ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 29 Aprili 2016

Kilombero watafakari ongezeko la maji

SERIKALI ya Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro imejipanga kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza endapo kivuko cha Mv Kilombero II kitasimama kutoa huduma kutokana na maji katika mto Kilombero kufikia kiwango cha ujazo wa mita 90 kutoka usawa wa bahari.
Mkakati huo unatokana na kuendelea kunyesha kwa mvua za masika hali itakayosababisha mto Kilombero kujaa maji na kukifanya kivuko hicho kusitishwa kuendelea kufanya kazi zake.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya kikao cha Afya ya Msingi Mkoa kilichofanyika mjini Morogoro.
“Hadi leo (jana) maji katika mto Kilombero yamefikia ujazo wa mita 60 kutoka usawa wa bahari na ili Kivuko cha Mv Kilombero kisimame kufanya kazi ni pale ujazo wa maji utakapofikia mita 90 kutoka usawa wa bahari,” alisema Gembe na kuongeza: “Kwa sasa bado kiwango cha ujazo wa maji mto Kilombero ni mita 60 kutoka usawa wa bahari na kufanya Kivuko cha Mv Kilombero II kiendelee utoaji wa huduma na tunaomba mvua hizi zisizidi kupita kiwango hicho.”
Alisema Kivuko cha Mv Kilombero II bado kinaendelea kufanya kazi za uvushaji wa abiria, mizigo na magari kulingana na taratibu zilizowekwa.

Hakuna maoni: