka takribani miezi miwili iliyopita.

Mwandishi  alipofika katika ofisi za wakala huyo kwa ajili ya kupata ukweli wa usajili, alielezwa na mmoja wa watumishi ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi kwamba ni vigumu kupata hilo jalada kwa sababu ya mvutano ulioibuka.

Hata baada ya kufuata taratibu za kupewa jalada hilo kwa ajili ya kupitia masuala mbalimbali, alijibiwa kuwa jalada hilo halionekani ingawa baadaye Kanyusi alisema limechukuliwa na Takukuru.

Sakata la Lugumi liliibuka wiki iliyopita wakati PAC ilipokutana na Jeshi la Polisi kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na CAG.

Katika hesabu hizo ilibainika kuwa mwaka 2011, Polisi iliingia mkataba na Lugumi kwa ajili ya kufunga mashine hizo katika vituo 108 vya polisi kwa gharama ya Sh 37 bilioni.

Hata hivyo, ilibainika kuwa kampuni hiyo imefunga mitambo hiyo kwenye vituo 14 tu, huku ikilipwa asilimia 99 ya fedha hizo.

Kutokana na ukakasi huo, PAC ambayo ilibaini viashiria vya ufisadi katika mkataba huo, iliagiza watendaji wa Polisi kuwasilisha taarifa za mkataba huo pamoja na vielelezo vyake ili kamati hiyo iweze kuupitia na kujiridhisha.

Lakini hadi sasa Jeshi la Polisi halijawasilisha mkataba huo, jambo ambalo huenda likazua mjadala mkali katika mkutano wa Bunge unaoanza Jumanne ijayo.

Hakuna maoni: