Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema vijana wake wameiva vya kutosha na ana matumaini makubwa ya kupata ushindi mnono.
Alisema kwa namna ambavyo wachezaji wake wanavyotimiza majukumu yao vizuri kwenye mazoezi Uwanja wa Gombani, ana uhakika ushindi lazima na mashabiki wasiwe na hofu.
“Nafarijika kuona vijana wangu wakitimiza kikamilifu majukumu yao katika mazoezi ambayo tunawapa, kila mchezaji amekuwa akionesha bidii kwa anachotakiwa kufanya, jambo hili linatupa matumaini na kuamini tuna uwezo wa kushinda ingawa ni vigumu kutabiri idadi ya mabao, lakini yatakuwa ya kutosha,” alisema Mwambusi.
Kocha huyo ambaye anamsaidia Mholanzi Hans Pluijm, alisema katika siku tatu zilizobaki kabla ya mchezo huo wamepanga kuwafundisha wachezaji vitu vichache ambavyo ni muhimu vitakavyowapatia matokeo mazuri.
Alisema wanaelekea kwenye mchezo huo wakiwa na furaha baada ya idadi kubwa ya wachezaji wao kuwa fiti kwa ajili ya pambano hilo isipokuwa kiungo Haruna Niyonzima ambaye hatacheza kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.
“Ukimtoa Niyonzima, wachezaji wengine wote wapo katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo huo, akiwemo Juma Abdul na Nadir Haroub `Cannavaro’…,” alisema Mwambusi na kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi Jumamosi kuwashangilia wakiwa na imani kwamba hawatawaangusha.
Alisema wanataka kushinda ili watakaporudiana ugenini mambo yasiwe magumu zaidi na kusisitiza kuwa ushindi ni lazima kwa mchezo wao.
Zitarudiana wiki ijayo huko Misri. Yanga ilifikia hatua ya raundi ya pili baada ya kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius katika mchezo wa raundi ya awali kwa jumla ya mabao 3-0 na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.
Lakini jana Pluijm (pichani) alikaririwa akisema ushindi katika mchezo huo utategemea na namna wachezaji watakavyojituma na kucheza kama wanavyoelekezwa kutokana na siku za karibuni washambuliaji wake kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini wanashindwa kuzitumia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni